Tafuta

Vatican News
OSCE yapembua kuhusu: Utunzaji bora wa mazingira, utawala bora, ulinzi na usalama miongoni mwa nchi wanachama! OSCE yapembua kuhusu: Utunzaji bora wa mazingira, utawala bora, ulinzi na usalama miongoni mwa nchi wanachama! 

OSCE yazungumzia: Mazingira, Utawala Bora, Ulinzi & Usalama!

Askofu mkuu Charles Balvo amesema, miongoni mwa mada zilizojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na suala la mazingira ndani ya nchi wanachama wa OSCE, utawala bora, ulinzi na usalama. Ushirikiano wa kimataifa ni muhimu katika kukabiliana na changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza katika masuala ya ulinzi, usalama na mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu.

Na Padre Angelo Shikombe, - Vatican.

Askofu mkuu Charles Daniel Balvo, Balozi wa Vatican nchini Czech amempongeza  Rais wa Shirikisho la Ushirikiano wa Kimataifa, Usalama na Maendeleo, OSCE, kwa maandalizi na hatimaye, maadhimisho ya mkutano wa 27 wa OSCE, uliohitimishwa hivi karibuni huko  mjini Prague. Askofu mkuu Charles Balvo amesema, miongoni mwa mada zilizojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na suala la mazingira ndani ya nchi wanachama wa OSCE, utawala bora, ulinzi na usalama. Ushirikiano wa kimataifa ni muhimu katika kukabiliana na changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza katika masuala ya ulinzi na usalama sanjari na mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Akifafanua hayo kutoka katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, amesisitiza kwamba, kuna muunganiko mkubwa kati ya ustawi wa mazingira, na ulinzi wa jamii.

Changamoto ya kimazingira haiwezi kutenganishwa na madhara ya kiuchumi yanayosababishwa na uharibifu wa mazingira pamoja na kuporomoka kwa kanuni maadili na utu wema, hivyo Shirikisho hilo halina budi kukuza  hatua za kuboresha mazingira na kurekebisha mienendo ya maisha ya watu. Hiyo ndiyo shauku ya Vatican na Vatican inasubiri kwa hamu kubwa hitimisho la hatua ya pili ya utekelezaji wa mikakati ya utunzaji bora wa mazingira.   Pia Vatican ingependa kuziona nchi wanachama wa OSCE zikitekeleza kwa haraka malengo waliyojiwekea. Katika mkutano huo suala la uongozi bora lilipewa kipaumbele katika masuala ya kiuchumi na kimazingira. Pamoja na athari za utandawazi katika ueledi wa uongozi, taarifa ya mwaka 2019 kutoka Shirika la mazingira Ulaya (EEF) zimetoa upekee wa muunganiko kati ya uongozi bora, nguvu ya ulinzi, na majadiliano.  Sehemu ya 5 na 6 ya mkutano  huo imejikita katika kubaini maswali na kuyafanyia utafiti. Aidha Vatican imedokeza kuwa kukosekana kwa ushirikiano kati ya Serikali na jamii kutadhoofisha ukuaji wa kiuchumi na teknolojia.

Madhara makubwa yanasababishwa na rushwa na ufisadi wa mali ya umma; mambo yanayodumaza uwezo wa ukuaji wa kiuchumi na athari zake tayari zimeanza kuonekana Barani Ulaya. Hata hivyo,  umoja bado unahitajika  kati ya jamii za kisiasa na asasi zisizo za kiserikali, ili kupambana na rushwa katika matumizi ya fedha na kuhamasisha utawala bora na uwajibikaji wa pamoja katika utengenezaji wa sheria na miundo mbinu ya uhakika. Lengo  likiwa ni kufikia utamaduni fungamano.  Changamoto ya pili ni  pale utawala unaposhindwa kuwa makini, wazi na kukosa uwajibikaji.  Kutokana na hilo inalazimika kuweka miundo mbinu yenye kulinda: mafao, ustawi na maendeleo ya wengi.  Mwishoni, Charles Daniel Balvo, Balozi wa Vatican nchini Czech amewashuru kwa maandalizi na kuwaahidi ushirikiano kutoka Vatican.

Askofu mkuu Balvo

 

18 September 2019, 15:21