Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Mapadre wote ni muhtasari wa maisha na utume wa Kipadre katika ulimwengu mamboleo! Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Mapadre wote ni muhtasari wa maisha na utume wa Kipadre katika ulimwengu mamboleo! 

Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Mapadre Duniani: Muhtasari wa Maisha!

Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Mapadre Wote Duniani, inaonesha: Ukuu, wito na utakatifu wa maisha ya Kipadre. Inakazia: maisha ya Kijumuiya, ili kukuza na kudukisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati miongoni mwa Mapadre. Ni kwa njia ya umoja na mshikamano, Mapadre wataweza kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika Maadhimisho ya Miaka 160 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney, Msimamizi wa Maparoko wote duniani, Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia Mapadre wote duniani, barua ya upendo na mshikamano wa kibaba, akiguswa na furaha ya huduma inayotolewa na Mapadre sehemu mbali mbali za dunia, kila kukicha! Hawa ni mapadre ambao wengine wamechoka na kudhohofu kwa afya mbaya na changamoto za maisha; kuna baadhi yao wametumbukia katika mateso na mahangaiko makubwa ya ndani kutokana na huduma yao kwa familia ya Mungu. Licha ya mambo yote hayo, Baba Mtakatifu anasema, Mapadre wanaendelea kuandika kurasa za maisha na utume wa Kipadre sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu katika barua hii anapenda kuwashukuru na kuwatia moyo Mapadre wote, wakitambua kwamba, wao kwa hakika ni marafiki wapendwa wa Kristo Yesu katika maisha na utume wao.

Baba Mtakatifu anasema, kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale, ameyaona mateso na mahangaiko ya ndugu zake Mapadre na kamwe haachi kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili yao, akiwakumbuka katika sala zake; anataka kuwafariji Mapadre wote katika nyoyo zao, ili hatimaye, waweze kuimba ukuu na utukufu wa Mungu katika maisha yao kwa njia ya huduma kwa watu wa Mungu. Askofu mkuu Jorge Carlos Patron Wong, Katibu mkuu wa Seminari, Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano kuhusu Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Mapadre Wote Duniani anabainisha kiini cha barua hii; umuhimu wa Padre katika maisha na utume wa Kanisa; Mapadre kama mashuhuda na vyombo vya matumaini kwa watu wa Mungu. Mapadre hata katika udhaifu wao, wawe na ujasiri wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi na wito wa Upadre, ili wasitumbukie katika upweke hasi na hatimaye kujikatia tamaa. Katika shida na mahangaiko yao ya ndani, Mapadre wawe na ujasiri wa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, daima wakiendelea kumjifunza Kristo Yesu kwa njia ya shule ya Bikira Maria.

Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Mapadre Wote Duniani, inaonesha: Ukuu, wito na utakatifu wa maisha ya Kipadre. Katika barua hii, Baba Mtakatifu anakazia pamoja na mambo mengine: Maisha ya Kijumuiya, ili kukuza na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati miongoni mwa Mapadre, huku wakisaidiana katika uhalisia wa maisha na utume wao. Ni kwa njia ya umoja na mshikamano, Mapadre wataweza kukabiliana uso kwa uso na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu ameandika Barua hii kama kiongozi na mchungaji mkuu anayetambua: furaha, shida, changamoto na fursa mbali mbali walizo nazo Mapadre katika maisha na huduma kwa watu wa Mungu. Barua hii ni matunda na safari ya utamaduni wa kukutana na kuzungumza na Mapadre kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kama njia ya kushirikishana: ukuu, utakatifu, changamoto na fursa mbali mbali zinazojitokeza miongoni mwa Mapadre kama wahudumu wa Neno, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya huruma yanayotekelezwa na Mama Kanisa sehemu mbali mbali za dunia.

Mtakatifu Yohane Maria Vianney ni mfano bora wa kuigwa katika upendo na ukarimu wa kichungaji; sadaka na utakatifu wa maisha unaomwilishwa katika huduma kwa watu wa Mungu. Wito na maisha ya Kipadre yanafumbatwa katika sadaka na majitoleo binafsi; huruma, upendo na unyenyekevu wa moyo; mambo ambayo mara nyingi yanafanyika sirini, lakini Baba yao wa mbinguni anayafahamu hayo yaliyofichika machoni pa waja wake. Mtakatifu huyu ni mfano bora wa kuigwa katika maisha kama mtu binafsi na kama Jumuiya ya Mapadre, wakitambua kwamba, wamepakwa mafuta kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili ya upendo na matumaini kwa watu wa Mungu. Licha ya udhaifu na mapungufu yanayooneshwa na baadhi ya Mapadre, lakini kuna umati mkubwa wa Mapadre wanaoendelea kuandika kurasa za ushuhuda wa utakatifu wa maisha yanayosimikwa katika sadaka na huduma kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia.

Mapadre hawa watakatifu ni nguzo muhimu zinazoendelea kulisimamisha Kanisa linapokabiliana na mawimbi mazito ya bahari katika ulimwengu mamboleo. Mapadre watambue kwamba, wao ni sehemu ya watu wa Mungu, wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Neno, Sakramenti na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili! Katika udhaifu na mapungufu ya kibinadamu, Mapadre wawe wepesi kukimbilia huruma na upendo wa Mungu; ulinzi na tunza ya Bikira Maria katika maisha na utume wao. Kashfa ya nyanyaso za kijinsia imegusa na kutikiza maisha na utume wa Mapadre sehemu mbali mbali za dunia! Baba Mtakatifu Francisko ameonesha umuhimu wa Kanisa kuambata toba na wongofu wa ndani, tayari kukumbatia upya na utakatifu wa maisha. Huu ni mwaliko na changamoto ya kuondokana na unafiki, hali ya kutaka kujikweza ili kuonekana na watu! Kwa njia ya unyenyekevu, Mapadre wajikabidhi mikononi mwa Roho Mtakatifu, ili aweze kuwasaidia kuambata upya huu wa maisha, kwa kutambua kwamba, toba na wongofu wa ndani ni changamoto endelevu katika maisha na utume wa Mapadre.

Mapadre watambue kwamba, wao ni wafuasi wa Kristo Yesu, mafanikio wanayoyapata katika utume wao, ni kazi ya Roho Mtakatifu na wala si kwa nguvu na jeuri, sera na mikakati yao binafsi, anasema Askofu mkuu Jorge Carlos Patròn Wong. Mapadre wawe ni vyombo na mashuhuda wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, aliyewaita, akawachagua, akawaweka wakfu na kuwatuma kwenda kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Maisha na utume wa Kipadre ni sadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Mambo msingi ya kuzingatia ni ukweli, uaminifu, uadilifu na ile furaha katika kutangaza na kushuhudia: utukufu na matendo makuu ya Mungu katika maisha yao. Mapadre wajenge na kudumisha umoja, urafiki, mshikamano na mafungamano ya dhati na Kristo Yesu katika maisha na utume wao; ili kuendelea kuboresha utakatifu wa watu wa Mungu ndani ya Kanisa. Mapadre wanapaswa kutambua na kuthamini kwamba, wao ni wahudumu wa Fumbo la Ekaristi Takatifu, kumbe, wanapaswa kujisadaka na kujimega bila ya kujibakiza.

Mapadre wasikubali kutumbukia katika upweke hasi unaoweza kuwapelekea katika hali ya kujikatia tamaa ya maisha. Watambue kwamba, katika maisha na utume wao, wanahitaji nguvu, neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kumbe, wanapaswa kujiaminisha na kujiweka katika ulinzi na tunza ya Mungu. Mapadre waendelee kushikamana na kufungamana katika maisha na utume wao. Kristo Yesu ni kielelezo cha mchungaji mwema na kwamba, Kanisa kila wakati linaendelea kupyaishwa kwa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu. Kumbe, Mapadre wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini kwa watu wa Mungu. Mapadre katika maisha na utume wao, watambue kwamba, wanaweza kujipatia nguvu, ari na mwamko mpya kwa: kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Wajenge na kudumisha maisha na utamaduni wa sala; maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na hasa zaidi Sakramenti ya Upatanisho, kwa kutambua kwamba, kimsingi wao ni wadhambi wa kwanza ambao wanapaswa kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Katika changamoto za ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, Mapadre wajitafutie Mwongozi wa maisha ya kiroho na kamwe wasijiamini kipumbavu! Ujenzi wa umoja na udugu wa Kipadre, iwe ni changamoto ya kuvaliwa njuga kila kukicha pasi na kukata tamaa. Ushuhuda wa Mapadre wengine, iwe ni fursa ya kujikita katika toba, wongofu na utakatifu wa maisha. Askofu mkuu Jorge Carlos Patròn Wong  anasema, Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa anayo nafasi ya pekee katika maisha na utume wa Mapadre. Bikira Maria amekuwa ni hujaji wa kwanza katika historia nzima ya ukombozi wa mwanadamu, pale alipokubali kwa moyo radhi kabisa kushiriki katika mpango wa Mungu kwa ajili ya ukombozi wa binadamu, kiasi cha kujiaminisha mbele ya Mungu na kupokea kwa wasi wasi na furaha kubwa ujumbe kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu. Akajulishwa kwamba, binamu yake Elizabeti, amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake, yeye aliyeitwa tasa!

Kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana mbele ya Mwenyezi Mungu. Bikira Maria akaondoka kwa haraka kwenda kumhudumia binamu yake, kielelezo makini cha mtume wa Bwana aliyejisadaka bila ya kujibakiza, kiasi hata cha kudiriki kusimama chini ya Msalaba na kupokea maiti ya mwanaye mpendwa, Kristo Yesu! Bikira Maria ni mfano na kielelezo cha imani ambaye amediriki kuwa ni mfuasi wa Mwanaye mpendwa Yesu Kristo na jirani zake, huu ndio mtindo na mfumo wa maisha unaopaswa kutekelezwa na Mapadre. Daima mapadre wajitahidi kukua na kukomaa katika imani, matumaini na mapendo; sanjari na kuendelea kujikita katika majiundo endelevu ili kuboresha huduma yao kwa watu wa Mungu. Kwa njia hii, mapadre wanaweza kujenga na kuimarisha umoja, udugu na upendo wao wa kikasisi. Hili ndilo lengo kuu ambalo linapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Padre anasema, Askofu mkuu Jorge Carlos Patròn Wong.

Mapadre wawe na kiu ya upendo kwa Mungu na jirani zao, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza katika maisha na utume wa kipadre. Watambue kwamba, wao ni madaraja, mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake; mambo ambayo wanapaswa kuwashirikisha wale wote wanaokutana nao katika safari ya maisha na utume wao kama Makuhani.

Barua Kwa Mapadre
07 August 2019, 16:15