Tafuta

Vijana nchini Msumbiji wanataka kuandika kurasa mpya za maisha zinazosheheni: matumaini, amani, upatanisho, haki, elimu, afya na maendeleo fungamani ya binadamu! Vijana nchini Msumbiji wanataka kuandika kurasa mpya za maisha zinazosheheni: matumaini, amani, upatanisho, haki, elimu, afya na maendeleo fungamani ya binadamu! 

Hija ya Papa Francisko Msumbiji: Vijana: Sanaa, Michezo &Umoja!

Vijana wa kizazi kipya nchini Msumbiji wamemwambia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wanataka kujizatiti kuandika ukurasa mpya wa matumaini yanayofumbatwa katika amani na upatanisho wa kidugu; kwa kukazia haki ya afya bora, chakula na elimu bora zaidi; tayari kujielekeza zaidi katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu, ili kuboresha maisha ya vijana wa Msumbiji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu anasema, vijana wapewe kipaumbele cha kwanza kwani wao wanaunda sehemu kubwa ya familia ya Mungu nchini Msumbiji. Changamoto mamboleo, ziwabidiishe kutumia vipaji vyao vya ubunifu, hawa ni mbegu iliyopandikizwa tayari, wakipewa fursa, watachangia mchakato wa ukuaji wa jamii unaotakiwa na wengi. Vijana kutoka dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo nchini Msumbiji, Alhamisi, tarehe 5 Septemba 2019 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Michezo wa Maxaquene “Mashakene” mjini Maputo.

Vijana wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwapatia kipaumbele cha pekee katika hija yake ya kitume nchini Msumbiji. Wanasema wao ni vijana waliobahatika kuzaliwa katika nchi iliyoshehenu maziwa na asali; nchi yenye utajiri mkubwa wa lugha, mila na tamaduni na kwamba, kwa njia ya “Mdundo wa Sindimba”, wanasheheni furaha kiasi kwamba matatizo yao yanapewa kisogo. Licha ya utajiri mkubwa ambao Msumbiji imejaliwa na Mwenyezi Mungu, lakini bado umaskini unasigina utu na heshima ya vijana wengi nchini Msumbiji, kiasi cha kutokuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Pamoja na kutambua tofauti zao, lakini bado wanajisikia wote kuwa ni watoto wa Baba wa milele.

Kwa sasa vijana wa Msumbiji wanataka kujizatiti kuandika ukurasa mpya wa matumaini yanayofumbatwa katika amani na upatanisho wa kidugu; kwa kukazia haki ya afya bora, chakula na elimu bora zaidi; tayari kujielekeza zaidi katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu, ili kuboresha maisha ya vijana wa Msumbiji. Vijana wanamuuliza Baba Mtakatifu Francisko,  Je, wanawezaje, kuhakikisha kwamba, hii ndoto yao inamwilishwa katika uhalisia wa maisha? Vijana wa Msumbiji wanamtakia Baba Mtakatifu Francisko afya njema ya roho na mwili; ili aendelee kutangaza na kushuhudia uzuri wa upendo, amani, utulivu na upatanisho miongoni mwa watu wa Mungu.

Msumbiji: Vijana

 

05 September 2019, 16:37