Tafuta

Vatican News
Waamini walei wana haki, dhamana na wajibu msingi katika maisha na utume wa Kanisa! Hawana budi kuwezeshwa kwa njia ya majiundo makini, ili watekeleze dhamana hii kwa vitendo! Waamini walei wana haki, dhamana na wajibu msingi katika maisha na utume wa Kanisa! Hawana budi kuwezeshwa kwa njia ya majiundo makini, ili watekeleze dhamana hii kwa vitendo!  (ANSA)

Dhamana na utume wa waamini walei ndani ya Kanisa: Ni muda wa vitendo zaidi!

Mkutano wa Chama cha Vijana Wakatoliki Hispania: 1 Agosti hadi tarehe 4 Agosti 2019, huko Avila, nchini Hispania: Kauli mbiu “Kutekeleza ndoto ya Mungu; majiundo ya waamini walei Parokiani” Dr. Ghison anasema, walei ni mhimili wa Kanisa kwani, wanaitwa kutekeleza: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo katika maisha yao, kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dhamana na utume wa waamini walei ndani ya Kanisa kwa namna ya pekee, ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican unaobainisha: wito, utume na dhamana ya waamini walei katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati. Waamini walei ni wadau pia katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa! Dr. Linda Ghisoni, Katibu mkuu msaidizi, Idara ya Walei, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha katika hotuba yake ya kufunga mkutano wa Chama cha Vijana Wakatoliki Nchini Hispania uliofunguliwa tarehe 1 Agosti hadi tarehe 4 Agosti 2019, huko Avila, nchini Hispania, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kutekeleza ndoto ya Mungu; majiundo ya waamini walei Parokiani” anasema, waamini walei ni mhimili wa Kanisa kwani, wanaitwa kutekeleza: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo katika maisha yao, kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, walei, kama washiriki wa huduma ya Kristo kuhani, nabii na mfalme, wanayo nafasi hai katika maisha ya Kanisa na katika utendaji wake. Ndani ya jumuiya za Kanisa matendo yao yanahitajika sana, kiasi kwamba pasipo haya hata utume wenyewe wa wachungaji huwa hauwezi kufikia mafanikio kamili.  Maana walei wenye roho halisi ya kitume, kama wale wanaume na wanawake waliokuwa wakimsaidia Mtume Paulo katika kueneza Injili (Taz. Mdo 18:18.26; Rum 16:3), wanawakirimia ndugu zao yale waliyopungukiwa, na wanaburudisha roho za wachungaji na za waamini wengine wa taifa la Mungu (Taz. 1Kor 16:17-18). Tangu baada ya Mtaguso Mkuu wa Vatican, kumekuwepo na uanzishwaji wa mashirika na vyama vya kitume sehemu mbali mbali za dunia na vyama hivi vimesaidia kukuza na kudumisha ari na moyo wa kimissionari, malezi na majiundo makini ya maisha ya: imani na uadilifu, Sakramenti za Kanisa pamoja na maisha ya sala; mambo muhimu yanayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini, kama kielelezo cha imani tendaji! 

Adhimisho la  Fumbo la Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa na hiki ni kiini cha maisha ya Parokia. Kimsingi, Fumbo la Ekaristi Takatifu linaadhimishwa siku ya Bwana; Jumuiya ya waamini inapopata nafasi ya kusikiliza, kutafakari Neno la Mungu na hatimaye, kutumwa kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao, kama kielelezo cha imani ntendaji! Neno Parokia, linapata asili yake kutoka katika lugha ya Kigiriki yaani “παρоικια” maana yake “Ujirani”. Kumbe, kwa maneno machache, Parokia ni kitovu cha maisha na utume wa Kanisa, mahali pa kuinjilisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, tayari kutoka kifua mbele kutangaza furaha ya Injili; huruma na upendo wa Mungu. Mababa wa Kanisa wanasema, sasa umefika wakati wa kuangalia ya mbeleni kwa matumaini zaidi, ili kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa zinazoendelea kujitokeza miongoni mwa waamini walei ndani ya Kanisa Katoliki, ili waendelee kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu.

Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana kwa mwaka 2018 wamekazia umuhimu wa Kanisa kupyaisha maisha na utume wa Parokia, ili kuleta mvuto na mashiko kwa vijana wa kizazi kipya pamoja na waamini katika ujumla wao, ili kujenga familia ya Mungu inayowajibikiana katika: imani, matumaini na mapendo. Dr. Linda Ghisoni anasema, waamini walei kamwe hawataweza kuyachachua na kuyatakatifuza malimwengu ikiwa kama watashindwa kutoka katika undani wa maisha yao kuwa kweli ni chumvi ya dunia na nuru ya mataifa. Mkutano mkuu wa Chama cha Vijana Wakatoliki Nchini Hispania umehudhuriwa na waamini walei 750 kutoka katika Majimbo 45, huku wakiwa wameambatana na Maaskofu pamoja na Mapadre wao. Waamini walei ndani ya Kanisa wanapaswa kutambua dhamana na wajibu wao kama wabatizwa, yaani watu waliozaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu; wanao wajibu na haki zao msingi zinazopaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa.

Kimsingi wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo mintarafu uhalisia wa maisha yao. Waamini walei daima wajibidishe kuchota utajiri na amana ya maisha yao ya Kikristo kutoka katika: Neno la Mungu, Sala, Sakramenti za Kanisa pamoja na Mafundisho Jamii ya Kanisa, dira na mwongozo wa jinsi ya kuyatakatifuza malimwengu. Waswahili wanasema, “kitu kizuri na chema, kula na ndugu yako”. Waamini walei watambue kwamba, amana na utajiri huu wanapaswa kuwashirikisha pia jirani zao kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene; katika kuyatakatifuza maeneo ya kazi pamoja na utume wa familia. Waamini walei wakiwa wamepyaishwa kutoka katika undani wa maisha yao, wanaweza sasa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu; watu wenye wenye uwezo wa kusikiliza kwa makini na kujibu kilio cha maskini wanaowazunguka; watu wanaoweza kuendeleza majadiliano katika ukweli na uwazi; ukarimu na upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Upya wa maisha unawataka waamini walei kujenga na kudumisha umoja, upendo, mshikamano na mafungamano ya dhati na viongozi wa Kanisa, ili kuwajibika barabara katika maisha na utume wa Kanisa, kila mwamini akijitahidi kutekeleza wajibu wake. Dr. Linda Ghisoni, Katibu mkuu msaidizi, Idara ya Walei, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha katika hotuba yake ya kufunga mkutano wa walei nchini Hispania, amewaangalisha kuwa macho dhidi tabia ya kudhani kwamba, wanaweza kufanya yote kwa nguvu na jeuri yao, kwa kumweka Mwenyezi Mungu pembezoni mwa vipaumbele, sera na mikakati ya maisha yao. Katika mtindo na mwelekeo kama huu vi vigumu sana kuweza kutekeleza ndoto ya Mungu katika maisha yao. Mwenyezi Mungu apewe kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji maparokiani na majimboni. Kwa njia hii, waamini walei wataweza kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani.

Kishawishi kingine ni kile cha kuendelea kubaki wakiwa wanaelea katika ombwe, bila kuzama na kumwilisha maana ya Kanisa na umuhimu wa malezi na makuzi ya awali na endelevu kwa waamini walei. Utakatifu wa maisha ni ushuhuda wenye mvuto katika utume wa Kanisa. Changamoto, matatizo na fursa mbali mbali zinazoendelea kuibuliwa ndani na nje ya Kanisa, ni mahali muafaka ambapo waamini walei wanaitwa na kutumwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu. Waamini walei wasikatishwe tamaa na dhuluma, nyanyaso na magumu wanayokabiliana nayo katika maisha na utume wao hapa duniani, bali waendelee kusimama kidete kama mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Huruma na upendo wa Mungu uwaimarishe na kuwapyaisha kutoka katika undani wa maisha yao!

Walei Hispania
10 August 2019, 15:46