Tafuta

Siku kuu ya Kutukuka kwa Msalaba inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 14 Septemba Siku kuu ya Kutukuka kwa Msalaba inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 14 Septemba 

Siku kuu ya Kutukuka kwa Msalaba, 14 Septemba: Huruma & Upendo wa Mungu kwa binadamu

Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu: Ni kilele cha ufunuo wa: huruma, upendo, ukuu, utukufu na utakatifu wake, changamoto kwa Wakristo ni kushikamana pamoja na Kristo katika mapambano, ili siku moja waweze kushinda pamoja naye! Huu ndio ujumbe wa matumaini unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba, mwaliko wa: kumtafakari Kristo mfufuka ni kiini cha imani na matumaini ya Kikristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 14 Septemba, anaadhimisha Siku kuu ya Kutukuka kwa Msalaba “Exaltatio Sanctae Crucis” kwa lugha ya Kilatini. Fumbo la Msalaba linayagusa maisha ya mwamini kwa namna ya pekee. Msalaba katika mapokeo ya kale, ilikuwa ni alama ya uovu wa kutisha na hali ya kukatisha tamaa, lakini, kwa njia ya Yesu Kristo Mkombozi wa dunia, Msalaba umepata maana mpya katika maisha ya mwanadamu; sasa ni kielelezo cha ushujaa wa  Kristo Yesu na mashuhuda wa imani wanaoendelea kuteseka pamoja na kuyamimina maisha yao kwa ajili ya imani yao kwa Kristo na Kanisa lake sehemu mbali mbali za dunia. Siku kuu ya Kutuka kwa Msalaba inapata chimbuko lake kunako mwaka 335 Mfalme Costantino alipojenga Makanisa makuu mawili na kwa mara ya kwanza akawaonesha watu Masalia ya Msalaba Mtakatifu. Hata hivyo, hii ni Siku kuu yenye ukuu na maana yake kwani inadhihirisha kuwa Msalaba wa Kristo ni chombo cha wokovu na utukufu wa Mungu; ni siku ambayo Msalaba wa Kristo unang’ara duniani!

Badala ya kashfa na utupu, Msalaba unakua ni chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Ni ishara ya mapendo, neema, sala, msamaha, upatanisho na matumaini. Ni kutokana na maana hii mpya, Mama Kanisa anaona fahari kuu kuutangaza utukufu na kuimba sifa kuu za Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Msalaba unaendelea kumfunza mwamini kwamba, hakuna mapendo kamili yasiyokuwa na mateso na matumaini ya uzima wa milele. Changamoto kwa waamini katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo ni kuuangalia, kuutafakari, kuushangaaa, kuusikiliza, kuheshimu, kuutukuza na kuuabudu kwa imani, matumaini na mapendo, kwani ni kielelezo ambacho wokovu wa dunia umetundikwa juu yake! Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu yaani: Mateso, kifo na ufufuko wake ni kilele cha ufunuo wa: huruma, upendo, ukuu, utukufu na utakatifu wake, changamoto kwa Wakristo ni kushikamana pamoja na Kristo katika mapambano, ili siku moja waweze kushinda pamoja naye!

Huu ndio ujumbe wa matumaini unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika Fumbo la Msalaba, mwaliko kwa waamini kumtafakari Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kuwa ni kiini cha imani ya Kikristo. Waamini watambue ukuu wa Msalaba na wala si tu kama kito cha thamani wanachovaa shingoni au kupamba majumbani mwao, bali ni dira na mwaliko wa kuutafakari upendo wa Yesu aliyejisadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Siku kuu ya Kutukuka kwa Msalaba iwasaidie waamini kutambua na kuthamini ukuu wa Msalaba, madhara ya dhambi na thamani ya mateso ya Kristo Yesu Msalabani kwa ajili ya ukombozi wa watu wote. Fumbo la Msalaba ni alama ya upendo wa Mungu kwa binadamu; kielelezo cha sadaka ya hali ya juu kabisa ya Kristo dhidi ya ukosefu wa haki msingi za binadamu; ubinafsi, dhuluma na nyanyaso. Msalaba ni alama ya ushindi dhidi ya kifo. Msalaba ni kielelezo cha mateso, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo wanaouwawa kikatili kwa kuchomwa moto wangali hai; na wakati mwingine nyanyaso na dhuluma hizi zinatendwa katika hali ya ukimya mkubwa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Msalaba unatisha, kama ilivyojionesha hata kwa Mitume wa Yesu, waliotaka kukimbia madhulumu ya Nero; Petro kwa mshangao mkubwa akakutana na Yesu njiani akielekea mjini Roma ili aweze kusulubishwa mara ya pili; hapo ndipo Mtume Petro alipoishiwa nguvu, akapiga moyo konde na kufuata nyayo za Kristo, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake juu ya Msalaba kwa kutambua kwamba, Yesu alikuwa amempenda upeo! Baba Mtakatifu anasema, kwa njia ya Msalaba, Yesu anajiunga na wale wote wanaodhulumiwa na kuteswa; watu ambao hawana tena nguvu ya kupiga kelele; hasa watu wasiokuwa na hatia wala ulinzi madhubuti; familia zinazokabiliana na hali ngumu ya maisha; wale wanaolia na kuomboleza kwa kuondokewa na wapendwa wao katika maisha; wanaowalilia watoto wao waliotumbukia katika matumizi haramu ya dawa za kulevya.

Kwa njia ya Fumbo la Msalaba, Yesu anaungana na mamillioni ya watu wanaoteseka kutokana na baa la njaa wakati ambapo kuna sehemu nyingine za dunia wanakula na kusaza! Anajiunga na wale wanaoteswa na kudhulumiwa kutokana na imani, mawazo na rangi ya ngozi. Yesu anaendelea kujiunga na umati mkubwa wa vijana uliopoteza dira, mwelekeo na matumaini ya maisha kutokana na wanasiasa wanaowaongoza kuelemewa mno na ubainfsi, rushwa na ufisadi. Yesu anaendelea kuungana kwa njia ya Fumbo la Msalaba na waamini ambao wamepoteza imani yao kwa Mungu na Kanisa kutokana na kashfa na utepetevu wa imani ulioneshwa na watumishi wa Injili. Yesu anayapokea yote haya kwa mikono miwili na kujitwika mabegani mwake pamoja na Misalaba ya wafuasi wake, tayari kuwaambia, jipeni moyo kwani yuko pamoja nao na kwamba, ameshinda dhambi na mauti na yuko kati yao ili kuweza kuwakirimia matumaini na maisha tele!

Fumbo la Msalaba ni mwaliko kwa kila mwamini kuwa kama Simoni wa Kirene, aliyemsaidia Yesu kubeba Msalaba, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria na kwa wanawake wengine watakatifu, waliopiga moyo konde, wakaifuata ile njia ya uchungu wakiwa wamesheheni upendo na huruma hadi chini ya Msalaba.

Kutukuka kwa Msalaba

 

13 September 2019, 11:53