Tafuta

Vatican News
Baraza la Kipapa la Mawasiliano: Mawasiliano ni kujenga, kuunganisha na kuelekeza! Baraza la Kipapa la Mawasiliano: Mawasiliano ni kujenga, kuunganisha na kuelekeza!  (ANSA)

Baraza la Kipapa la Mawasiliano: Kujenga, kuunganisha & kuelekeza

Utume huu unatekelezwa kwa kuzingatia maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii, ili kuweza kuwafikia walengwa mahali walipo! Ni huduma inayotumia karama na mapaji mbali mbali ambayo wafanyakazi hawa wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu, ili ziweze kuzaa matunda yanayokusudiwa. Lengo kuu la mawasiliano ni kujenga, kuunganisha na kuelekeza. Mawasiliano!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika hotuba yake kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa niaba ya wafanyakazi na wajumbe wa Baraza, zaidi ya 500, Jumatatu, tarehe 23 Septemba 2019, amekazia pamoja na mambo mengine: Umoja wa jumuiya ya wanahabari wanaomzunguka Baba Mtakatifu, rasilimali na umuhimu wake; huduma inayofumbatwa katika kipaji cha ubunifu katika ukweli na unyenyekevu; miradi inayofanyiwa kazi kwa sasa pamoja na changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza kila kukicha! Dr. Ruffini anasema, Baraza la Kipapa la Mawasiliano linaundwa na: wakleri, watawa na waamini walei kutoka katika mataifa mbali mbali, wenye: lugha na tamaduni mbali mbali, kwa pamoja wanashuhudia umoja na mshikamano wa Kanisa, linalotaka kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Utume huu unatekelezwa kwa kuzingatia maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii, ili kuweza kuwafikia walengwa mahali walipo!

Ni huduma inayotumia karama na mapaji mbali mbali ambayo wafanyakazi hawa wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu, ili ziweze kuzaa matunda yanayokusudiwa. Lengo kuu la mawasiliano ni kujenga, kuunganisha na kuelekeza. Baraza linaendelea kuwekeza zaidi katika mawasiliano ili kuunganisha shughuli zinazotekelezwa na Sekretarieti kuu ya Vatican, Kanisa la Kiulimwengu na Makanisa mahalia pamoja na kuwasaidia waamini kuwa na mwelekeo sahihi; kwa waamini wa Makanisa mbali mbali kufahamiana; kwa kuimarishwa katika imani, matumaini na mapendo. Shughuli hii inatekelezwa kwa njia ya: Radio, Luninga, Magazeti pamoja na mitandao ya kijamii, ili kushuhudia imani ya Kanisa inayomwilishwa katika matendo. Huduma hii imeendelea kuwa ni jukwaa la majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Dr. Ruffini anasema vitengo mbali mbali vya mawasiliano vinaendelea kujielekeza kuanzisha miradi itakayoliwezesha Kanisa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayofumbatwa katika: wema, uzuri na haki, ili kukuza na kudumisha uwezo wa waamini katika kufikiri na kutenda.

Ni miradi inayopania kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Makanisa mahalia katika ujumla wake. Mabadiliko mbali mbali ya rasilimali watu na teknolojia yanapania pamoja na mambo mengine kuongeza tija, ufanisi sanjari na kubana matumizi. Licha ya mapungufu ya kibinadamu yanayoweza kutokea, lakini bado Baraza la Kipapa la Mawasiliano limekuwa ni chombo cha kutangaza na kushuhudia ukweli. Linaendeleza mchakato wa mabadiliko ili kuhama kutoka katika “nyumba ya zamani; ili kuanza maisha mapya kwenye “nyumba mpya” pamoja na magumu na changamoto zake. Jambo la kujivunia ni kuona kwamba, Baraza linaendelea kujikita katika ujenzi wa mtandao wa umoja unaopaswa kuboreshwa kila kukicha. Ukweli ni tunu inayolifanya Baraza kuwa na nguvu zaidi, kwa kutambua pia mapungufu yao kibinadamu. Baraza linamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu kwa kuendelea kuunga mkono jitihada mbali mbali za maisha na utume wake.

Dr. Ruffini: Mawasiliano

 

23 September 2019, 16:19