Tafuta

Vatican News
Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela limetoa tamko la kupinga shutuma dhidi ya Askofu mkuu Edgar Pena Parra, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican. Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela limetoa tamko la kupinga shutuma dhidi ya Askofu mkuu Edgar Pena Parra, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican.  (ANSA)

Mshikamano wa Maaskofu wa Venezuela na Askofu mkuu Edgar Parra: Habari za kughushi ni hatari!

Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela linataka kuonesha mshikamano wa dhati na Askofu mkuu Edgar Peña Parra, ambaye kwa sasa ni Katibu mkuu msaidizi wa Vatican. Kanisa nchini Venezuela linatambua na kuthamini mchango wake katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Venezuela. Habari za kughushi zinalenga kuchafua utu na heshima yake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela limetoa tamko kuhusu habari za kughushi, potofu na zisizo na ukweli wowote kuhusiana na Askofu mkuu Edgar Peña Parra, Katibu mkuu Msaidizi wa Vatican. Baraza la Maaskofu linasema, Askofu mkuu Edgar Peña Parra ambaye kwa asili ni mzaliwa wa Jimbo kuu la Maracaibo, lililoko nchini Venezuela ni kiongozi anayefahamika ndani na nje ya Venezuela kutokana na huduma yake ya shughuli za kichungaji ndani ya Kanisa kwa takribani miaka thelathini sasa. Amemwalikisha Khalifa wa Mtakatifu Petro sehemu mbali mbali za dunia, kwa uaminifu, uadilifu na busara ya kichungaji. Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela linataka kuonesha mshikamano wa dhati na Askofu mkuu Edgar Peña Parra, ambaye kwa sasa  ni Katibu mkuu msaidizi wa Vatican.

Kanisa nchini Venezuela linatambua na kuthamini mchango wake katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Venezuela. Baadhi ya shutuma zinazotolewa dhidi ya Askofu mkuu Edgar Peña Parra zinasigana katika maeneo na muda ambamo matukio hayo yanayosemwa kwamba, yametendeka. Shutuma hizi zinazotolewa na baadhi ya wakleri zinapania pamoja na mambo mengine ni kutaka kuchafua jina, heshima na utume ambao umekuwa ukitekelezwa na Askofu mkuu Edgar Peña Parra katika maisha na utume wa Kanisa kwa sababu zao binafsi. Ni shutuma zinazotaka kumsadikisha Baba Mtakatifu Francisko kwamba, “anazungukwa na watu wasiokuwa makini”. Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela linawaalika watu wa Mungu nchini humo, kusali na kuomba huruma na upendo wa Mungu, ili uweze kutawala kati ya waja wake kwa kujikita katika ukweli ambao utawaweka huru badala ya kuendekeza “mchezo mchafu wa kuchafuliana majina, utu na heshima kama binadamu na kama Kanisa”.

Venezuela

 

23 August 2019, 12:00