Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amempongeza Askofu Anthony Banzi wa Jimbo Katoliki la Tanga kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu awekwe wakfu kuwa Askofu, 15 Septemba 2019. Baba Mtakatifu Francisko amempongeza Askofu Anthony Banzi wa Jimbo Katoliki la Tanga kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu awekwe wakfu kuwa Askofu, 15 Septemba 2019. 

Papa Francisko ampongeza Askofu Banzi kwa Jubilei 25 ya Uaskofu

TEC: Jubilei Miaka 25 ya Askofu Banzi: Uwepo na utume wake; kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano katika huduma mbali mbali kwa watanzania, lakini zaidi kwa wakati huu, kwa kusaidia kuokoa maisha ya Askofu mkuu Ruwaichi na kwamba, Kanisa Katoliki nchini Tanzania litaendelea kushirikiana na Serikali katika mchakato wa: ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi.

Na Padre Richard A.  Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu Anthony Banzi wa Jimbo Katoliki Tanga, Jumapili, tarehe 15 Septemba 2019 ameadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu. Sherehe hizi zimekuwa ni fursa kwa familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Tanga, lakini zaidi kwa Askofu Banzi, kuweza kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini! Imekuwa ni fursa ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya uhai na utimilifu wa Daraja Takatifu ya Upadre, yaani Uaskofu. Ibada ya Misa Takatifu imeongozwa na Askofu Banzi na mahubiri kutolewa na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, ambaye ndiye aliyemweka wakfu kuwa Askofu, miaka 25 iliyopita! Katika mahubiri yake, Kardinali Pengo amekazia dhamana, nafasi na wajibu wa Askofu Banzi kwa familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Tanga.

Baba Mtakatifu Francisko amempongeza Askofu Banzi kwa maisha, huduma na utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Tanga. Salam za Baba Mtakatifu zimetolewa kwa niaba yake na Askofu mkuu Marek Solczyński,  Balozi Vatican nchini Tanzania. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu Flavian Matindi Kassala, Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC kuhusu maadhimisho haya anasema, imekuwa ni nafasi ya pekee kabisa kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Tanzania kumshukuru Mungu kwa mambo makuu matatu: Uwepo na utume wa Askofu Banzi katika kipindi cha Miaka 25 ya Uaskofu wake; kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano katika huduma mbali mbali kwa watanzania, lakini zaidi kwa wakati huu, kwa kusaidia kuokoa maisha ya Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam na kwamba, Kanisa Katoliki nchini Tanzania litaendelea kushirikiana na Serikali katika mchakato wa kuwaletea watanzania wengi ustawi na maendeleo fungamani.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linampongeza Askofu Banzi kwa sadaka na majitoleo yake kwa ajili ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimboni Tanga. Baraza linatambua mchango wake mkubwa katika tasnia ya mawasiliano ya jamii, kwa kutoa mwelekeo chanya wa umuhimu wa mawasiliano kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji kwa kusoma alama za nyakati, ili kuhakikisha kwamba, hata Kanisa Katoliki nchini Tanzania linajifunga kibwebwe kuhakikisha kwamba, linatumia maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano katika maisha na utume wake. Mchango wake katika tasnia ya mawasiliano, ukaonekana na kuwavuta Maaskofu wenzake wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, yaani AMECEA na hivyo, kumteuwa kuwa ni Mwenyekiti wa Idara ya Mawasiliano, leo hii, AMECEA imepiga hatua kubwa katika mawasiliano ya jamii. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, likaona na kuthamini mchango wake, akateuliwa kuwa Mwenyekiti mwenza wa Tume ya Mawasiliano SECAM.

Askofu Kassala anakiri kwa kusema kwamba, kwa hakika Askofu Banzi amelijengea Baraza la Maaskofu Katoliki mfumo thabiti wa mawasiliano, changamoto iliyoko mbele yao ni kuhakikisha kwamba, mfumo huu unatumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa ndani na nje ya Tanzania. Askofu Banzi katika maisha na utume wake, amekumbana na changamoto za maisha, hasa katika afya, lakini bado ameendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya watu wa Mungu ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Tanga. Kwa sasa Askofu Banzi ni mlezi wa mashirika ya kitawa na kazi za kitume nchini Tanzania. Katika kipindi cha miaka 25 ya maisha na utume wake, kwa hakika amekuwa ni amana na utajiri mkubwa kwa familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Tanga katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Askofu Kassala anasema, Jimbo limewekeza sana katika sekta ya elimu na afya kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaofumbatwa katika ushuhuda na majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi.

Ni katika huduma makini kwa watanzania, Askofu Banzi amekuwa pia ni kiungo muhimu sana kati ya Kanisa na Serikali kwa ajili ya huduma za kijamii, ili kulinda, kukuza na kutetea utu, heshima ya watanzania wote bila ubaguzi. Kanisa Katoliki Tanzania litaendelea kushirikiana na kushikamana na Serikali katika huduma kwa watanzania. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linamshukuru na kumpongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kupokea na kukubali kuitikia mwaliko wa kushiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Askofu Anthony Banzi. Katika sherehe hizi, Rais Magufuli aliwakilishwa na Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu. Askofu Kassala anasema, imekuwa ni nafasi adhimu kwa Maaskofu kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa jitihada za makusudi zilizofanywa kwa ajili ya kuokoa maisha ya Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, ambaye alipatwa na ugonjwa wa kiharusi akiwa mkoani Kilimanjaro, akapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kilimanjaro, (KCMC) na kisha kupelekwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili, (MOI) ambako alifanyiwa upasuaji mkubwa chini ya jopo la Profesa Joseph Kahamba, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu, (MOI).

Itakumbukwa kwamba, tarehe 10 Septemba, 2019, Rais John Pombe Magufuli akamtembelea ili kumtakia hali, Askofu mkuu Ruwaichi, jambo ambalo ni faraja kubwa kwa watu wa Mungu nchini Tanzania. Kanisa linaipongeza Serikali kwa kufanikiwa kupunguza rufaa za upasuaji wa wagonjwa nje ya Tanzania kwa asilimia 95% baada ya kujenga uwezo wa ndani, kadiri ya takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, MOI imepiga hatua kubwa katika huduma, kwa kukamilisha jengo, kuongeza vitanda vinavyohitajika katika vyumba vya upasuaji na chumba cha wagonjwa mahututi, (ICU). MOI imenunua vifaa vipya vya uchunguzi wa magonjwa na sasa iko mbioni kununua kifaa kiitwacho Endovascular Neurosuite ambacho kinagharimu shilingi Bilioni 7.5, hali ambayo itaiwezesha MOI kufikia kiwango cha kimataifa. Askofu Kassala anakiri kwamba, hii ni hatua kubwa katika kujali utu, heshima na maisha ya watanzania, kielelezo makini cha kukumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Rais Magufuli kwa upande wake, amesema, Serikali ya awamu ya tano inatambua na kuthamini mchango wa madhehebu ya dini mbali mbali nchini Tanzania, kwani hii ni huduma ambayo haina mbadala. Changamoto kubwa ni kuendelea kuimarisha misingi ya haki, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, ili kwa njia ya ushirikiano, kuweza kuongeza kasi ya maendeleo fungamani nchini Tanzania. Rais Magufuli anasema, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya ushirikiano kwa kuheshimu uhuru wa kuabudu. Serikali imewataka viongozi wa kidini kuhakikisha kwamba wanakuwa makini ili watu wachache wasitumike kuvuruga amani na umoja wa kitaifa nchini Tanzania. Tofauti mbali mbali miongoni mwa watanzania ni amana na utajiri na wala zisiwe ni sababu ya chuki, uhasama na utengano. Serikali pia imempongeza Askofu Anthony Banzi kwa mchango wake katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Jimboni Tanga katika harakati za kuchochea maendeleo. 

Sherehe za Jubilei ya Miaka 25 ya Askofu Banzi zimeadhimishwa kwenye viwanja vya Kanisa kuu la Mtakatifu Anthony wa Padua, vilivyoko Chumbageni. Sherehe hizi zimehudhuriwa na umati mkubwa wa wakleri, watawa na waamini kutoka ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Tanga. Itakumbukwa kwamba, Askofu Anthony Banzi, alizaliwa tarehe 28 Oktoba 1946 huko Morogoro. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 29 Julai 1973 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 10 Juni 1994 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Tanga na kuwekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Tanga, tarehe 15 Septemba 1994.

Askofu Banzi 25 Uaskofu
19 September 2019, 11:23