Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo, PCPM inasema, itaendelea kushirikiana na Mabaraza ya Maaskofu na Mashirika ya Kitawa katika kujenga mazingira bora zaidi ya malezi na makuzi. Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo, PCPM inasema, itaendelea kushirikiana na Mabaraza ya Maaskofu na Mashirika ya Kitawa katika kujenga mazingira bora zaidi ya malezi na makuzi. 

Tume ya Kipapa PCPM: Yaliyojiri kwenye Mkutano Mkuu wa 2019

Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo, PCPM inasema: Itaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, Mashirika ya kitawa na kazi za kitume pamoja na vyama na mashirika ya kitume iili kujenga utamaduni wa ulinzi na usalama kwa ajili ya malezi na makuzi ya watoto na vijana katika mazingira ya Kikanisa. Maadili na utu wema!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP. S. – Vatican.

Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo, PCPM, imehitimisha mkutano wake mkuu wa XI ulioadhimishwa hapa mjini Vatican kuanzia tarehe 12-15 Septemba 2019. Wajumbe walipata fursa ya kusikiliza shuhuda za mateso, mchakato wa uponyaji na msamaha kutoka Brazil kwa mtu ambaye alinyanyasika kwanza kabisa ndani ya familia yake na hatimaye, akajikuta anatumbukia pia hata katika nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Ushuhuda huu ni kuwawezesha wajumbe kutambua kwamba, wamepewa dhamana na utume na Mama Kanisa katika mchakato wa kuhakikisha kwamba, watoto na vijana wanakuwa na mazingira ya malezi na makuzi bora zaidi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na maisha yao ya kiroho na kimwili. Wajumbe wa Kamati, kabla ya mkutano wao, wamepata nafasi ya kutembelea Mabaraza mbali mbali ya Kipapa ili kujenga ushirikiano na mafungamano kwa ajili ya ufanisi na utekelezaji bora wa dhamana na majukumu yao ndani ya Kanisa.

Tume inajielekeza zaidi kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa nyanyaso za kijinsia; malezi, makuzi na elimu sanjari na kutoa sheria, kanuni, taratibu na miongozo. Tume inaendelea kusikiliza shuhuda na ushauri kutoka kwa watu mbali mbali kama sehemu ya mchakato unaopania kuganga, kuponya na kusaidia upatanisho. Tume itaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, Mashirika ya kitawa na kazi za kitume pamoja na vyama na mashirika ya kitume iili kujenga utamaduni wa ulinzi na usalama kwa ajili ya malezi na makuzi ya watoto na vijana katika mazingira ya Kikanisa. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake ya Mwaka mpya kwa Mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Baba Mtakatifu anasema, Jumuiya ya Kimataifa kwa Mwaka 2019 inaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 30 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza haki msingi za watoto; utu na heshima yao kama binadamu.

Watoto wajengewe mazingira mazuri ya maisha, kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao kiroho na kimwili. Kanisa pia linaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 30 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka wa “Mulieris dignitatem” yaani “Utu na wito wa wanamke”. Amekazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa ni jukwaa na wajenzi wa amani, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Jumuiya ya Kimataifa. Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia inaundwa na Makleri pamoja na waamini walei, kutoka sehemu mbali mbali za dunia.  Tume hii ni msaada mkubwa kwa Baba Mtakatifu Francisko katika utekelezaji wa utume wake kwa kuhakikisha kwamba, watoto na vijana wanaishi katika mazingira yenye usalama, amani na utulivu kwa ajili ya makuzi na majiundo yao kiroho na kimwili.  Tume hii ya Kipapa ni mwendelezo wa utekelezaji wa sera na mikakati iliyoanzishwa na watangulizi wake katika kulinda watoto na vijana dhidi ya nyanyaso za kijinsia ambazo zilijitokeza katika miaka ya hivi karibuni na hivyo kuchafua utume na maisha ya Kanisa. Huu pia ni utekelezaji wa ushauri uliotolewa na viongozi wa Kanisa na wataalam katika masuala ya malezi na makuzi ya watoto.

Tume: Ulinzi watoto
17 September 2019, 11:00