Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anasema kuwa thamani ya mawasiliano ni urithi wa kumbukumbu. Baba Mtakatifu Francisko anasema kuwa thamani ya mawasiliano ni urithi wa kumbukumbu.  (AFP or licensors)

Papa Francisko:Thamani ya mawasiliano ni urithi wa kumbukumbu!

Tarehe 28 Septemba 2019 imetangazwa Kauli mbiu ya Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko wa siku ya 54 ya Upashanaji habari duniani 2020, usemao “ili mpate ninyi kuwasimulia watoto wenu na wajukuu wenu:maisha huwa historia”. Mada hii, imechukuliwa kutoka kifungu cha Kitabu cha Kutoka, 10, 2.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Ili mpate ninyi kuwasimulia watoto wenu na wajukuu wenu:maisha huwa historia. Ndiyo kauli mbiu iliyochaguliwa  na Baba Mtakatifu Francisko katika  ujumbe wa Siku ya 54 ya Upashanaji habari duniani 2020, siku ambayo itaadhimishwa tarehe 24 Januari katika siku ya kumbukumbu ya Mtakatifu Francisko wa Sales, Msimamizi wa Vyombo vya habari Katoliki. Kwa uchaguzi wa mada hii yenye sehemu iliyochukuliwa kutoka kifungu cha Kitabu cha Kutoka, 10, 2, Baba Mtakatifu Francisko anaelezea kwa namna ya pekee jinsi urithi wa kumbukumbu ulivyo muhimu sana katika mawasiliano. Mara nyingi Baba Mtakatifu Francisko amesisitiza kwamba hakuna wakati ujao bila mizizi ya historia ya kuishi. Na inatusaidia kuelewa kwamba kumbukumbu haipaswi kuzingatiwa kama mwili uliotulia, bali ni ukweli wa nguvu inayozunguka. Kupitia kumbukumbu ndipo kuna uwasilishaji wa hadithi, matumaini, ndoto na uzoefu kupitia kizazi kimoja hadi kingine.

Kila hadithi inazaa maisha katika kukutana na mwingine

Mada ya siku ya Upashanaji habari duniani inatukumbusha kuwa kila simulizi  au hadidhi kunazaliwa maisha, kwa njia ya  kukutana na mwingine. Mawasiliano kwa njia hiyo yanaalika kuunganisha kumbukumbu na maisha kupitia hadithi. Yesu alitumia mifano ili kuwasilisha nguvu muhimu ya Ufalme wa Mungu, akiwaachia wasikilizaji wawe na uhuru wa kupokea simulizi hizo pia kuzirejesha zenyewe. Hata hivyo nguvu ya historia inajieleza kwa uwezo wa kutoa mabadiliko. Hadithi yenye mfano hai ina nguvu ya kubadilisha. Tunapata uzoefu tunapokutana na kubadilishana mawazo , kupitia hadithi na maisha ya watakatifu. Na ndiyo hoja ambayo, hivi karibuni  Baba Mtakatifu ameitoa wakati akihutubia Baraza la Kipapa la Mawasiliano Vatican, hasa aliposhauri kuwasilisha utajiri mkubwa ambao unatolewa na ushuhuda wa maisha ya watakatifu.

Kupasha habari ni nyenzo kwa ajili ya kujenga madaraja

Katika kiini cha tafakari ya Baba Mtakatifu Francisko anapendeza kumweka katikati mtu na mahusiano yake na uwezo wake wa ndani wa kuwasiliana. Baba Mtakatifu Francisko anawaomba kila mtu bila ubaguzi, kufanya talanta hiyo izae  matunda. Kufanya mawasiliano kuwa chombo cha kujenga madaraja, kuungana na kushirikisha  uzuri wa kuwa ndugu katika wakati wa sasa unaoonesha uwepo wa utengano na mgawanyiko.

28 September 2019, 15:57