Tafuta

Kumbu kumbu ya Daraja la Morandi: Imani na matumaini mapya miongoni mwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Genova, Kaskazini mwa Italia. Kumbu kumbu ya Daraja la Morandi: Imani na matumaini mapya miongoni mwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Genova, Kaskazini mwa Italia. 

Daraja la Morandi: Kumbu kumbu ya Matumaini mapya Genova!

Kardinali Angelo Bagnasco, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Genova, Jumatano, tarehe 14 Agosti 2019 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wote waliofariki dunia kwenye ajali ya Daraja la Morandi. Jimbo kuu la Genova, limeadhimisha Ibada maalum kwa ajili ya kumbu kumbu hii, ambayo imeacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za wananchi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika kumbu kumbu ya mwaka mmoja tangu Daraja la Morandi “Il Ponte Morandi” liporomoke na kuanguka chini hapo tarehe 14 Agosti 2018 na kupelekea watu 43 kupoteza maisha yao, wengine wengi kupata majeraha na vilema vya kudumu anasema, hili ni Fumbo la Msalaba katika maisha ya mwanadamu. Kuna watu 566 walilazimika kuyaacha makazi yao kwa vile hayakuwa tena salama kwa matumizi ya binadamu. Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anawataka waamini na watu wenye mapenzi mema  kamwe wasiruhusu matukio kama haya yavuruge umoja, upendo, mshikamano na mafungamano ya kijamii. Isiwe ni sababu ya kufutilia mbali kumbu kumbu pamoja na matukio muhimu yaliyojitokeza katika maisha yao. Kristo Yesu, akiwa ametundikwa Msalabani, watu wengi walimdhihaki, wakamtukana na kumdhalilisha; wakamchoma mkuki ubavuni, na hatimaye, akafa kifo cha aibu pale Msalabani. Kristo Yesu katika mambo yote alikuwa sawa na binadamu, isipokuwa hakutenda dhambi.

Katika shida na mahangaiko ya binadamu, Kristo Yesu, aliweza kuhuzunika, akatoa machozi, akawa faraja na chombo cha baraka kwa wale waliokuwa wanamzunguka. Katika shida na magumu ya maisha, waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema, wawe wepesi kumkimbilia na kumwangalia Kristo Yesu aliyetundikwa Msalabani, ili kujiaminisha na kujikabidhi katika ulinzi na tunza yake. Watambue kwamba, katika shida na mahangaiko yao, bado pia kuna Jumuiya ya Wakristo, kuna Kanisa mahalia la Genova na pamoja nao, Baba Mtakatifu Francisko pia anashiriki kikamilifu katika mateso na mahangaiko yao. Pale wanapotambua ukubwa wa udhaifu wao wa kibinadamu, hapo ndipo wanapoweza pia kutambua na kuthamini mahusiano na mafungamano yao ya kibinadamu; kifungo cha upendo kinachowaunganisha kama wana familia na jamii katika ujumla wake.

Kardinali Angelo Bagnasco, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Genova, Kaskazini mwa Italia, Jumatano, tarehe 14 Agosti 2019 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wote waliofariki dunia kwenye ajali ya Daraja la Morandi, mwaka mmoja uliopita. Jimbo kuu la Genova, limeadhimisha Ibada maalum kwa ajili ya kumbu kumbu hii, ambayo imeacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za wananchi wa Genova. Huu ni muda wa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano na wale wote walio baki pweke kutokana na ajali hii. Kardinali Bagnasco anawashukuru wale wote waliojisadaka kwa upendo na uzalendo katika kuokoa maisha ya watu waliokuwa wamekumbwa na mkasa huu. Huu ni upendo ambao ulikita mizizi yake katika matumaini, ujasiri na sadaka kubwa.

Genova, inataka kusimama tena na kuendelea na safari ya imani, matumaini na mapendo! Ajali hii imesababisha athari kubwa kwa watu na mali zako; gharama ya maisha imeongezeka maradufu, wakati hali ya maisha imeendelea kuchechemea. Kumekuwepo na uhaba mkubwa wa fursa za ajira pamoja na uchafuzi mkubwa wa mazingira. Pamoja na changamoto zote hizi, Genova imeanza kuona cheche za matumaini ya ujenzi wa Daraja Jipya litakalokamilika kunako mwaka 2020. Ni muda wa kushikamana, kutumaini, kuamini na kupendana kama ndugu; kwa kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii ndiyo kanuni ya dhahabu inayopaswa kuzingatiwa na wote. Haki jamii ipewe kipaumbele cha kwanza, uchoyo, ubinafsi na kinzani vifyekelewe mbali, ili kukazia maendeleo ya watu wa Mungu Genova!

Daraja la Morandi

 

14 August 2019, 14:06