Tafuta

Vatican News
Mkutano wa VIII wa Kikosi kazi cha ushirikiano kati ya Vatican na Vietnam umeridhishwa na mahusiano yaliyopo sasa ni wakati wa kuwa na Balozi mkazi wa Vatican nchini Vietnam. Mkutano wa VIII wa Kikosi kazi cha ushirikiano kati ya Vatican na Vietnam umeridhishwa na mahusiano yaliyopo sasa ni wakati wa kuwa na Balozi mkazi wa Vatican nchini Vietnam.  (Vatican Media)

Diplomasia kati ya Vatican na Vietnam: Mkutano XIII wa Kikosi kazi: Tamko la pamoja

Wajumbe wameridhishwa na mwenendo wa mahusiano kati ya Vatican, Kanisa na Serikali ya Vietnam katika miaka ya hivi karibuni pamoja na mwendelezo wa mawasiliano ambao uliibuliwa kutoka kwenye mkutano wa VII wa Kikosi kazi uliofanyika nchini Vietnam kunako mwaka 2018. Kumekuwepo na mawasiliano ya mara kwa mara kati ya Kikosi kazi cha Vietnam na Askofu mkuu Zalewski. B

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano wa nane wa kikosi kazi cha ushirikiano kati ya Vatican na Vietnam kuanzia tarehe 21-22 Agosti 2019 umehitimishwa hapa mjini Vatican. Ujumbe wa Vietnam kwenye mkutano huo umeongozwa na Bwana To Anh Dung, Naibu Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Vietnam na ujumbe wa Vatican umeongozwa na Monsinyo Antoine Camilleri, Katibu mkuu msaidizi wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican ambaye pia ameratibu mwenendo mzima wa mkutano. Kikosi kazi katika tamko la pamoja, kinasema kwamba, wajumbe wameridhishwa na mwenendo wa mahusiano kati ya Vatican, Kanisa na Serikali ya Vietnam katika miaka ya hivi karibuni pamoja na mwendelezo wa mawasiliano ambao uliibuliwa kutoka kwenye mkutano wa VII wa Kikosi kazi uliofanyika nchini Vietnam kunako mwaka 2018. Kumekuwepo na mawasiliano ya mara kwa mara kati ya Kikosi kazi cha Vietnam na Askofu mkuu Marek Zalewski, Balozi wa Vatican asiye mkazi nchini Vietnam.

Katika mkutano huu, ujumbe wa Vietnam umebainisha kwamba, kumekuwepo na utekelezaji wa sera na mikakati inayopania kudumisha uhuru wa kidini na kiimani na hivyo kuiwezesha Jumuiya ya Kanisa Katoliki nchini humo kuweza kutekeleza vyema maisha na utume wake. Ujumbe wa Vatican umeridhishwa na msaada mkubwa unaotolewa na Serikali ya Vietnam kwa waamini wa Kanisa Katoliki nchini humo na kwamba, wameonesha utashi wa kutaka kuishi kikamilifu wito wao kama waamini na raia wema, ili kuchangia kwa hali na mali katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Vietnam; daima wakiwa waaminifu kwa Mafundisho ya Kanisa pamoja na kuheshimu sheria, taratibu na kanuni za nchi ya Vietnam. Wajumbe wa kikosi kazi wamegusia pia hali ya maisha na utume wa Kanisa nchini Vietnam na kwamba, kuna haja ya kuendeleza zaidi mahusiano ya kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili, kwa kuwa na kanuni na mwongozo wa utume wa Balozi mkazi nchini Vietnam, mapema iwezekanavyo.

Wajumbe wa pande hizi mbili wameonesha utashi wa kuendeleza majadiliano kati yao; kwa kuheshimiana na kuthaminiana, ili kufikia muafaka wa kanuni na mwongozo wa mahusiano ya kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili. Wajumbe wameridhia uwezekano wa kuboresha mahusiano yatakayowahusisha viongozi wakuu wa nchi hizi mbili. Ujumbe wa Vietnam umepata nafasi ya kukutana na kuzungumza pia na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na kusalimiana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Mkutano umefanyika katika mazingira ya amani na utulivu mkubwa; kwa wote kuheshimiana na kuthaminiana.

Vatican Diplomasia

 

23 August 2019, 14:28