Tafuta

Siku kuu ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje Bosnia na Erzegovina 2019: Muda wa Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, katekesi awali na endelevu: Vijana wau wa uinjilishaji mpya! Siku kuu ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje Bosnia na Erzegovina 2019: Muda wa Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, katekesi awali na endelevu: Vijana wau wa uinjilishaji mpya! 

Utume wa Mama Kanisa kwa Vijana: Wadau wa uinjilishaji mpya!

Katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje, Kardinali de Donatis amewataka vijana wa kizazi kipya kupyaisha maisha yao kwa kutakasa dhamiri zao ili kupokea Neno la Mungu. Askofu mkuu Fisichella amewataka vijana kuwa ni vyombo na mashuhuda wa uinjilishaji mpya kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto katika maisha yao. Vijana wawe wainjilishaji mahiri!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya 30 ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje nchini Bosnia na Erzegovina kuanzia tarehe 31 Julai hadi tarehe 6 Agosti 2019, Sherehe ya Kung’ara Bwana, yameongozwa na kauli mbiu “Mladifest 2019”: “Njoo unifuate” (Mk. 10:21). Maadhimisho haya yamepambwa kwa Ibada ya Misa Takatifu zilizoongozwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa; Sakramenti ya Upatanisho; Katekesi makini kama sehemu ya majiundo endelevu ya vijana wa kizazi kipya, sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo ya Mababa wa Sinodi kuhusu utume wa vijana. Kimekuwa ni kipindi cha shuhuda mbali mbali za maisha na utume wa vijana katika kukabiliana na changamoto mamboleo na hatimaye, wameadhimisha pia Ibada ya Njia ya Msalaba, kwa kuwakumbusha vijana kubeba vyema Misalaba yao na kuanza kumfuasa Kristo Yesu katika maisha ya huduma ya upendo kwa Mungu na jirani.

Kardinali Angelo De Donatis katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya ufunguzi wa maadhimisho haya yaliyoanzishwa miaka thelathini iliyopita na Padre Slavko Barbaric aliyewakusanya vijana ili kuwafundisha katekesi kuhusu Ibada na Tasaufi ya Bikira Maria; kwa namna ya pekee amekazia umuhimu wa upyaisho wa maisha ya Kikristo, ili kuuvua utu wa kale na kuanza kutembea katika utu mpya katika mwanga wa Kristo Mfufuka! Ili kuweza kufikia hatua hii ya maisha, vijana wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kutakasa dhamiri zao, ili waweze kuwa tayari kupokea ujumbe wa Kristo Yesu katika maisha yao; ujumbe wa Injili, kimsingi unahitaji kutua nanga katika akili na moyo uliotulia, tayari kusubiri kwa ari na moyo mkuu siku ile Kristo Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Kristo Yesu ni: Njia, Ukweli na Uzima.

Vijana wanahamasishwa kufikiri na kutenda katika mwanga wa kweli za Kiinjili. Kwa njia hii, wataweza kupyaisha maisha, kwa kuuvua utu wa kale uliochakaa kama “ jani la mgomba wa ndizi”. Upya wa maisha katika Kristo Yesu ni kielelezo cha hekima na busara ya wafuasi wa Kristo wanaotoa mwanya ili huruma na upendo wa Mungu viweze kung’aa na kushuhudiwa hapa ulimwenguni. Kardinali Angelo De Donatis amehitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, Kanisa lina utajiri na amana kubwa ya uzoefu na mang’amuzi ya watakatifu waliokuwa wadhambi, lakini wakatubu na kumwongokea Mungu katika maisha yao, leo hii ni mifano bora ya kuigwa na familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Utakatifu ni mapambano endelevu katika maisha ya waamini.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya, alijichimbia zaidi katika katekesi kwa kuonesha umuhimu wa vijana wa kizazi kipya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kiinjili. Upendo wa Kikristo ni amana na utajiri unaotoa utambulisho wa maisha ya mwamini, kama sehemu ya maandalizi ya kurithi maisha na uzima wa milele. Kwa namna ya pekee, Askofu mkuu Fisichella amehimiza umuhimu wa neema ya Mungu katika maisha ya waamini, Utume wa Filipo katika mchakato wa kumwinjilisha yule towashi mkushi; kielelezo cha upya wa maisha ya Mkristo Mbatizwa; fumbo na maana ya maisha ya mwanadamu; imani katika maisha ya mwamini inayofungwa na kifungo cha upendo, ili mwamini aweze kupenda kwa ajili ya kupenda zaidi!

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella anafafanua kwamba, Filipo katika kumtangazia, kumshuhudia na kumfafanulia Maandiko Matakatifu yule towashi mkushi, lakini mhusika mkuu hapa ni Mwenyezi Mungu, ambaye alifungua nyoyo za watu hawa wawili, kuwa ni watangazaji na mashuhuda makini wa Injili ya Kristo Yesu. Injili ni mpango wa ukombozi ambao Mwenyezi Mungu anapenda kuwashirikisha watu wote ili waweze kuokoka na hatimaye, kuingia katika maisha na uzima wa milele. Habari Njema ya Wokovu inatoa na kufafanua maana ya maisha; kwa kuachia nafasi ya kupokea neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Filipo katika Kitabu cha Matendo ya Mitume anawawakilisha vijana wanaojisadaka usiku na mchana kwa ajili ya kuwafafanulia watu wa Mungu utamu wa Maandiko Matakatifu. Filipo alikuwa na kiu na ari ya kutaka kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo katika hali ya unyenyekevu pasi na makuu. Wainjilishaji wanapaswa kuwaheshimu na kuwathamini wale wanaotangaziwa Injili ya Kristo pamoja na kuzingatia uhuru wa wale wote wanaotangaziwa Injili, kwani uhuru wao unapaswa kuheshimiwa pia. Filipo alihubiri kwa umahiri mkubwa na hatima yake yule towashi mkushi  akaamini na kubatizwa. Filipo kwa njia ya nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, aliweza kutangaza na kushuhudia Injili kwa njia ya maisha yake; akagusa akili na moyo wa towashi mkushi, kiasi cha kuamua kubatizwa, ili kuuvua utu wa kale na kuanza kuambata njia mpya ya maisha katika mwanga wa Kristo Mfufuka.

Hiki ndicho kinachopaswa kuwa ni kielelezo makini cha wale wote wanaojisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sehemu mbali mbali za dunia. Lazima wawe ni watu wanaomtii Roho Mtakatifu wanapotekeleza dhamana na wajibu wao wa kuinjilisha. Wahubiri wawe na ujasiri wa kuzima kiu na matamanio halali ya watu wa Mungu katika maisha yao. Wawe na ujasiri wa kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu, chemchemi ya msamaha na wokovu wa walimwengu. Neno ambalo ni msingi wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu!

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella katika katekesi yake, anaendelea kuchambua kwa kina na mapana Fumbo la maisha ya binadamu; uhusiano wake na Mwenyezi Mungu, kwani ameumbwa kwa sura na mfano wake. Lakini, katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, inaonekana kana kwamba, sayansi inaendelea kumpeleka “puta mwanadamu” kiasi hata cha kumfanya kukengeuka na hatimaye kupoteza dira na mwelekeo sahihi wa maisha kuhusu kazi ya uumbaji! Angalia wanavyochezea viini tete na maisha katika ujumla wake! Bikira Maria ni mfano bora wa imani inayomwilishwa katika matendo. Binadamu anatambua kwamba, maisha yake, yanapata umuhimu wa pekee katika Fumbo zima la huruma na upendo wa Mungu. Binadamu ataendelea kubaki kuwa ni fumbo hata katika maisha yake mwenyewe, kwani kifo ndicho kizingiti cha mambo yote haya!

Mwanadamu anaweza kupata ukweli na uhalisia wa maisha yake kwa njia ya toba na wongofu wa ndani; kwa kukubali kupokea na kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Ni kwa njia hii, waamini wataweza kushinda changamoto mamboleo katika maisha yao. Imani iwe ni dira na mwongozo wa maisha katika kufikiri, kuamua na kutenda. Watambue kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa na Mungu. Kumbe hata wao wanapaswa kupenda, ili waweze kupenda zaidi na kwamba, upendo una nguvu zaidi kuliko kifo! Imani na upendo ni sawa na chanda na pete; upendo unavuka kizingiti cha kifo na Mungu ni upendo na wala hakuna kitu chochote kinachoweza kuwatenga na upendo wa Mungu katika maisha yao!

Siku kuu ya Vijana 2019
10 August 2019, 15:13