Siku kuu ya Kung'ara kwa Bwana: ni tafakari ya ufunuo wa Sheria na Unabii unaopata utimilifu wake katika Fumbo la Msalaba yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kwa wafu! Siku kuu ya Kung'ara kwa Bwana: ni tafakari ya ufunuo wa Sheria na Unabii unaopata utimilifu wake katika Fumbo la Msalaba yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kwa wafu! 

Siku kuu ya Kung'ara Bwana: Utukufu Umetundikwa Msalabani

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anasema, Mama Kanisa katika maadhimisho ya Sherehe ya Kung'ara Bwana, Mama Kanisa ni muhtasari wa Mafumbo ya Kanisa na kwamba, anaungama kwa dhati kabisa kuhusu: Ubinadamu na Umungu wa Kristo; Kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu na Mkombozi wa dunia sanjari na kuzaliwa kwa Kanisa Sakramenti ya wokovu kwa binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Agosti anaadhimisha Sherehe ya Kung’ara kwa Bwana, kielelezo cha utimilifu wa Sheria na Unabii, unaofumbatwa katika Kashfa ya Fumbo la Msalaba, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Kung’ara kwa Bwana ni tukio ambalo Kristo Yesu alilitumia ili kuweza kuwaimarisha Mitume wake, ili waweze kukabiliana uso kwa uso na Kashfa ya Msalaba, kielelezo makini cha: hekima ya Mungu, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu, ili hatimaye, waweze kuwa ni watangazaji na mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika Fumbo la Msalaba! Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa kumi na sita, akifanya tafakari kuhusu Siku kuu hii anasema kwamba, ni muhtasari wa Mafumbo ya Imani ya Kanisa, yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu, ili aweze kuwaimarisha wafuasi wake katika hija ya mwanga wa imani. Ni kielelezo cha mshikamano wa dhati kati ya  Kristo Yesu na kazi ya uumbaji ambayo ameikomboa kwa njia ya Msalaba.

Mama Kanisa katika maadhimisho haya, anaungama kwa dhati kabisa kuhusu: Ubinadamu na Umungu wa Kristo; Kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu na Mkombozi wa dunia sanjari na kuzaliwa kwa Kanisa Sakramenti ya wokovu kwa binadamu! Sherehe hii inagusa kwa namna ya pekee, umuhimu wa Kanisa kusimama kidete kulinda na kutunza kazi ya uumbaji kama anavyokaza kusema Mtakatifu Damascene.  Kristo Yesu anaufunua Umungu wake kwa njia ya mwili uliotukuka, ndiyo maana Kanisa linamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na utukufu kwani ukuu una Yeye milele hata na milele! Hii ni changamoto kwa kila mwamini kuhakikisha kwamba, anatoa nafasi kwa mwanga wa imani, ili uweze kumletea mabadiliko ya dhati katika maisha, kwa kuifia dhambi na nafasi zake, ili kutoa fursa ya kuishi katika utu mpya unaofikia hatima yake katika Fumbo la Msalaba wa Kristo. Ni mchakato unaopania kumsafisha mwamini katika hija ya maisha yake ya kiroho, ili siku moja aweze kuufikia utukufu wa maisha na uzima wa milele.

Ni ufunuo wa mwanga utakaozima giza la Kashfa ya Fumbo la Msalaba, tayari kutoa nafasi kwa binadamu kumwabudu, kumsifu, kumtukuza na kumwomba Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kabisa, kuisikiliza sauti ya Mungu na kutekeleza mapenzi yake katika uhalisia wa maisha yao, kwani Neno la Mungu ni dira na mwongozo wa maisha. Neno la Mungu ni Ufunuo wa utambulisho wa Mwana wa Mungu kama siku ile ya Ijumaa kuu atakavyosema yule Akida kwamba, “kwa hakika huyu alikuwa ni Mwana wa Mungu”. Sherehe ya Kung’ara Bwana ni mwendelezo wa Siku kuu ya Ubatizo na Ukuu wa Fumbo la Msalaba na Mwanga unaong’ara katika maisha na utume wa Kanisa. Huu ni mwanga utakaojionesha kwa namna ya pekee, Siku ile Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho!

Kusikiliza ni sanaa inayohitaji majiundo makini na endelevu, mwaliko kwa waamini kumwomba Roho Mtakatifu, ili awasaidie kuwa wasikivu wema na wazuri, tayari kumwilisha kile wanachokisikia kutoka katika dhamiri zao nyofu! Yesu kama ilivyokuwa kwa Mitume wake wa karibu aliowateuwa kuwa mashuhuda kwa matukio muhimu ya maisha yake yaani: Petro, Yakobo na Yohane, Wakristo pia wanahamasishwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu imefunuliwa kwa njia ya Maandiko Matakatifu katika Sheria na Unabii na kupata utimilifu wake katika Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipotwaa mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu na kuzaliwa kwake Bikira Maria katika mambo yote alikuwa sawa na binadamu, isipokuwa hakutenda dhambi!

Wakristo wanatumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko kwa kutambua kwamba, daima Mwenyezi Mungu anaandama nao katika hija ya maisha yao. Sherehe ya kung’ara kwa Bwana ni chachu ya mabadiliko katika maisha, kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata upendo na huruma ya Mungu katika maisha, mambo msingi yanayowaelekeza waamini katika ukamilifu na utakatifu wa maisha. Katika maadhimisho ya Sherehe ya Kung’ara Bwana, Kanisa  kwa mwaka huu, 2019, linafanya kumbu kumbu ya miaka 41 tangu Mtakatifu Paulo VI alipofariki dunia, “dies natalis” akiwa kwenye Ikulu ndogo ya Castel Gandolf, nje kidogo ya mji wa Roma na kuzikwa tarehe 12 Agosti 1978 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, anasema, Mtakatifu Paulo wa VI, ni kiongozi aliyeongozwa na Msalaba wa Kristo katika maisha na utume wake. Akawa ni kielelezo makini katika kutoa maana ya uongozi kama huduma kwa ajili ya Familia ya Mungu hata katika mateso na mahangaiko ya ndani. Hii ni huduma iliyokuwa inaongozwa na dira na mwanga wa imani, kiasi hata cha kukubali kubeba ndani mwake shutuma ambazo hazikuwa na msingi wowote. Ni kiongozi aliyejizatiti kumwilisha Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa. “Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa” ni changamoto endelevu iliyovaliwa njuga na Mtakatifu Paulo VI, sasa, libeneke hili linaendelezwa na Baba Mtakatifu Francisko. Mtakatifu Paulo VI, akapambana na tawala dhalimu katika nyakati zake. Vita baridi ilikuwa imepamba moto, lakini daima akasimama kidete kutangaza kweli za Injili na Mapokeo ya Kanisa, huku akionesha mwanga wa imani hata katika giza la undani wa maisha ya mwanadamu.

Mtakatifu Paulo VI alikuwa ni mtu wa sala na imani thabiti; aliyekirimiwa uwezo mkubwa katika uongozi kwa njia ya diplomasia, ukomavu wa maisha ya kiroho, huku akitoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo na Kanisa lake. Alibahatika kuwa na ujasiri wa kufanya mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa; ujasiri ambao ulikuwa unabubujika kutoka katika imani; iliyomwezesha kufanya hija mbali mbali za kichungaji, ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, ni matunda ya changamoto za kichungaji zilizotolewa na Mtakatifu Paulo VI enzi ya uhai wake. Ni kiongozi aliyethamini majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kwa ajili ya maendeleo, ustawi na mafao ya wengi.

Itakumbukwa kwamba, alitangazwa kuwa Mwenyeheri hapo tarehe 19 Oktoba 2014 na Baba Mtakatifu Francisko na kunako tarehe 14 Oktoba 2018 wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana, akamtangaza kuwa Mtakatifu. Mama Kanisa mwaka 2018 ameadhimisha pia kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu Mtakatifu Paulo VI alipochapisha Waraka wa Kitume: “Humanae vitae” yaani “Maisha ya binadamu”.  Ni waraka unaopembua kanuni maadili na Mafundisho tanzu ya Mama Kanisa kuhusu mwono na maisha ya mwanadamu, tangu pale anapotungwa mimba hadi pale mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Anahimiza: wajibu wa wazazi katika kushiriki kazi ya uumbaji, kulea na kutetea zawadi ya maisha. Huu ni waraka wa kinabii unaobainisha dhamana na wajibu wa wanandoa wanaoushiriki katika kazi ya uumbaji, ili kuendeleza zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Ni dhamana ambayo inapaswa kumwilishwa katika furaha ya maisha na utume wao ndani ya familia. Mtakatifu Paulo VI alikuwa na upeo mpana na uwezo wa kuona mbali, akagundua changamoto na vikwazo vinavyowakabili wanandoa; akabainisha wajibu wa Kanisa kama Mama na Mwalimu na kuwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Mtakatifu Paulo VI katika tafakari aliyokuwa ameiandaa kwa ajili ya Sala ya Malaika wa Bwana, tarehe 6 Agosti 1978, alikuwa anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanatekeleza kwa uaminifu ahadi, wito na maisha yao ya Kikristo, kabla ya kuungana na Mwenyezi Mungu katika maisha na uzima wa milele!

Kung'ara Bwana
06 August 2019, 10:19