Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake Barani Afrika ameshuhudia mubashara nguvu na imani ya watu wa Mungu Barani Afrika. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake Barani Afrika ameshuhudia mubashara nguvu na imani ya watu wa Mungu Barani Afrika.  Tahariri

Hija ya Papa Francisko Barani Afrika: Nguvu & imani ya watu!

Hii kiu ya watu wa Mungu wanaohitaji nguvu ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili waweze kuimarika katika imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Huu ni muungano wa watu wa Mungu waliokuwa wanamsubiri kwa hamu kubwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kiini cha maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, yaani, kuwaimarisha ndugu zake katika imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika kuanzia tarehe 4 hadi 10 Septemba 2019, pamoja na mambo mengine, ilipania kukuza misingi ya: amani na upatanisho wa kidugu; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, sanjari na ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika. Kauli mbiu iliyoongoza hija ya Baba Mtakatifu nchini Msumbiji ni: matumaini, amani na upatanisho”. Kwa upande wa Madagascar, ni “Mpanzi wa amani na matumaini” na kauli mbiu ya familia ya Mungu nchini Mauritius ni “Hujaji wa amani”. Jumatano tarehe 11 Septemba 2019, Baba Mtakatifu wakati wa Katekesi yake kwa waamini, mahujaji na wageni ; baada ya kurejea kutoka kwenye hija yake ya kitume Barani Afrika amesema, matumaini ya watu ni Kristo Yesu na Injili yake, chachu makini ya udugu, uhuru, haki na amani kwa watu wote. Baba Mtakatifu kwa kufuata nyayo za wamisionari na watakatifu waliojisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili, amesema, hija yake Barani Afrika ilikuwa ni kupandikiza chachu hii kwa watu wa Mungu nchini Msumbiji, Madagascar na Mauritius.

Ni katika muktadha huu, Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika tahariri yake anasema, kwa hakika kuna jambo moja kubwa linalounganisha hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Msumbiji, Madagascar na Mauritius pamoja na hija zilizofanywa na watangulizi wake, bila kuweka kando umuhimu wa hija hii kwa wakati huu, yaani kiu ya watu wanaohitaji nguvu ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili waweze kuimarika katika imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Huu ni muungano wa watu wa Mungu waliokuwa wanamsubiri kwa hamu kubwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kiini cha maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, yaani, kuwaimarisha ndugu zake katika imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Bahari ya watu kutoka sehemu mbali mbali, wakiwa na nyuso za matumaini pamoja na shuhuda mbali mbali walizoonesha; walimsubiri, Baba Mtakatifu kwa hamu na furaha kubwa, kielelezo makini cha nguvu ya watu kukutana katika mchakato wa imani. Watu walijipanga kando ya barabara; wakakusanyika kwenye viwanja mbali mbali; wakapanda mitini, ili tu waweze kupata fursa ya kumwona Khalifa wa Mtakatifu Petro anayepita kati yao, ili kuandika historia katika maisha ya mtu binafsi na ile ya jamii katika ujumla wake.

Huu ni ushuhuda unaoonesha maana ya ile nguvu ya Kanisa. Watu walitafuta kila nafasi iliyokuwa mbele yao ili kutangaza na kushuhudia ile furaha ya Injili pamoja na kuimarishwa katika imani, matumaini na mapendo na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, ameshuhudia imani ya watu wa Mungu Barani Afrika ikimwilishwa mubashara katika matendo, kielelezo makini cha nguvu ya watu wa Mungu. Kwa watu kutazamana katika hali ya unyonge na imani, hapo pia kuna fumbo la Kanisa ambalo Kristo Yesu amemkabidhi Mtakatifu Petro pamoja na waandamizi wake; kuna utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro wa kuwaimarisha ndugu zake katika imani, licha ya matatizo na changamoto mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu katika mahojiano maalum na waandishi wa habari waliokuwemo kwenye msafara wake amekiri kwamba, kuna cheche za mpasuko wa Kanisa, lakini kuna haja ya kukazia umuhimu wa unyenyekevu katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anasema kukosoana kwa heshima ni sehemu ya mchakato wa ukuaji wa mtu katika ukweli, haki na upendo kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Shutuma mbali mbali zinazotolewa dhidi yake na Kanisa katika ujumla wake, amesema kwamba, anategemea sana sala ndiyo iliyosaidia hata kukuza na kukomaza mbegu ya Ukristo huko Msumbiji, Madagascar na Mauritius. Hakuna sababu ya wongofu wa shuruti, bali ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika Injili ya upendo, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kidugu. Dr. Paolo Ruffini katika tahariri yake anakaza kusema, hii ni Sala ya Kikuhani ilyotolewa na Kristo Yesu wakati wa Karamu ya mwisho, siku ile iliyotangulia mateso, kifo cha Msalaba na hatimaye, ufufuko kutoka kwa wafu. Hili ni tukio ambalo lilikuwa limetangulia Jumapili ya matawi, alipokuwa anaingia Yerusalemu, watu wakamlaki kwa shangwe kubwa kama Mfalme. Kumbe, nguvu ya Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na waandamizi wake, inafumbatwa katika sala, ambayo Kristo Yesu, aliitumia kumwaminisha Mtakatifu Petro, Mtume kwa Baba yake wa milele.

Mtakatifu Yohane Paulo II akinukuhu Mwinjili Luka aliwahi kusema, “...tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini limekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako” Lk. 22: 31-32. Bila shaka huu ni mwelekeo wa nyakati za mwisho, pale ambapo Mitume watapewa Mamlaka ya kuweza kutoa hukumu kwa Makabila 12 ya Israeli. Lakini, pia wanayo dhamana na utume huku “huku bondeni kwenye machozi”, hasa wakati wa majaribu. Dr. Paolo Ruffini anahitimisha tahariri yake kwa kusema, haya maneno ni mwaliko kwa waamini kuangalia kwa jicho la imani uteuzi, dhamana, utume na mamlaka ya Mtakatifu Petro. Kristo Yesu anamhakikishia Petro Mtume, nguvu kutoka juu, kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Dr. Ruffini

 

12 September 2019, 17:05