Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amewateua makardinali watatu kuwa marais wawakilishi wa Sinodi Maalumu ya Maaskofu kwa ajili ya Ukanda wa Amazonia inayotajiwa kuanza Oktoba ijayo Baba Mtakatifu Francisko amewateua makardinali watatu kuwa marais wawakilishi wa Sinodi Maalumu ya Maaskofu kwa ajili ya Ukanda wa Amazonia inayotajiwa kuanza Oktoba ijayo  (AFP or licensors)

Papa awateua marais 3 kuwa wawakilishi wa Sinodi Maalum ya Ukanda wa Amazonia,Oktoba ijayo!

Baba Mtakatifu Francisko amewateua mardinali watatu kuwa marais wawakilishi,ambao watakuwa na wajibu wa kuongoza kazi ya Sinodi Maalum ya Amazonia inayotarajiwa kufanyika Oktoba ijayo mjini Vatican.Makardinali hawa ni Porras Cardozo,(Venezuela)Kardinali Barreto Jimeno(Peru) na Kardinali Braz de Aviz(Brazil).

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Katika matarajio ya Sinodi Maalum ya Maaskofu wa Ukanda wa Amazonia inayotarajiwa kufanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 6 hadi 27 Oktoba 2019, kwa kuongozwa Kauli mbiu:“Amazonia:njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya maendeleo fungamani”, tarehe 7 Septemba 2019, Baba Mtakatifu Francisko, amewateua Kardinali Baltazar Enrique Porras Cardozo msimamizi wa kitume  kwa jimbo la Carcas ambaye ni Askofu Mkuu wa  Jimbo Kuu Katoliki la Mérida (Venezuela); Kardinali Pedro Ricardo Barreto Jimeno Askofu Mkuu wa Jimbo kuu katoliki la Huancayo (Perù) na Makamu Rais wa Mtandao wa Kanisa Ukanda wa Amazonia (REPAM, pamoja na  Kardinali João Braz de Aviz,(Brazil) na Rais wa Baraza la kipapa la Mashirika ya Kitawa na vyama vya Kitume kuwa marais wawakilishi wake kwenye Sinodi hii tarajiwa.

Hata hivyo uteuzi huo umetanguliwa  mwezi Mei mwaka huu, ambapo Baba Mtakatifu Francisko alimteua Kardinali Claudio Hummes, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Sao Paulo, Brazil, ambaye pia aliwahai kuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri kuwa Mwezeshaji mkuu wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, pamoja na Askofu David M. De Aguirre Guinea na P. Michael Czerny, ambaye ni Katibu mkuu msaidizi, Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi na Baraza ya Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu kuwa Makatibu maalum wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia.

Hatua za maandalizi ya Sinodi maalum, zinapamba moto

Hatua zote za maandalizi tayari zimekwisha kutekelezwa na pia Hati ya Maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia iko tayari.  Katika Hati ya maandalizi ya Sinodi ya Amazonia inakazia umuhimu wa: kuona, kung'amua na kutenda. Ni Sinodi ambayo itakijita kwa kina kupembembua tema mbali mbali kuhusu: haki jamii, malezi ya awali na endelevu, katekesi makini, liturujia na utambulisho wa Kanisa katika Ukanda wa Amazonia. Hati ya Kutendea Kazi: “Instrumentum Laboris” ilipitishwa na  Wajumbe Washauri wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Hati hii imegawanyika katika Sehemu Kuu III, kwa kuanza na utangulizi pamoja na hitimisho lake. Na kwa maelezo zaidi juu ya hati ya kitendea kazi soma habari hii:  https://www.vaticannews.va/sw/vatican-city/news/2019-08/sinodi-maaskofu-ukanda-amazonia-2019-padre-michael-czerny-unabii.html

Ijue nafasi ya rais mwakilishi katika Sinodi

Je nafasi ya rais mwakilishi ni nini? Sinodi ya Maskofu iko chini ya Baba Mtakatifu ambaye ni rais wake. Na kabla ya kuanza Sinodi  Baba Mtakatifu huchagua marais wawakilishi ambao wanasimamia uendeshaji wa kazi kwa niaba yake. Kwa mujibu wa mpango wake (Ordo Synodi Episcoporum), Kanuni ya Sinodi ya Maaskofu iliyosasishwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kunako 2006, rais mwakilishi, anayo majukumu ya kuongoza sinodi, kwa kushirikiana na wajumbe wa kazi maalum, ili Sinodi iweze kuendesha kazi yake kwa ubora, na kutia sahihi katika hati za Mkutano. Na ikiwa mada, iliyojadiliwa katika Sinodi, inahitaji kuitazama kwa kina  zaidi, ni  shughuli ya rais mwakilishi aliyetumwa, kwa idhini ya Papa, kuunda tume maalum ya kuifanyia utafiti zaidi kati ya wajumbe. Maraiswaliotumwa kuwakilisha hufanya kazi hiyo ili kufanikisha kila mmoja kulingana na agizo lililowekwa na Papa, husitishwa shughuli hiyo, mara baada ya kumalizika au kufungwa kwa  Sinodi ambayo wao walikuwa wameteuliwa kuwa wawakilishi.

07 September 2019, 12:38