Tafuta

UCAP: Mchakato wa uchaguzi Barani Afrika: Dhamana na wajibu wa vyombo vya mawasiliano ya jamii katika kukuza amani jamii: Mkazo ni uandishi wa amani Barani Afrika! UCAP: Mchakato wa uchaguzi Barani Afrika: Dhamana na wajibu wa vyombo vya mawasiliano ya jamii katika kukuza amani jamii: Mkazo ni uandishi wa amani Barani Afrika! 

UCAP: Mchakato wa Uchaguzi Barani Afrika: Wajibu wa vyombo vya mawasiliano ya jamii

Dr. Ruffini katika ujumbe wake kwa Washiriki wa Jukwaa la Shirikisho la Wanahabari Wakatoliki Barani Afrika, UCAP, kuanzia tarehe 8-16 Agosti 2019 amekazia ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko, uliotolewa wakati wa maadhimisho ya Siku ya 52 ya Upashanaji Habari Duniani, kwa mwaka 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Ukweli utawaweka huru, habari potofu na uandishi wa amani”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ukweli utawaweka huru, habari potofu na uandishi wa amani ndiyo kauli mbiu iliyoongoza Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 52 ya Upashanaji Habari Duniani, kwa mwaka 2018. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mawasiliano ni sehemu ya mpango wa Mungu kwa binadamu na ni njia muhimu ya kung’amua na kujenga mshikamano kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wana uwezo wa kujieleza na kushirikishana ukweli, uzuri na wema. Baba Mtakatifu katika ujumbe huu, anakazia umuhimu wa mawasiliano ya kijamii katika huduma ya ukweli kwa kuondokana na habari potofu zinazofichama katika maamuzi ya kisiasa na azma ya kutaka kukuza mapato kiuchumi. Usambazaji wa habari potofu unatumia kwa ujanja mitandao ya kijamii na kwa mantiki ya kuhakikisha inafanya kazi. Habari za uongo zinaweza kuenea kwa haraka sana na hivyo kuhatarisha sifa za watu wengine. Baba Mtakatifu anakazia ukweli katika tasnia ya mawasiliano ya jamii, ili ukweli uweze kuwaweka watu huru, kwa kukazia haki na amani.

Ni katika muktadha huu, Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano, katika ujumbe wake kwa washiriki wa Jukwaa la Shirikisho la Wanahabari Wakatoliki Barani Afrika, UCAP, kuanzia tarehe 8-16 Agosti 2019 amekazia tena ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko, uliotolewa wakati wa maadhimisho ya Siku ya 52 ya Upashanaji Habari Duniani, kwa mwaka 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Ukweli utawaweka huru, habari potofu na uandishi wa amani”. Kongamano hili linafanyika mjini Abijan, Pwani ya Pembe, chini ya uratibu wa Askofu Raymond Ahoua wa Jimbo Katoliki la Grend Bassam ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kurugenzi wa Mawasiliano Baraza la Maaskofu Katoliki Pwani ya Pembe. Kongamano hili linaongozwa na kauli mbiu “Mchakato wa Uchaguzi Barani Afrika: Dhamana na wajibu wa vyombo vya mawasiliano ya jamii katika kukuza amani jamii”.

Baba Mtakatifu anasema, amani ni habari ya kweli: Dawa ya kuzuia uongo siyo mkakati, bali ni watu: watu ambao ni huru, kutokana na kiu, wako tayari kusikiliza na kwa njia ya jitihada za mazungumzo ya dhati ili ukweli uonekane; watu ambao, wamevutiwa na mema wanawajibika hata katika matumizi sahihi ya lugha. Iwapo njia ya kuondokana na usambazaji wa habari za uongo ni kuwajibika kwa namna ya pekee ni kujumuisha hasa wale wahusika wa ofisi za mawasiliano, waandishi wa habari na walinzi wa habari. Hawa katika ulimwengu mamboleo si kazi tu, bali ni utume wa kweli. Wanalo jukumu, licha ya uharaka wao wa kutaka kutoa habari wa  kwanza, wanapaswa kukumbuka kuwa kiini  cha habari si katika uharaka wa kutoa habari kwa wasikilizaji, lakini kitovu ni watu. Kuhabarisha watu ni kuwaunda, kwa sababu inahusiana na maisha ya watu, na kwa njia hiyo kuhifadhi vyanzo na ulinzi wa mawasiliano ndiyo ukweli na mchakato wa maendeleo ya wema, ambayo yanazaa matumaini na kufungua njia za mawasiliano na amani.

Baba Mtakatifu anapenda kuwaalika wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii, kila mmoja kuhamasisha uandishi wa habari wa amani.  Kwa  kufanya hivyo si kwa  maana ya kuwa na uandishi wa uzuri kwa kukataa matatizo makubwa yaliyopo ya kutotoa  sauti isiyo nzuri. Kinyume chake kuna ulazima wa uandishi wa habari za kweli bila uongo; zenye uadui na uongo na kushikilia matukio kutangaza yaliyo kinyume, zenye kutafuta ufanisi na matangazo kama mabomu; uandishi ambao unafanywa na watu kwa ajili ya watu ambao wanatambua kama huduma ya watu wote, hasa wale ambao wako katika ulimwengu, sehemu kubwa hawana sauti. Uandishi wa habari unaojibidiisha kutafuta sababu za kweli za migogoro, ili kukuza uelewa wa mizizi na ushindi  kwa njia  ya mchakato wa fadhila; uandishi  ambao unajikita katika kuelekeza suluhisho tofauti dhidi ya mlolongo wa habari mbaya na  unyanyasaji wa maneno. 

Kardinali Marc Armand Ouellet, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu  hivi karibuni alisema, siasa ni wito na si kila mwamini ana wito wa kuwa ni mwana siasa! Ikumbukwe kwamba, siasa si njia pekee inayoweza kuwahakikishia watu haki, kumbe, medani mbali mbali za maisha, ziwe ni mahali ambapo patawasaidia waamini kuweza kuyatakatifuza malimwengu, kwa kujikita katika mchakato wa kutafuta na kudumisha haki, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Waamini wanahimizwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe kwa Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2019 anasema, upendo na fadhila za kiutu ziwe ni kwa ajili ya siasa safi inayohudumia haki msingi na amani, kila mtu akijitahidi kujikita katika mafao ya wengi, kama sehemu ya ujenzi wa mji wa Mungu hapa duniani, ili kuendeleza historia ya maisha ya familia ya binadamu. 

Haki na usawa; tabia ya kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu; ukweli, uwazi na uaminifu ni tunu msingi zinazoboresha siasa safi. Papa anasema mwanasiasa bora ni yule anayetambua dhamana na wajibu wake kwa jamii; anayeaminika na kuthaminiwa na jamii; ni kiongozi anayejitaabisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; mwaminifu katika ahadi zake kwa wananchi waliomchagua, daima akijitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, tayari kuchochea mageuzi katika maisha ya watu; kwa kuwasikiliza na kutenda kwa ujasiri! Siasa safi inayojikita katika ujenzi wa amani inatambua karama za watu na inaendeleza majadiliano na watu kuaminiana na kuthaminiana badala ya kuangaliana kwa “jicho la kengeza”. Hizi ni dalili za ubinafsi unaofumbatwa katika dhana ya utaifa usiokuwa na tija wala mashiko badala ya kukuza umoja na udugu, wao wanakuwa ni sumu ya kusambaratisha watu. Jamii inawahitaji wajenzi wa amani, watakaokuwa ni watangazaji, mashuhuda na vyombo vya wema, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake ambaye anawatakia watoto wake furaha.

Dr. Ruffini:UCAP
13 August 2019, 15:14