Tafuta

Vatican News
Kardinali Pietro Parolin anasema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika: Ujumbe: Amani na Upatanisho wa kidugu; Utunzaji wa mazingira; Utamaduni wa watu kukutana Kardinali Pietro Parolin anasema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika: Ujumbe: Amani na Upatanisho wa kidugu; Utunzaji wa mazingira; Utamaduni wa watu kukutana 

Hija ya Papa Francisko Barani Afrika: Amani, Mazingira & Upatanisho wa kidugu!

Kardinali Pietro Parolin katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, hija ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika kuanzia tarehe 4-10 Septemba 2019 inapania kukoleza mchakato wa amani na upatanisho wa kidugu; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na familia ya Mungu Barani Afrika kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Matayarisho yote ya hija ya thelathini na moja ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika kuanzia tarehe 4-10 Septemba 2019 kwa kutembelea Msumbiji, Madagascar pamoja na Mauritius yamekamilika. Familia ya Mungu Barani Afrika ina kiu ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu. Kauli mbiu inayoongoza hija ya Baba Mtakatifu nchini Msumbiji ni: matumaini, amani na upatanisho. Kwa upande wa Madagascar ni “Mpanzi wa amani na matumaini na kauli mbiu ya familia ya Mungu nchini Mauritius ni “Hujaji wa amani”. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, Injili ya amani; utunzaji bora wa nyumba ya wote na utamaduni wa watu kukutana ni kati ya tema ambazo zinatarajiwa kupewa uzito wa juu wakati wa hotuba mbali mbali za Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika. 

Hii ni hija ya pili ya kitume kwa Baba Mtakatifu Francisko kutembelea Bara la Afrika ambalo kwa hakika limejeruhiwa sana kwa vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Ni eneo ambalo kwa miaka ya hivi karibuni limekumbwa na majanga asilia, lakini bado lina imani na matumaini ya kuanza tena upya kujenga Injili ya matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi katika misingi ya haki, amani na maridhiano yanayofumbata majadiliano katika ukweli na uwazi!  Picha ya watu wengi nje ya Bara la Afrika ni ile ineyolionesha Bara la Afrika linalozama katika vita, magonjwa, umaskini na majanga mbali mbali na kusahau kwamba, Bara la Afrika limesheheni tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu anasema Kardinali Pietro Parolin. Baba Mtakatifu katika hija yake ya kitume Barani Afrika anataka kukazia mambo makuu matatu: Injili ya amani; utunzaji wa mazingira nyumba ya wote, mintarafu Waraka wa Kitume “Laudato si”, yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji bora wa nyumba ya wote” pamoja na utamaduni wa watu kukutana kama kikolezo cha Injili ya matumaini.

Baba Mtakatifu anapenda kutumia fursa hii kuhakikisha kwamba, anapyaisha matumaini ya watu wa Mungu Barani Afrika ili kuweza kupata suluhu ya vita, kinzani na mipasuko mbali mbali ya kijamii inayoendelea kujitokeza, sanjari na kujikita katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu, yanayogusa mahitaji yake msingi kiroho na kimwili; kwa kuheshimu na kuthamini kazi ya uumbaji. Bara la Afrika linapaswa kuwa ni kitovu cha maendeleo fungamani ya binadamu kama ambavyo aliwahi kusema Mtakatifu Paulo VI, kwa kuendelea kujikita katika Injili ya matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Baada ya Msumbiji kujipatia uhuru wake wa bendera kutoka kwa Wareno, ilijikuta ikiingia na kuzama katika vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyo sababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Ili kusitisha vita hii, FRELIMO na RENAMO waliwekeana sahihi Mkataba wa Amani kunako mwaka 1992 na huo ukawa ni mwanzo wa hija ya amani nchini Msumbiji.

Bado kuna changamoto ya kuhakikisha kwamba, amani ambalo ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu inadumishwa nchini Msumbiji, lakini hatua kubwa imekwisha kutekelezwa hadi sasa! Mkataba huu ulikuwa ni juhudi za Umoja wa Mataifa, Kanisa Katoliki, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio pamoja na Serikali ya Italia. Hayati Askofu Jaime Pedro Gonzalves anakumbukwa sana kwa mchango wake katika mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa nchini Msumbiji. Rais Nyusi amedhamiria na anataka kuhakikisha kwamba, Msumbiji inajenga na kudumisha misingi ya haki, amani na umoja wa kitaifa, ndiyo maana hivi karibuni, Chama cha FRELIMO kimewekeana tena sahihi Mkataba wa Amani na Chama cha RENAMO ambacho kwa sasa kinaongozwa na Bwana Ossufo Momade na ambacho ni Chama kikuu cha Upinzani nchini Msumbiji. Lengo ni kusitisha vita na mashambulizi dhidi ya watu wasiokuwa na hatia; pamoja na kuhakikisha kwamba, ulinzi na usalama wa Msumbiji unaendelea kuimarishwa.

Hakuna tena sababu msingi za vikosi vya ulinzi na usalama vya Serikali ya Msumbiji kushambuliana na majeshi ya RENAMO. Mkataba huu, unaweka matumaini makubwa katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa. Kardinali Parolin anakaza kusema, huu ndio umuhimu wa majadiliano katika ukweli na uwazi ili hatimaye, kuachana kabisa na falsafa ya kutumia mtutu wa bunduki” kwa kutambua kwamba, tofauti zao msingi ni sehemu ya amana na utajiri wa watu wa Mungu nchini Msumbiji. Baba Mtakatifu anasema, watu wanapaswa kuwa na mawazo na mwelekeo mpya katika kutafuta suluhu ya migogoro inayowaandama kama Jumuiya.

Baba Mtakatifu Francisko katika mafundisho yake anasema, Kanisa linawategemea sana maskini katika maisha na utume wake, kwani maskini ni amana na utajiri wa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kimsingi, maskini ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu. Dhana ya umaskini inajikita katika umaskini wa hali na mali; maadili na utu wema; kwani wote hawa Kristo Yesu amejisadaka kwa ajili ya kuwatangazia Injili inayoganga, inayoponya na kuokoa. Baba Mtakatifu Francisko anatembelea Magascar ambako kwa hakika Kanisa ni maskini; na kuna idadi ndogo ya Wakristo. Familia ya Mungu nchini Madagascar inakabiliwa na umaskini mkubwa unaochangiwa na uharibifu mkubwa wa mazingira, kinzani na mipasuko ya kisiasa na kijamii. Kardinali Parolin ambaye katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, alipata nafasi ya kutembelea Madagascar anasema, licha ya changamoto zote hizi, lakini watu bado wana ari na moyo wa kutaka kupiga moyo konde na kusonga mbele kwa imani na matumaini makubwa.

Changamoto kubwa nchini Madgascar ni ukosefu wa fursa za ajira kwa vijana wengi nchini humo, kiasi cha kuwakosesha matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Kuna kiwango kikubwa cha umaskini kinachowapekenya wananchi wa Madagascar. Ni matumaini ya Kardinali Parolin kwamba, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Madagascar itapyaisha Injili ya matumaini miongoni mwa vijana wa kizazi kipya kwa njia ya elimu bora na makini; kwa huduma bora za afya, dhamana na utume unaovaliwa pia njuga na Mama Kanisa nchini Madagascar. Jumatatu tarehe 9 Septemba 2019 Baba Mtakatifu atakuwa nchini Mauritius na kauli mbiu ya familia ya Mungu nchini Mauritius ni “Hujaji wa amani”. Kihistoria hii ni nchi ambayo iko njia panda, daraja linalowakutanisha watu katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene. Baba Mtakatifu katika mazingira haya anapenda kuwaimarisha watu wa Mungu kuendelea kujikita katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa watu wa kukutana, ili kwa pamoja waweze kusimama kidete katika kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Majadiliano ya kitamaduni ni muhimu sana nchini Mauritius anasema Kardinali Parolin, kwani hii ni nchi ambayo ina utajiri mkubwa wa lugha, mila na tamaduni za watu mbali mbali. Hii ni changamoto ya kuvunjilia mbali ubaguzi ili kuonesha moyo wa upendo na mshikamano kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi, yawasaidie waamini wa dini mbali mbali nchini humo kukabiliana na hatimaye, kutoa ufumbuzi wa kudumu wa changamoto mamboleo zinazowaandama walimwengu katika ujumla wao. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, uzoefu wake wa kwanza katika utume wa kidiplomasia umepata chimbuko lake Barani Afrika, hususan Afrika Magharibi, kumbe, anayo mapenzi mema na mtazamo chanya kwa Bara la Afrika. Jambo la msingi kwa watu wa Mungu Barani Afrika ni kuhakikisha kwamba, wao wenyewe wanajisikia kuwa ni wadau katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya katika ujumla wao.

Waafrika wanao uwezo wa kuzipatia ufumbuzi changamoto na matatizo wanayokabiliana nayo katika hija ya maisha yao. Ustawi na maendeleo ya Bara la Afrika yako mikononi mwa waafrika wenyewe. Kumbe wanapaswa kuwajibika barabara ili kupambana na vikwazo vinavyopelekea Afrika kujikuta inagubikwa na vita, kinzani na migogoro mbali mbali sanjari na kutafuta mambo yanayokwamisha mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Bara la Afrika halina budi kufanya maamuzi magumu kwa kuwachagua marafiki watakaosaidia mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu; kwa kutumia rasilimali na utajiri wa Bara la Afrika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika na wala si vinginevyo. Kanisa Barani Afrika linapaswa kuendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake kama familia ya Mungu inayowajibika katika misingi ya haki, amani na maridhiano. Ni jukumu la Kanisa la Kiulimwengu kulisaidia Kanisa Barani Afrika kuendelea kukua na kukomaa, ili liweze kuwa kweli ni chombo cha Injili ya huduma kwa watu wa Mungu Barani Afrika!

Kard. Parolin: Mahojiano

 

31 August 2019, 13:43