Tafuta

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia ni mbinu mkakati wa Kanisa kutaka kutekeleza dhamana na utume wake wa kinabii Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia ni mbinu mkakati wa Kanisa kutaka kutekeleza dhamana na utume wake wa kinabii 

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Dhamana ya kinabii & Utu na heshima ya binadamu

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia yanapania pamoja na mambo mengine, kuganga na kuponya uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote, uvunjwaji wa haki msingi za binadamu na hivyo kuanza mchakato njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani. Mama Kanisa anataka kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kinabii huko Ukanda wa Amazonia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia yatafanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 6-27 Oktoba 2019 kwa kuongozwa na kauli mbiu: "Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani". Hati ya maandalizi ya Sinodi ya Amazonia ilikazia umuhimu wa: kuona, kung'amua na kutenda! Hii ni Sinodi itakayopembua tema mbali mbali kuhusu: haki jamii, malezi ya awali na endelevu, katekesi makini, liturujia na utambulisho wa Kanisa katika Ukanda wa Amazonia. Hati ya Kutendea Kazi: “Instrumentum Laboris” imepitishwa hivi karibuni na Wajumbe Washauri wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Hati hii imegawanyika katika Sehemu Kuu III, kwa kuwa na utangulizi pamoja na hitimisho lake.

Sehemu ya kwanza inapembua kuhusu Sauti kutoka Amazonia kwa kujikita katika: Maisha, Ukanda wa Amazonia, Nyakati na Majadiliano. Sehemu ya Pili ni kuhusu Ekolojia fungamani:Kilio cha Dunia Mama na Kilio cha maskini. Hapa wanaangaliwa watu mahalia waliojitenga, wahamiaji, ukuaji wa miji; familia na jumuiya za watu, rushwa na ufisadi; afya fungamani, elimu makini na wongofu wa kiekolojia. Sehemu ya Tatu: Kanisa Sauti ya Kinabii Ukanda wa Amazonia: Changamoto na matumaini. Sura ya Kanisa na Umisionari Ukanda wa Amazonia; changamoto za utamadunisho; maadhimisho ya fumbo la imani na liturujia iliyotamadunishwa. Muundo wa jumuiya; Uinjilishaji mijini; Majadiliano ya kidini na kiekumene pamoja na utume wa vyombo vya mawasiliano ya jamii.

Utume wa kinabii wa Kanisa pamoja na mkakati wa maendeleo fungamani ya binadamu ni mada inayopembeuliwa kwa kina na mapana na Padre Michael Czerny, Katibu mkuu msaidizi, Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza ya Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu, ambaye hivi karibuni aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa mmoja wa Makatibu Maalum wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Kanisa kama mfano wa Msamaria mwema, linataka kujikita zaidi katika mchakato wa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; Ukanda wa Amazonia, kwa kuanzisha majadiliano katika ukweli na uwazi na hatimaye, kufanya maamuzi magumu katika maisha na utume wa Kanisa.

Hii ndiyo changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati akitangaza nia ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Ukanda wa Amazonia. Kwa njia ya Sinodi, Kanisa litafanikiwa kupambanua sera na mpango mkakati wa shughuli za kichungaji pamoja na kubainisha utambulisho wake. Dhamana hii imefafanuliwa vizuri zaidi kwenye Sura ya tatu ya “Instrumentum Laboris” yaani “hati ya Kutendea Kazi”, ambayo kwa ufupi kabisa inabainisha: changamoto, fursa na matumaini ya Kanisa Ukanda wa Amazonia. Kanisa linapenda kukazia zaidi: Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; haki na amani kwani haya ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume “Laudato si”, yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” anasema kwamba, kuna uhusiano mkubwa kati ya ekolojia ya mazingira, uchumi na jamii, mambo ambayo hayawezi kutenganishwa kama ilivyo pia hata katika mambo ya kiakili, maisha ya kiroho, kisiasa na kiuchumi yana athari zake katika mchakato mzima wa utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia yanapania pamoja na mambo mengine, kuganga na kuponya uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote, uvunjwaji wa haki msingi za binadamu na hivyo kuanza mchakato wa njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani.

Hapa Mama Kanisa anakazia kuhusu: Unabii wa Kanisa sanjari na Maendeleo fungamani ya binadamu, mambo ambayo ni sawa na chanda na pete, kwani yanategemeana na kukamilishana. Mama Kanisa anataka kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kusimama kidete katika shughuli za kichungaji; utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na kuhimiza mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Padre Michael Czerny, anasema, Waraka wa Kitume “Laudato si”, yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” unashughulikia uchafuzi wa mazingira: Kihistoria, kisayansi na kuangalia madhara yake katika mchakato mzima wa uchumi na maendeleo fungamani ya binadamu pamoja athari zake katika sera na shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa katika Ukanda wa Amazonia.

Hati ya Kutendea Kazi inapembua kwa kina na mapana hali halisi ya Ukanda wa Amazonia ambao sasa umegeuka kuwa ni uwanja wa vita na kinzani za kiuchumi kwa wawekezaji wanaotaka kufaidika na uchimbaji wa gesi asilia, nishati ya mafuta; kilimo cha mashamba makubwa pamoja na mazao ya misitu bila kusahau mali ghafi kwa ajili ya viwanda. Shughuli hizi za binadamu zina madhara makubwa katika utunzaji wa mazingira nyumba ya wote pamoja na maisha ya watu! Kumbe, hapa watu wote wanawajibika kimaadili kuona, kufikiri na kuamua kutenda kwa ujasiri. Ukanda wa Amazonia “sasa umekuwa uwanja wa fujo: vita, rushwa na uvunjifu wa utu, heshima na haki msingi za binadamu!

Watu mahalia pamoja na makampuni makubwa ya kigeni yanayoendelea kuwekeza katika fursa zinazojitokeza pamoja na vitega uchumi mbali mbali pamoja na raia wanahusika katika uharibifu wa mazingira. Matokeo yake ni makundi makubwa ya watu kuhama katika maeneo yao asilia; tamaduni za watu mbali mbali kuanza kutoweka pamoja na watu kukosa matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Mambo yote haya ni uvunjaji wa “Haki Msingi za Binadamu Ukanda wa Amazonia” zinazotambuliwa na Umoja wa Mataifa. Haki msingi, utu na heshima ya watu mahalia ni muhimu sana katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu!

Mambo haya yasiyopewa kipaumbele cha pekee, matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Ukanda wa Amazonia; idadi kubwa ya watu wasiokuwa na fursa za kazi na ajira, vita, ghasia na machafuko wa kisiasa, kijamii na kitamaduni; baa la njaa, magonjwa na umaskini wa hali na kipato. Hii ni njia ya Msalaba inayowatumbukiza watu mahalia katika ombwe na machafuko ya kisiasa sanjari na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Katika kipindi cha mwaka 2003 hadi mwaka 2017, watu 1,119 waliuwawa kikatiliki nchini Brazil, kwa sababu walijitokeza kuetetea utu, heshima na haki zao msingi; wakaonekana kuwa ni tishio kwa wawekezaji na matokeo yake, “wakfyekelewa mbali” na mkono wa chuma!

Ni katika muktadha huu, Mama Kanisa katika maisha, utume na dhamana yake ya kinabii anataka kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Kanisa linataka kujipambanua kama alivyowahi kusema Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika kuwalinda na kuwatetea maskini, kwani hawa ndio wale “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”. Kanisa pia linatambua mapungufu katika maisha na utume wake kwenye Ukanda wa Amazonia. Kanisa linataka pia kujikita katika wongofu wa kichungaji kwa kuzama katika tunu msingi za Kiinjili na Mafundisho Jamii ya Kanisa, bila kusahau mchango mkubwa uliotolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu: Injili ya uhai, haki, amani na ekolojia fungamani.

Padre Michael Czerny,anasemema huu ni mwaliko kwa Mama Kanisa kuendelea kujizatiti katika uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili sanjari na utamadunisho wa Injili katika uhalisia wa maisha na tamaduni za watu wa Ukanda wa Amazonia. Huu ni mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kanisa linataka kutembea bega kwa bega na watu mahalia, likiwasaidia kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, maendeleo fungamani ya binadamu na uinjilishaji ni mambo msingi yanayobainisha kwa ufupi kiini cha Habari Njema ya Wokovu!

Sinodi: Sauti ya Kinabii
01 August 2019, 13:57