Tafuta

Vatican News
Rais Filipe Jacinto Nyusi wa Msumbiji, hivi karibuni amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Askofu mkuu Piergiorgio Bertoldi. Rais amemsifu na kumpongeza Papa Francisko kwa utume wake! Rais Filipe Jacinto Nyusi wa Msumbiji, hivi karibuni amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Askofu mkuu Piergiorgio Bertoldi. Rais amemsifu na kumpongeza Papa Francisko kwa utume wake! 

Hija ya Papa Francisko Msumbiji: Rais ampongeza Papa & Kanisa

Rais Nyusi amelishukuru Kanisa kwa mchango wake mkubwa katika kuhamasisha: haki, amani, upatanisho na umoja wa kitaifaa Amempongeza na kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa sadaka na majitoleo yake kwa ajili ya maskini, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, haki, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, changamoto changamani katika ulimwengu mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kufanya hija ya kitume Barani Afrika kuanzia tarehe 4-10 Septemba 2019 kwa kutembelea Msumbiji, Madagascar pamoja na Mauritius. Kauli mbiu inayoongoza hija ya Baba Mtakatifu nchini Msumbiji ni: matumaini, amani na upatanisho. Kwa upande wa Madagascar ni “Mpanzi wa amani na matumaini na kauli mbiu ya familia ya Mungu nchini Mauritius ni “Hujaji wa amani”. Askofu mkuu Piergiorgio Bertoldi, aliyeteuliwa hivi karibu na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Balozi wa Vatican nchini Msumbiji, amewasilisha hati zake za utambulisho wakati huu Baba Mtakatifu Francisko anapojiandaa kuanza hija ya kitume nchini Msumbiji kama hujaji wa matumaini, amani na upatanisho. Askofu mkuu Piergiorgio Bertoldi, akiwa ameandamana na viongozi wakuu kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji chini ya Askofu mkuu Francisco Chimoio wa Jimbo kuu la Maputo, Msumbiji, walikutana na kuzungumza na Rais Filipe Jacinto Nyusi wa Msumbiji.

Katika mazungumzo yao, Rais Nyusi amegusia urafiki na uhusiano mwema wa kidiplomasia kati ya Vatican na Msumbiji; mchango wa Kanisa Katoliki katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Msumbiji hasa katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu. Rais Nyusi amelishukuru Kanisa kwa mchango wake mkubwa katika kuhamasisha: haki, amani, upatanisho na umoja wa kitaifa. Kwa namna ya pekee kabisa, amempongeza na kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa sadaka na majitoleo yake kwa ajili ya maskini, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, haki, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, changamoto changamani katika ulimwengu mamboleo. Askofu mkuu Piergiorgio Bertoldi alipata pia fursa ya kukutana na kuzungumza na viongozi mbali mbali wa Serikali ya Msumbiji, ili kuhakikisha kwamba, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Msumbiji, inakwenda kama ilivyopangwa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini Msumbiji.

Askofu mkuu Piergiorgio Bertoldi alipata pia fursa ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Jimbo kuu la Maputo, kwa kushirikiana na Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji. Katika Ibada hii ya Misa Takatifu, Askofu mkuu Piergiorgio Bertoldi aliwasilisha hati zake za utambulisho kutoka kwa Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na kupokelewa na Askofu Lucio Andrice Muandula wa Jimbo Katoliki la Xai-Xai, ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji.

Papa: Msumbiji

 

29 August 2019, 13:51