Tafuta

Vatican News
Kardinali Marc Armand Ouellet anasema Barua Binafsi ya Papa Francisko "Ninyi ni nuru ya ulimwengu": Sheria mpya kwa ajili ya kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia ni matunda ya umoja. Kardinali Marc Armand Ouellet anasema Barua Binafsi ya Papa Francisko "Ninyi ni nuru ya ulimwengu": Sheria mpya kwa ajili ya kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia ni matunda ya umoja.  (ANSA)

Mapambano dhidi ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia: Ushirikiano!

Barua hii binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko “Ninyi ni nuru ya ulimwengu” ni sehemu ya utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa ili kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Hati hii ni matunda ya ushirikiano kutoka ndani na nje ya Sekretarieti kuu ya Vatican. Kashfa hii ni janga la kimataifa linalohitaji kupata ufumbuzi wa kimataifa kwa ushirikiano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Barua binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko “Motu proprio” ijulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia ni mbinu mkakati wa kichungaji kwa ajili ya kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Kwa muhtasari, barua hii inawataka Maaskofu na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kuwajibika barabara katika kushughulikia tuhuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Hadi kufikia mwezi Juni 2020, Mabaraza ya Maaskofu pamoja na Majimbo yote Katoliki yatapaswa kuwa na mfumo maalum utakaoiwezesha jamii kuwasilisha shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Wakleri na watawa kwa sasa wanatakiwa kisheria kuhakikisha kwamba, wanatoa taarifa kuhusu nyanyaso za kijinsia wanazozifahamu. Tangu sasa hakutakuwepo tena na mwanya wa kuwalinda watuhumiwa wa nyanyaso za kijinsia na kwamba, wale wote wanaotoa habari pamoja na waathirika wanapaswa kulindwa na kamwe waibezwe na kunyanyaswa!

Kardinali Marc Armand Ouellet, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, Barua hii binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko “Ninyi ni nuru ya ulimwengu” ni sehemu ya utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa ili kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Hati hii ni matunda ya ushirikiano kutoka ndani na nje ya Sekretarieti kuu ya Vatican. Hii ni sehemu ya mchango uliotolewa na wajumbe walioshiriki kwenye mkutano wa ulinzi wa watoto wadogo ndani ya Kanisa uliofanyika mwezi Februari 2019. Kashfa ya nyanyaso za kijinsia ni janga la kimataifa, lililokuwa linahitaji kupatiwa ufumbuzi wa kimataifa. Sheria hizi mpya zinaonesha umuhimu wa Sekretarieti kuu ya Vatican kushirikiana kwa karibu zaidi na Majimbo mahalia pamoja na Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, ili kuwahudumia vyema zaidi watu wa Mungu.

Kwa wale wote watakaotoa taarifa za shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa kwa nia njema watalindwa kisheria. Lakini wale watakaowachafulia wakleri na watawa sifa njema kwa shutuma za uongo, watapaswa kuwajibika! Kardinali Marc Armand Ouellet anakaza kusema, changamoto kubwa iliyoko mbele ya wakleri na watawa ni kuhakikisha kwamba, wanachuchumilia utakatifu wa maisha, kwa kufuata na kutekeleza sheria, kanuni na taratibu za Kanisa kwa kuendelea kuwa waaminifu mbele ya Mungu, Kanisa na waamini wanaowahudumia. Viongozi na wahudumu wa Injili wanahamasishwa kuwa kweli ni watangazaji na mashuhuda wa Injili ya Kristo kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya matendo yao yenye mvuto na mashiko. Wajibu na dhamana ya Askofu mkuu wa Kanda imeimarishwa katika mchakato wa kufanya uchunguzi na upelelezi ikiwa kama shutuma hizi zinaelekezwa kwa Askofu. Baba Mtakatifu anawahamaisha Maaskofu kushirikiana kwa karibu zaidi na waamini walei wenye sifa, ujuzi na maarifa katika kukabiliana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Viongozi wa Kanisa wanakumbushwa kwamba wao ni nuru ya ulimwengu!

Kard. Marc: Nyanyaso

 

 

22 August 2019, 14:44