Tafuta

Vatican News
Kardinali  Marc Ouellet anawasihi waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuwaonesha wakimbizi na wahamiaji Uso wa huruma, upendo na mshikamano. Kardinali Marc Ouellet anawasihi waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuwaonesha wakimbizi na wahamiaji Uso wa huruma, upendo na mshikamano.  (AFP or licensors)

Onesheni huruma na upendo kwa wakimbizi na wahamiaji!

Wakimbizi na wahamiaji ni watu ambao wako hatarini sana kunyanyaswa: utu, heshima na haki zao msingi. Ni watu ambao wanaendelea kukumbana na “mkono wa chuma” kutoka kwenye serikali mbali mbali. Ni watu wanaoteseka na kusukumiziwa pembezoni mwa jamii kama ilivyokuwa hata kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akasulubishwa na hatimaye, akafia nje ya kuta za Yerusalemu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2019 itaadhimishwa Jumapili, tarehe 29 Septemba 2019 kwa kuongozwa na  kauli mbiu “Si Wahamiaji peke yao”. Baba Mtakatifu Francisko anasema, mambo yanayopewa kipaumbele cha pekee katika Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa ajili ya huduma endelevu na fungamani kwa wakimbizi na wahamiaji ni: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha. Baba Mtakatifu anashauri kwamba, kuwepo na ushirikiano wa dhati kati ya nchi wanakota wakimbizi na wahamiaji pamoja na nchi wahisani, ili kuhakikisha kwamba, changamoto zinazosababisha wimbi kubwa la wakimbizi zinadhibitiwa kikamilifu, ili kufuta mambo yale yanayosababisha watu kuzikimbia nchi zao. Mikakati ya kudumu ipewe kipaumbele cha kwanza kwa kusitisha kabisa: vita, uvunjaji wa haki msingi za binadamu; rushwa, ufisadi na umaskini; mipasuko ya kijamii sanjari na athari za uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote; kwani mambo yote haya yanasababisha mateso makubwa kwa watu.

Kuwepo na sera makini na endelevu kwa ajili ya nchi ambazo zimekuwa na migogoro na kinzani za kijamii, ili kusaidia mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu, kwa kukuza: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; utu na heshima ya binadamu vikipewa msukumo wa pekee. Mwezi Agosti, waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanafanya hija ya kimataifa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima, nchini Ureno. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordiae vultus” yaani “Uso wa huruma” anabainisha umuhimu wa hija katika maisha ya waamini, kwa kutambua kwamba, kimsingi maisha yenyewe ni hija na mwanadamu ni hujaji anayesafiri kuelekea kwenye makao na maisha ya uzima wa milele. Hija inakita uzoefu wake katika toba na wongofu wa ndani; katika tafakari ya Neno la Mungu pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Ni katika muktadha huu, Kardinali Marc Armand Ouellet, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu, hivi karibuni katika mahubiri yake, wakati wa maadhimisho ya Juma la 47 la Wakimbizi na Wahamiaji nchini Ureno, lililoanza kutimua vumbi hapo tarehe 11 hadi 18 Agosti 2019, alikazia kuhusu wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, wanaothubutu kuhatarisha maisha yao kwa kuanzisha “safari za matumaini Barani Ulaya”. Wakimbizi na wahamiaji ni watu ambao wako hatarini sana kunyanyaswa na kudhulumiwa utu, heshima na haki zao msingi. Ni watu ambao wanaendelea kukumbana na “mkono wa chuma” kutoka kwenye serikali mbali mbali. Ni watu wanaoteseka na kusukumiziwa pembezoni mwa jamii kama ilivyokuwa hata kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akasulubishwa na hatimaye, akafia nje ya kuta za Yerusalemu.

Kardinali Marc Armand Ouellet amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha moyo wa upendo na mshikamano wa hali na mali, ili kweli wakimbizi na wahamiaji waweze kupata: huduma na faraja katika mahangaiko yao mbali mbali katika safari ya matumaini ambayo wanathubutu kuifanya hata kama kifo wanakiona mbele ya macho yao daima. Kwa wakimbizi na wahamiaji, amewaombea ili waonje ushuhuda wa huruma na upendo kutoka kwa watu wa Mungu, ili waweze kutunza ndani mwao matumaini ya safari ndefu zaidi katika maisha. Ikumbukwe kwamba, Wakristo tangu mwanzo, wameendelea kujitambulisha kama mahujaji.

Kanisa linaendelea kufanya hija katika maisha ya watu; kuna wakati linateswa na kudhulumiwa; lakini linasindikizwa, na daima liko chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu. Ndiyo maana waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahimizwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo kwa jirani zao. Kristo Yesu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wake, amewafunulia watu Uso wa huruma na upendo wa Mungu, kielelezo makini cha mshikamano na binadamu wadhambi ili aweze kuwakomboa na hatimaye, kuwashirikisha katika maisha na uzima wa milele.

Wakristo wajenge na kudumisha utamaduni na Injili ya huduma na mapendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hawa ni wakimbizi na wahamiaji; waathirika wa biashara ya silaha duniani na ni watu wanaotumbukizwa katika mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Wote hawa, utu, heshima na haki zao msingi vimewekwa rehani. Mshikamano wa umoja na udugu wa kibinadamu, ulete faraja kwa watu wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali duniani. Kardinali Marc Armand Ouellet amehitimisha mahubiri yake kwa kuwakumbusha wakimbizi na wahamiaji kwamba, wao kwa hakika ni wajumbe wa Mungu, wanaoendelea kuwakumbusha watu wa Mataifa kwamba, hapa duniani, binadamu ni msafiri na wala hana makazi ya kudumu, kumbe, wanapaswa kujiwekea hazina mbinguni kwa njia ya huduma ya huruma na mapendo, kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Hija Fatima
16 August 2019, 14:30