Mwenyeheri Benedetta Bianchi Porro ni shuhuda amini wa Fumbo la Msalaba katika maisha yake, chachu ya kuyatakatifuza malimwengu. Mwenyeheri Benedetta Bianchi Porro ni shuhuda amini wa Fumbo la Msalaba katika maisha yake, chachu ya kuyatakatifuza malimwengu. 

Mwenyeheri Benedetta Bianchi Porro: Shuhuda wa Msalaba!

Mwenyeheri Benedetta Bianchi Porro ni shuhuda wa Msalaba uliofumbatwa katika udhaifu wa mwili wake, akaukubali na kujisadaka kwa ajili ya kuwashirikisha jirani zake: huruma na upendo wa Mungu. Fumbo la Msalaba ni kielelezo cha cha upendo wa Mungu kwa binadamu, aliyejinyenyekesha katika Fumbo la Umwilisho ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu: Ni kilele cha ufunuo wa: huruma, upendo, ukuu, utukufu na utakatifu wake, changamoto kwa Wakristo ni kushikamana pamoja na Kristo katika mapambano, ili siku moja waweze kushinda pamoja naye! Huu ndio ujumbe wa matumaini unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba, mwaliko wa: kumtafakari Kristo mfufuka kiini cha imani na matumaini ya Kikristo. Mama Kanisa katika maadhimisho ya Siku kuu ya Kutukuka kwa Msalaba “Exaltatio Sanctae Crucis”, Jumamosi tarehe 14 Septemba 2019, huko Forli, nchini Italia, Kardinali Giovanni Angelo Becciu, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, amemtangaza mtumishi wa Mungu Benedetta Bianchi Porro kuwa Mwenyeheri. Kardinali Giovanni Angelo Becciu katika mahubiri yake amesema, sadaka ya Msalaba ni kielelezo cha upendo wa hali ya juu kabisa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Kardinali Becciu amekazia kwa namna ya pekee kuhusu: Fumbo la Msalaba, Mwenyeheri Benedetta Bianchi Porro, shuhuda wa Msalaba uliofumbatwa katika udhaifu wa mwili wake, akaukubali na kujisadaka kwa ajili ya kuwashirikisha jirani zake: huruma na upendo wa Mungu ambao umeacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za watu wa Mungu nchini Italia. Fumbo la Msalaba ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa binadamu, aliyejinyenyekesha katika Fumbo la Umwilisho ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Huu ni mwaliko kwa waamini kuondokana na utandawazi unaofumbatwa katika uchoyo na ubinafsi; utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani. Fumbo la Msalaba ni kielelezo na ushuhuda wa upendo, nguvu ya huruma na msamaha wa Mungu, unaofyekelea mbali : kiburi, chuki, uhasama na tabia ya kutaka kulipiza kisasi. Upendo na huruma ya Mungu ni njia inayomwelekeza mwamini katika ukombozi.

Si rahisi sana kulielewa Fumbo la Msalaba, lakini mang’amuzi ya watakatifu, wafiadini na waungama imani wanasema Fumbo la Msalaba ni chemchemi ya amani, furaha ya ndani na mwanga angavu wa maisha. Mwenyeheri Benedetta Bianchi Porro ni shuhuda wa Fumbo la Msalaba kwani katika ujana wake, alijifunza kujisadaka bila ya kujibakiza; akatumia kikamilifu karama na mapaji yake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ulemavu wake haukuwa kikwazo cha kushindwa kushirikishana na wengine matendo makuu ya Mungu. Katika ujana wake, akakita maisha katika sala iliyomwezesha kuanza hija ya ukomavu na utakatifu wa maisha kwa njia ya imani iliyomwilishwa katika matendo. Ulemavu na udhaifu wake wa mwili, vikamsaidia kushinda hofu na wasi wasi iliyokuwa ndani mwake. Katika safari ya maisha yake, akajiaminisha kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; akaonja mwanga wa huruma na mapendo yaliyomsaidia kuwa kweli ni chombo cha upendo na furaha ya Injili.

Mwenyeheri Benedetta Bianchi Porro akaukubali ulemavu na udhaifu wa mwili wake kama sadaka safi mbele ya Mwenyezi Mungu. Alipata faraja katika huduma na tiba aliyokuwa anapata kutoka hospitalini. Akazamisha maisha yake katika tafakari na sala, kiasi cha kuwa ni mshauri na mfariji wa wale waliokuwa wanateseka kutokana na sababu mbali mbali. Ni kijana aliyebahatika kuwa na imani thabiti, amani na utulivu wa ndani licha ya ugonjwa na udhaifu wake wa mwili. Alijitahidi kuboresha maisha yake ya imani kwa njia ya ushiriki mkamilifu katika maadhimisho ya Sakramenti na Mafumbo ya Kanisa. Kardinali Giovanni Angelo Becciu anasema, Kanisa kwa kumtangaza mtumishi wa Mungu Benedetta Bianchi Porro kuwa Mwenyeheri ni kutaka kushuhuda uwepo endelevu wa upendo wa Kristo Yesu kati ya waja wake. Ni ushuhuda wa Fumbo la Msalaba kama kiini cha huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa binadamu. Kwa ufupi kabisa, Fumbo la Msalaba ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu. Watakatifu wa Mungu ni ufunuo endelevu wa huruma ya Mungu. Ni mfano bora wa mwamini mlei katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu pamoja na kuendelea kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu.

Mwenyeheri Porro
15 September 2019, 13:34