Tafuta

Changamoto za maisha ya kipadre, kitawa na kwa waamini walei nchini Msumbiji: Kumezwa sana na malimwengu: majadiliano ya kidini na kiekumene; majanga asilia. Changamoto za maisha ya kipadre, kitawa na kwa waamini walei nchini Msumbiji: Kumezwa sana na malimwengu: majadiliano ya kidini na kiekumene; majanga asilia. 

Hija ya Papa Francisko Msumbiji: Changamoto za mapadre, watawa & waamini walei!

Changamoto kubwa wanayokabiliana nayo waamini walei ni ukosefu wa majiundo makini katika: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maadili na Maisha ya sala. Majadiliano ya kidini na kiekumene ni changamoto zinazopaswa kuvaliwa njuga nchini Msumbiji, bila kusahau umuhimu wa utamadunisho wa imani katika vipaumbele vya maisha ya waamini nchini Msumbiji: Uaminifu & Udumifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume nchini Msumbiji, Alhamisi tarehe 5 Septemba 2019 amekutana na kuzungumza na: wakleri, watawa, waseminaristi, makatekista na wafanyakazi katika jumuiya mbali mbali za Kikristo nchini Msumbiji. Amesikiliza shuhuda zao na hatimaye, akawapatia mchango wake wa kinabii kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji, utamadunisho, ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana katika ukweli na haki pamoja na kujisadaka katika maisha na utume wa Kanisa Askofu Hilario da Cruz Massinga, Mwenyekiti wa Tume ya Wakleri na Watawa, Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Msumbiji amechukua fursa hii kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko nchini Msumbiji. Hiki ni kielelezo cha Kanisa ambalo ni la kimisionari, linaloendelea kujikita katika mchakato wa umisionari wa kitume, ili kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili katika medani mbali mbali za maisha ya watu wa Mungu nchini Msumbiji.

Kati ya changamoto zinazoendelea kujitokeza ni baadhi ya wakleri na watawa kuanza kumezwa na malimwengu! Lakini katika ujumla wake, familia ya Mungu nchini Msumbiji inaendelea kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha na kwamba, wakati huu kuna vyama na mashirika ya waamini walei yanayoendelea kuibuka kwa ajili ya kuchangia mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo zinaendelea kuimarika, licha ya kinzani na mipasuko inayojitokeza katika mahusiano na waamini wa dini na madhehebu mengine ya Kikristo. Maaskofu wanasema, uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko kati yao ni faraja baada ya kuteseka sana na athari zilizosababishwa na kimbunga cha Idai na Kenneth. Mapadre kwa upande wao, wamemshukuru Mungu kwa zawadi ya Daraja Takatifu ya Upadre, ingawa kwa wakati huu wanapambana na changamoto zinazotaka kuwakatisha tamaa katika maisha na utume wao.

Kuna idadi ndogo sana ya Mapadre, ili kukidhi mahitaji ya maisha na utume wa Kanisa nchini Msumbiji. Changamoto kubwa ni uinjilishaji, utamadunisho, majadiliano ya kiekumene pamoja na matumizi sahihi ya vyombo vya mawasiliano ya kijamii. Yote haya ni tisa, kumi ni changamoto ya kuendelea kuwa waaminifu kwa Mungu na Kanisa pamoja na kuchuchumilia utakatifu wa maisha, kwa kukataaa kutumbukizwa katika malimwengu. Watawa wanamshukuru Mungu kwa kuendelea kuwa ni alama ya unabii katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kujisadaka bila ya kujibakiza katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu. Hata wao wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kutaka kumezwa na malimwengu kwa kuthamini vitu zaidi kuliko utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wamemwomba ushauri utakaowasaidia kuwa waaminifu na wadumifu katika maisha na wito wao; bila kusahau umuhimu wa kujikita katika majiundo makini na endelevu.

Makatekista wao wamesema, kwa miaka mingi wameteseka sana kuhusiana na athari za vita pamoja na hali ngumu ya maisha, lakini wameendelea kuwa na ujasiri wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu kati ya ndugu zao, kama sehemu ya utekelezaji wa dhamana na wajibu waliojitwalia katika Sakramenti ya Ubatizo. Wao wamekuwa wasaidizi wakuu kwa wakleri na watawa katika katekesi na majiundo ya waamini walei nchini Msumbiji. Changamoto kubwa wanayokabiliana nayo waamini walei ni ukosefu wa majiundo makini katika: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maadili na Maisha ya sala, mambo yanayowafanya Wakatoliki wengi kuyumba kama “daladala iliyokatika usukani. Majadiliano ya kidini na kiekumene ni changamoto zinazopaswa kuvaliwa njuga nchini Msumbiji, bila kusahau umuhimu wa utamadunisho wa imani katika vipaumbele vya maisha ya watu wa Mungu nchini Msumbiji.

Makatekista
05 September 2019, 17:40