Tafuta

Vatican News
Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu imeanza rasmi shughuli zake kwa kufanya mkutano wa kwanza mjini Vatican: Rasimu ya Kabisa yaanza kufanyiwa kazi. Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu imeanza rasmi shughuli zake kwa kufanya mkutano wa kwanza mjini Vatican: Rasimu ya Kabisa yaanza kufanyiwa kazi. 

Hati ya Udugu wa Kibinadamu: Kamati ya Utekelezaji: Yaanza kazi!

Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu inajielekeza katika ujenzi wa misingi ya haki na amani ili kuondokana na utamaduni wa kifo kutokana na chuki, uhasama na mipasuko ya kidini na kiimani. Kamati hii imebahatika pia kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amewapatia nakala ya Hati hii iliyochapishwa na Maktaba ya Kitume mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Hati ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa sahihi kati yake na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari  2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu ni mwaliko kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hati ya Udugu wa Kibinadamu inapata chimbuko lake katika mikutano elekezi iliyowasaidia waamini wa dini hizi mbili kushirikishana: furaha, majonzi, matamanio yao halali pamoja na changamoto mamboleo.

Kwa kutambua umuhimu na uzito wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu, kumeundwa Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati hii na kati ya wajumbe wake ni pamoja na: Kardinali mteule Miguel Angel Ayuso Guixot, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, Professa Mohamed Hussein Mahrasawi, Mkuu wa Chuo cha Al Azhar na Monsinyo Yoannis Lahzi Gaidi, Katibu muhtasi wa Baba Mtakatifu Francisko. Wengine katika kamati hii ni Jaji Mohamed Mahmoud Abdel Salaam, mshauri mkuu wa Mufti mkuu. Wajumbe wengine ni wale walioteuliwa kutoka Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu, Baraza la Wazee wa Kiislam Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na watu maarufu katika tasnia ya habari Umoja wa Falme za Kiarabu. Kwa upande wao, viongozi wa Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na Amiri Jeshi Msaidizi, watahakikisha kwamba, Hati ya Udugu wa Kibinadamu inatekelezwa kwa dhati kabisa na Kamati iliyoundwa, ili kumwilisha malengo yaliyobainishwa kwenye Hati hii.

Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati hii, tarehe 11 Septemba 2019, imefanya mkutano wake wa kwanza mjini Vatican, ili kuweka sera na mpango mkakati wa kuweza kutekeleza malengo yaliyomo kwenye Hati ya Udugu wa Kibinadamu, kwa ajili ya kukuza na kudumisha amani, maridhiano, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu katika ujumla wake. Kamati hii inapenda kujielekeza zaidi katika ujenzi wa misingi ya haki na amani ili kuondokana na utamaduni wa kifo kutokana na chuki, uhasama na mipasuko ya kidini na kiimani. Kamati hii imebahatika pia kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amewapatia nakala ya Hati hii iliyochapishwa na Maktaba ya Kitume mjini Vatican. Baba Mtakatifu amewasihi wajumbe hawa kuwa ni vyombo na wajenzi wa udugu wa kibinadamu, kama chemchemi ya mwelekeo mpya wa kisiasa; kwa kushirikiana na kupendana kwa dhati kama ndugu wamoja, licha ya tofauti msingi zinazoweza kujitokeza.

Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu imemchagua Kardinali mteule Miguel Angel Ayuso Guixot, kuwa Rais wa Kamati na Katibu mkuu ni Jaji Mohamed Mahmoud Abdel Salaam, mshauri mkuu wa Mufti mkuu. Wajumbe pia wameanza kuandika muswada wa Katiba itakayoratibu na kusimamia shughuli za Kamati hii. Wajumbe wa Kamati huu wamewashukuru Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar kwa maneno yao ya faraja. Kamati kuu, imeanza kuchukua hatua madhubuti, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha ombi maalum kwa Umoja wa Mataifa ili kutenga siku moja kati ya tarehe 3-5 Februari ya kila mwaka ili iadhimishwe kama Siku ya Udugu wa Kibinadamu Kimataifa. Kamati imeamua pia kuwakaribisha wajumbe kutoka katika dini mbali mbali ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu hata ndani ya Kamati yenyewe. Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu inatarajia kukutana tena tarehe 20 Septemba 2019 huko New York, nchini Marekani.

Kwa namna ya pekee kabisa, wajumbe kila mmoja kadiri ya imani yake, alisali kwa ajili ya kuwakumbuka wahanga wa shambulizi la kigaidi lililotokea nchini Marekani tarehe 11 Septemba 2001 pamoja na wahanga wote wa mashambulizi ya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia. Hati ya Udugu wa Kibinadamu inawachangamotisha waamini wa dini mbali mbali kujenga na kuimarisha imani yao kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kuwa na imani na udugu wa kibinadamu, ili waweze kushirikiana, kushikamana na kufanya kazi katika umoja na udugu. Hati hii inaweza kuwa ni dira na mwongozo kwa vijana wa kizazi kipya kama sehemu ya majadiliano ya kidini na kitamaduni; kwa kuheshimiana na kuthaminiana, huku wakiheshimu neema ya Mwenyezi Mungu inayotenda kazi ndani mwao. Hati hii inakazia maisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Inawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na huruma, kwa kuonesha ukarimu kwa maskini, wakimbizi na wahamiaji; wahanga wa vita na mashambulizi mbali mbali; wafungwa wa vita na watu wasiokuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Udugu wa kibinadamu usaidie kuganga na kuponya: kinzani na mipasuko inayoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia kwa kutumiwa na wajanja wachache kwa ajili ya mafao yao binafsi. Hati hii inakazia uhuru, haki, amani; upendo, msamaha na huruma kama mambo msingi ya imani. Hati inajielekeza zaidi katika mchakato wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, ushirikiano na mshikamano; kwa kuzingatia kanuni maadili, vigezo na viwango kuzingatiwa. Waamini wote wanasubiri siku ya hukumu kwa kuzingatia wajibu wa waamini hawa kimaadili na kiutu. Hati ya Udugu wa Kibinadamu inawaalika: Viongozi wa kidini; viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa; Watunga sera; Wachumi wa Kimataifa pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kushirikiana na kushikamana katika ujenzi wa utamaduni wa maridhiano, haki na amani, ili hatimaye, kusitisha vita, kinzani na umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia.

Umefika wakati wa kugundua tena tunu msingi zinazofumbatwa katika amani, haki, wema, uzuri, udugu wa kibinadamu, upendo na mshikamano. Huu ni mwamba salama wa wokovu kwa watu wote; mambo yanayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Kamati pamoja na mambo mengine, itakuwa na dhamana ya kuandaa miradi maalum itakayotumika kumwilisha hati hii katika ngazi ya kikanda na kimataifa. Kamati inatarajiwa kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa dini, viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa pamoja na watu mashuhuri duniani, ili kuunga mkono hati hii pamoja na kuendeleza malengo ya Hati ya Udugu wa Kibinadamu ambayo itaendelea kuwa rejea ya kihistoria kwa sasa na kwa siku za usoni. Inafikiriwa kuwahusisha pia watunga sera pamoja na wabunge ili kuwahamasisha kushiriki katika utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu katika ngazi ya kitaifa, ili tunu msingi za haki, amani na maridhiano kati ya watu ziweze kukita mizizi yake kwa waamini wa dini mbali mbali kuheshimiana na kuthaminiana.

Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu utaratibiwa na kusimamiwa na Jumba la Makumbusho la “Abrahamic Family House” yaliyotembelewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Hija ya 27 ya Kitume kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu kuanzia tarehe 3-5 Februari 2019 iliyoongozwa na kauli mbiu “Nifanye chombo cha amani”. Ziara hii ilipania kuandika ukurasa mpya wa historia na matumaini ya watu wa Mungu mintarafru majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Hati ya Udugu wa Kibinadamu ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti katika kutafuta, kulinda na kudumisha amani duniani, ili kukihakikishia kizazi cha sasa na kile kijacho mazingira ya haki, amani na utulivu. Umoja wa Falme za Kiarabu umejitwalia dhamana ya kuhakikisha kwamba unaendeleza majadiliano ya kidini, kwa kushirikishana tunu msingi za maisha ya kiutu, kiimani na kitamaduni, ili kuimarisha maridhiano, amani na ujenzi wa umoja wa kidugu miongoni mwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia!

Kamati Udugu Kibinadamu
17 September 2019, 11:21