Vatican News
Kuanzishwa kwa Chuo Cha "Redemptoris Mater" huko Macau, nchini China, ni jitihada za Mama Kanisa katika azma ya uinjilishaji Barani Afrika! Kuanzishwa kwa Chuo Cha "Redemptoris Mater" huko Macau, nchini China, ni jitihada za Mama Kanisa katika azma ya uinjilishaji Barani Afrika! 

Chuo cha "Redemptoris Mater" Mkakati wa Uinjilishaji Barani Asia

Chuo cha "Redemptoris Mater" kitaanza kufanya kazi mwezi Septemba 2019 kwa kuwapokea wanafunzi kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hili ni jibu makini kwa changamoto iliyotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II, aliyeonesha kwamba, Bara la Asia linapaswa kupewa msukumo wa pekee katika mchakato wa uinjilishaji. Papa Francisko anakazia ari na mwamko wa kimisionari.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ameridhia uamuzi wa Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu wa kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha “Redemptoris Mater kwa ajili ya Bara la Asia”, kitakachokuwa na makao yake makuu huko Macau, Magharibi mwa mji wa Hong Kong, nchini China. Chuo hiki kitaanza kufanya kazi mwezi Septemba 2019 kwa kuwapokea wanafunzi kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hili ni jibu makini kwa changamoto iliyotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II, aliyeonesha kwamba, Bara la Asia linapaswa kupewa msukumo wa pekee katika mchakato wa uinjilishaji. Kwa upande wake, Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” analihamasisha Kanisa kutoka kifua mbele kwenda kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa.

Chuo hiki kitaendea kusimamiwa na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, litakalosaidiana na Askofu mahalia na kinaweza pia kuwa na vitivo mbali mbali ndani na nje ya China. Kimsingi hii ni Seminari kuu ya Kanisa Katoliki inayoundwa na jumuiya ya walezi wanaolindwa na sheria za nchi. Lengo la Chuo kikuu hiki ni maandalizi ya malezi kwa kufuata mwongozo wa malezi ya Kipadre unaojulikana kama “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre” kama sehemu ya mchakato wa kulinda, kukuza na kudumisha wito na maisha ya Daraja Takatifu ya Upadre. Huu ni wito wenye thamani kubwa katika maisha na utume wa Kanisa unaopaswa kuhudumiwa kwa umakini mkubwa kwa kuheshimu dhamiri nyofu, wajibu unaotekelezwa kwa kwa unyenyekevu na uvumilivu mkubwa, ili kweli wakleri waweze kung’ara kati ya watu wa Mungu wanaowahudumia!

Chuo kitaendeleza malezi na majiundo ya Kikasisi kwa kujikita zaidi katika malezi kama ambavyo yamefafanuliwa kwenye Mwongozo wa Malezi ya Kipadre mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa na Makanisa mahalia katika mchakato wa malezi na majiundo ya kipadre. Ni mwongozo makini unaotoa sheria, kanuni na taratibu zinazopaswa kutekelezwa katika hija ya malezi ya majandokasisi na mapadre kama sehemu ya majiundo endelevu. Mkazo umewekwa katika majiundo ya maisha ya kiroho kwa kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha; umuhimu wa maisha ya Kisakramenti; Mafundisho Tanzu ya Kanisa bila kusahau malezi  na majiundo ya kiakili, kiutu na kichungaji kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko.

Mapadre watakaopata malezi na majiundo kutoka Chuoni hapo, kwa kufuata ushauri wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, wanaweza kutumwa kutekeleza utume wao kwenye Majimbo yakayoomba msaada ndani na nje ya Bara la Asia, kadiri ya mahitaji ya Makanisa mahalia. Mapadre wataweza kusaidiwa na familia za Jumuiya ya Njia ya Ukatekumeni Mpya. Baba Mtakatifu Francisko anasema, jumuiya inayosimikwa katika imani, matumaini na mapendo thabiti inakuwa ni chemchemi ya miito mitakatifu, ari na mwamko mpya wa kimisionari. Hii inatokana na ukweli kwamba, neema ya utume inabubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, inayowakirimia waamini ari na nguvu ya kuwa kweli ni wamisionari. Waamini walei wanahamasishwa kuwa ni wamisionari kwa watu wanaowazunguka kwa kuwasikiliza na kuwapatia huduma: kiroho na kimwili; kwani ushuhuda wenye mvuto na mashiko ni chachu ya uinjilishaji mpya inayokolezwa na Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Kumbe, hata malezi ya Mapadre hao wapya yataendelea kuzingatia kanuni, taratibu na njia za Jumuiya ya Njia ya Ukatekumeni Mpya. Chuo hiki kitajipambanua kikamilifu kwa kutoa mwelekeo wa pekee katika ari na mwamko wa kimsionari katika maisha na utume wa Kanisa. Ni katika muktadha huu wa malezi na majiundo makini, tangu awali, majandokasisi hawa watakuwa wanapikwa taratibu katika ari na mwamko wa kimisionari, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu. Chuo hiki kitakuwa chini ya ulinzi, usimamizi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mkombozi na Mtakatifu Yosefu, Baba mlinzi wa Familia Tafakatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Chuo hiki kitakuwa kinaadhimisha kumbu kumbu za watakatifu na mashuhuda wa imani kutoka Kanisa la Bara la Asia kwa ibada na uchaji mkuu!

Kardinali Filoni

 

 

 

 

01 August 2019, 13:36