Tafuta

Vatican News
Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga: Pallio Takatifu ni alama ya Kristo Mchungaji mwema; kielelezo cha umoja, mshikamano na upendo kati ya Maaskofu wa Majimbo makuu pamoja na Baba Mtakatifu. Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga: Pallio Takatifu ni alama ya Kristo Mchungaji mwema; kielelezo cha umoja, mshikamano na upendo kati ya Maaskofu wa Majimbo makuu pamoja na Baba Mtakatifu.  (AFP or licensors)

Askofu mkuu Nyaisonga: Kuvikwa Pallio Takatifu: Umoja wa Kanisa

Askofu mkuu Gervas Nyaisonga katika maadhimisho Siku kuu ya Mtakatifu Mathayo, Mwinjili, inayoadhimishwa na Mama Kanisa tarehe 21 Septemba 2019 anavishwa Pallio Takatifu na Askofu mkuu Marek Solczyński, Balozi Vatican nchini Tanzania, katika Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa kwenye Kanisa la Hija Parokia ya Mwanjelwa, Jimbo kuu la Mbeya. Umoja wa Jimbo kuu la Mbeya!

Na Padre Richard A.  Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Pallio Takatifu ni kitambaa cha sufi safi kinachovaliwa na Baba Mtakatifu pamoja na Maaskofu wakuu wa majimbo ya Kanisa Katoliki. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema; Kristo Yesu aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ni alama ya umoja na mshikamano kati ya Maaskofu wakuu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baada ya mabadiliko yaliyotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2015 Maaskofu wakuu wapya wanavishwa Pallio Takatifu na Mabalozi wa Vatican majimboni mwao, ili kuwashirikisha watu wa Mungu kutoka katika majimbo yanayounda Jimbo kuu husika tukio hili adhimu katika maisha na utume wa Kanisa mahalia! Itakumbukwa kwamba, tarehe 29 Juni 2019, Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani, Baba Mtakatifu Francisko alitoa Pallio Takatifu kwa Maaskofu wakuu wapya 31 na kati yao walikuwemo Maaskofu wakuu wawili kutoka Tanzania: Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza pamoja na Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya kwa mara ya kwanza tukio hili katika historia na maisha ya Kanisa nchini Tanzania.

Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga katika maadhimisho Siku kuu ya Mtakatifu Mathayo, Mwinjili, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe  21 Septemba, anatarajiwa kumvikwa Pallio Takatifu na Askofu mkuu Marek Solczyński,  Balozi Vatican nchini Tanzania, katika Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa kwenye Kanisa la Hija Parokia ya Mwanjelwa, Jimbo kuu la Mbeya. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu Flavian Matindi Kassala, Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC anasema, tukio hili lisaidie kuamsha na kukuza: umoja na mshikamano wa Majimbo yote yanayounda Jimbo kuu la Mbeya katika maisha na utume wa Kanisa; liamshe dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Makanisa mahalia kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha pamoja na kukazia tena umuhimu wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa.

Askofu Flavian Matindi Kassala anasema,  Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kumwilisha matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kukazia umuhimu wa watu wa Mungu kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Hiki ndicho kiini cha “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Baba Mtakatifu anahimiza ukuhani wa waamini wote; umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa; umuhimu wa majadiliano ya kidini na kiekumene; ari na mwamko wa kimisionari pamoja na umuhimu wa waamini walei kuwa ni chachu ya kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha ya imani inayomwilishwa katika matendo. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa ianze pia kutekelezwa kuanzia katika Majimbo na hatimaye, mchakato huu kuendelezwa katika ngazi ya Jimbo kuu, ili tafakari, maamuzi na utekelezaji wake uweze kupata ufanisi mkubwa zaidi.

Akizungumzia kuhusu maadhimisho mbali mbali ya Kanisa, yaanzie kwenye ngazi ya chini kabisa ambayo ni familia, Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, Vigango, Parokia, Jimbo, Jimbo kuu na hatimaye, kitaifa. Mawazo na tafakari zikizingatia mfumo huu, hata utekelezaji wake utaongeza tija na ufanisi katika maisha na utume wa Kanisa. Umefika wakati kwa Kanisa kutembea pamoja kama familia ya Mungu inayowajibikiana. Umoja wa Jimbo kuu ujidhihirishe hata katika mchakato wa kukabiliana na changamoto za upungufu wa rasilimali watu kwa ajili ya uinjilishaji, yaani kuna Majimbo ambayo yana idadi ndogo sana ya Mapadre na Watawa katika shughuli za uinjilishaji. Kuna baadhi ya majimbo yamebahatika kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali watu na fedha. Umoja huu ujioneshe katika kushirikishana pia amana na utajiri wa Majimbo husika. Kumbe, kabla ya kufikiria kutuma Mapadre kwenda kuinjilishaji Ulaya na Marekani, kipaumbele cha kwanza kiwe ni katika Jimbo kuu!

Ukarimu uanzie nyumbani. Kuna majimbo ambayo yanakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi, kiasi hata cha kushindwa kumudu gharama za kusomesha waseminari wake! Pale inapowezekana, changamoto hii inaweza kushughulikiwa na Maaskofu wanaounda Jimbo kuu, ili katika umoja, upendo na mshikamano wa kidugu, iweze kupatia ufumbuzi. Huu ndio mwelekeo mpya katika maisha na utume wa Kanisa la Tanzania baada ya kuadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya uinjilishaji. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha umoja, ushirikiano na mafungamano ya kijamii yanayoongozwa na kanuni auni! Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Utume wa waamini walei nchini Tanzania umekuwa ni muda muafaka wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani; muda wakuomba msamaha kwa mapungufu yaliyojitokeza katika kipindi cha miaka 50 iliyopita na kuomba huruma, neema na upendo wa kuanza upya kwa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, tayari kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Ushirikiano na mshikamano wa waamini walei, uimarishwe kuanzia kwenye familia, katika ngazi ya parokia, jimbo, jimbo kuu na hatimaye, kitaifa. Kwa mwelekeo huu, Kanisa nchini Tanzania litaendelea kucharuka kama kawa! Askofu mkuu Gervas Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika salam zake za shukrani, kwa watanzania waliofika kuwapongeza kwa: kuteuliwa na hatimaye, kupewa Pallio Takatifu na Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 29 Juni 2019 alisema kwamba,  Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na upendo, aliyewateua  katika nafasi hii kama Maaskofu wakuu, aguse pia roho na nyoyo za waamini wa Majimbo haya makuu pamoja na majimbo yote ya kanda watakazozihudumia. Kwa njia ya umoja, upendo na mshikamano wa dhati, hakuna jambo lolote linaloweza kushindikana. Kwa njia hii, Kristo Yesu atatangazwa na kushuhudiwa sehemu mbali mbali za dunia na Ufalme wa Mungu utaendelea kusimikwa katika misingi ya haki, amani, umoja na upendo utajengeka na kushamiri kama “Mtende wa Lebanon”. Maaskofu wakuu wapya wanao nia njema na sababu msingi za kutekeleza wito, dhamana na utume wao, lakini wanaomba neema ya Mwenyezi Mungu iwaguse wote ili washikamane na kazi ya Mungu iweze kutendeka kwa ufasaha zaidi.

Askofu Mkuu Nyaisonga Pallio
20 September 2019, 14:30