Tafuta

Vatican News
Kardinali Parolin amewataka Umoja wa Mataifa kuhakikisha watu wanapata huduma ya afya inayofumbatwa na mshikamano,haki jamii na usawa katika kushiriki mafao ya wote. Kardinali Parolin amewataka Umoja wa Mataifa kuhakikisha watu wanapata huduma ya afya inayofumbatwa na mshikamano,haki jamii na usawa katika kushiriki mafao ya wote.  

Kard.Parolin:hakikisha huduma za afya kwa watu zinapatikana!

Kardinali Pietro Parolin Katibu wa Vatican akihutubia kikao cha 74 cha Umoja wa Mataifa amewataka Umoja wa Mataifa kuhakikisha watu wanapata huduma ya afya inayofumbatwa na mshikamano,haki jamii na usawa katika kushiriki mafao ya wote.Ni katika kikao kilichoongozwa na mada ya kutembea pamoja katika kujenga ulimwengu ulio bora.

Na Padre Angelo Shikombe, - Vatican

Kardinali Pietro Parolin Katibu wa Vatican na mwakilishi wa Vatican katika mkutano wa 74 juu ya chanjo ya afya ya duniani, uliofanyika mnamo tarehe 23 Septemba 2019 huko New York Marekani, ukiongozwa na Kaulimbiu ya “kutembea pamoja katika kujenga ulimwengu bora”, amewataka Umoja wa Mataifa kuhakikisha watu wanapata huduma ya afya inayofumbatwa na mshikamano, haki jamii, na usawa katika kushiriki mafao ya wote.

Katika kufafanua wosia wa Baba Mtakatifu Francisko, Kardinali Pietro Parolin amesema, afya ni haki msingi ya kila mtu na siyo upendeleo. Haki ya kuwa na afya njema, inaungana na haki ya kuishi. Hivyo inapaswa kulindwa kipindi chote cha maisha ya mtu. Changamoto ya huduma katika sekta ya afya duniani inaonesha kuwa sehemu nyingi duniani, jamii zinakosa huduma nzuri za afya kutokana na umaskini na kukosekana kwa miundo mbinu stahiki. Sehemu hizi za jumuiya za watu wazee, walemavu, maskini, ndizo zinahitaji kupewa kipaumbele katika utoaji wa huduma za afya. Aidha, jitahada za utafiti zinazofanywa na Shirika la afya dunia, zisibague maeneo ya watu maskini kwa vigezo vya kufuata sera za kisiasa na kiuchumi, bali zilenge kumkomboa mwanadamu katika mazingira hatarishi na kumkaribisha katika matumizi ya teknolojia na ustawi wa kijamii.

Akiwasilisha hoja yake kwa Rais wa Baraza la Umoja wa Mataifa Kardinali Pietro Parolin amesema, Mamlaka ya kipapa inakubaliana na Azimio la utoaji wa chanjo duniani linatekeleza mikakati iliyowekwa na Shirika la afya duniani (WHO) juu ya jinsia na afya ya uzazi. Hata hivyo Vatican haikubaliani kabisa na masuala ya utoaji mimba, upembuzi wa jinsia, mauaji ya watoto wanaosadikika kuwa na hitilafu au ulemavu, upandikizi wa mimba na ufanyaji – ugumba kwa njia ya mionzi.  Vitendo hivyo vinapingana na haki za binadamu na upendo kwa jirani.  Mwishoni Kardinali Parolin ameonesha ushiriki wa Vatican katika kuboresha sekta ya afya na hasa katika utoaji wa huduma katika mazingira yaliyoathirika na umaskini na ukosefu wa vitendea kazi.

23 September 2019, 15:41