Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu Protase Rugambwa: Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni: Ameongoza Jubilei ya Miaka 100 Parokia ya B.M.Mshindaji na Kutoa Daraja ya Upadre! Askofu mkuu Protase Rugambwa: Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni: Ameongoza Jubilei ya Miaka 100 Parokia ya B.M.Mshindaji na Kutoa Daraja ya Upadre!  (Vatican Media)

Jimbo Katoliki Kigoma: Miaka 100 Parokia B.M. Mshindaji & Mapadre: J. Hulilo & S. Tuhoye

Askofu mkuu Protase Rugambwa, katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni ameiongoza familia ya Mungu Jimbo Katoliki Kigoma, kusherehekea kilele cha Jubilei ya Miaka 100 ya Parokia ya Bikira Maria Mshindaji sanjari na kutoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi: Joseph Hulilo na Solomon Tuhoye. Jubilei ni muda wa kushukuru, kutubu na kuomba tena neema.

Na Askofu Mkuu Protase Rugambwa – Kigoma.

Wapendwa katika Kristo, Leo tunapoadhimisha rasmi Kilele cha Jubilei ya Miaka 100 ya Parokia ya Bikira Maria Mshindaji na kushuhudia kupewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa vijana wetu wawili, Joseph Hulilo na Solomon Tuhoye, kiliturujia tunasherehekea Kupalizwa Mbinguni Mama yetu Bikira Maria, ikiwa pia ni Sikukuu ya Jimbo letu la Kigoma. Napenda niwapongeze nyote kwa maadhimisho hayo makubwa, na kwa niaba ya Familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Kigoma niwashukuru wateule wetu (Joseph Hulilo na Solomon Tuhoye) kwa kuitikia wito wa kumtumikia Mungu na Familia yake, bila kuwasahau Wazazi, ndugu na jamaa pia walezi wao waliowasaidia kwa namna mbali mbali mpaka kufikia siku ya leo wanapopewa Daraja ya Upadre. Hongereni sana! Kila tarehe 15 ya mwezi wa nane Waamini Wakatoliki tunaalikwa kudhihirisha kwa njia ya adhimisho maalumu, kukiri tena na kuimarisha imani yetu Katoliki kwamba baada ya kumaliza safari ya maisha yake hapa Duniani, Bikira Maria alichukuliwa mwili na roho katika Utukufu wa mbinguni, ili Mama wa Yesu ashiriki mapema na kikamilifu katika Utukufu wa mwanae Mfufuka.

Pamoja na Elisabeti tunaalikwa leo tumshangilie Bikira Maria na kusema “Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa(Luka 1:42). Bikira Maria amebarikiwa kwa sababu ya imani yake kuu aliyokuwa nayo na kwa imani hiyo “Baraka” inayotolewa na Mungu kwa Bikira Maria inafikia ukamilifu wake katika kushiriki kwake Maria kwenye utukufu, kwani aliamini katika yote aliyosema Bwana. Mwenyezi Mungu anamtuza na kumzawadia tunu hiyo ikiwa ni matokea ya uaminifu wake katika wito alioitiwa, na jinsi alivyoishi wito huo akiyafuata daima mapenzi ya Mungu na hivyo kushirikiana na mwanae katika ukombozi wa mwanadamu. Sherehe ya kupalizwa mbinguni ni mwaliko kwa kila mmoja wetu kumwiga Mama yetu na kujifunza kwake kupokea kwa ukarimu, kwa furaha, kwa unyenyekevu, na kwa shukrani, miito yetu tuliyoitiwa. Ndugu zangu, katika imani na matumaini tunapenda tuipate “Baraka” hiyo aliyotunukiwa Mama yetu Bikira Maria ya kushiriki katika Utukufu wa Mungu na hivyo kupata uzima wa milele pamoja naye.

Hata hivyo, inatubidi tufahamu kuwa Mwenyezi Mungu atatukomboa na kutushirikisha utukufu wake iwapo sisi tutajitoa kwake kwa uhuru na utashi wetu. Kwa maneno mengine, inabidi tujifunze kutoka kwa Mama Maria kujiaminisha na kujitoa kwa Mwenyezi Mungu ili atubadilishe na kutuumba upya na yote yawezekana katika nguvu hiyo ya Imani kwake. Kwa namna ya pekee nawaalika Mapadre wateule (Joseph Hulilo na Solomon Tuhoye), wamwige Mama yetu Bikira Maria katika kuishi na kutekeleza matakwa ya wito na utume wa kipadre. Tunaamini kuwa leo hii mtaitikia rasmi na kwa hiari wito aliowaitia Mungu, na kwa utayari uleule wa Bikira Maria: “Ndimi Mtumishi wa Bwana, nitendewe ulivyonena”. Bikira Maria ni mfano na mwalimu wa utumishi (Ndimi Mtumishi wa Bwana). Katika Enjili tumesikia kwamba Bikira Maria baada ya kufunuliwa habari za ujauzito wa binamu yake Elizabeti, ambaye tayari alikuwa mama wa makamu, alienda kumuhudumia, kitendo ambacho ni kielelezo wazi cha moyo wa utumishi. Mwishoni mwa Enjili ya leo Mwinjili Luka anatwambia “Maria alikaa na Elizabeth kwa muda wa miezi mitatu hivi ndio akarudi nyumbani wake (Luka 1:56).

Licha ya kwamba Bikira Maria alikuwa ametunukiwa cheo kikubwa sana kuliko vyote duniani (kuwa Mama wa Mwana wa Mungu), hakusita kwenda kumtumikia Elizabeti. Na ninyi Mapadre wateule, kama vile ilivyo hata kwetu tuliowatangulia, lazima mkumbuke daima kuwa Upadre si ubwana wala ufahari, bali ni utumishi na kujitolea kwa kila hali katika kumtumikia Mungu na taifa lake (kuwa yote kwa watu wote), kwa mfano wa Bwana wetu Yesu Kristo Mchungaji Mwema ambaye “hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi (Taz. Mk 10:45). Kristo aliye Bwana na Mfalme alijitoa nafsi yake kwa ajili ya ndugu zake. Hali kadhalika na ninyi, ambao leo mnapewa heshima na dhamana ya kutenda katika jina na nafsi ya Kristo mwenyewe, tafuteni daima kuwatumikia wengine kuliko kutumikiwa, kuwa wadogo zaidi kuliko kutafuta ukubwa. Wakati wa karamu ya mwisho Yesu aliwaosha miguu mitume wake na kuwaambia: “Ikiwa mimi niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo hivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi” (Yoh 13:14). Hapo ndipo ulipo ukuu na uongozi katika Kristo, yaani kujinyenyekeza na kujishusha kwa njia ya utumishi.

Ufanisi na ubora wa huduma yenu vitategemea vile vile utayari wenu kutafuta siyo mapenzi yenu binafsi, bali mapenzi ya Yule aliyewatuma na mnayemwakilisha. Kama Bikira Maria, tangulizeni daima mapenzi ya Mungu na siyo maslahi yenu binafsi au mapendeleo yenu: Kwa kumwiga Bikira Maria nanyi, leo na daima, mwambieni Mungu: “nitendewe ulivyonena”! Iweni tayari kutekeleza matakwa ya wito wa Mungu kwenu kwa kujitoa kikamilifu kwake na kwa watu mtakaowatumikia. Kwa Mama yetu Bikira Maria, wito aliofunuliwa ulikuwa chemichemi ya furaha: “Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, na roho yangu imemfurahia Mungu Mwokozi wang...”. Padre anapaswa kuwa shuhuda na muhubiri wa Injili ya furaha. Papa Fransisko daima ameweka mkazo wa pekee juu ya furaha ya Injili, kiasi cha kuifanya dhana hiyo kuwa karibu kaulimbiu ya Utume wake. Baba Mtakatifu anazidi kutukumbusha kuwa Kanisa linainjilisha kwa njia ya ushuhuda na kuipeleka kwa wengine furaha tunayokuwa nayo kati yetu na Mungu.

Kama anavyosema Mwandishi mmoja (Viktor Frankl), furaha hii ni “matokeo ya kujitoa kwa mtu binafsi kwa ajili ya sababu iliyo kuu kuliko yeye mwenyewe.” Na ni nini kinaweza kuwa sababu kuu kuliko ile ambayo Mungu ametuitia? Kwa mantiki hiyo furaha ya Padre itategemea hasa utayari wake wa kujitoa kumtumikia Mungu na watu wake: hiyo ndiyo sababu iliyo kuu kuliko yeye mwenyewe. Ila haitoshi sisi wenyewe kuwa na furaha. Yatubidi kuwashirikisha wengine furaha yetu kama alivyofanya Bikira Maria kwa Familia nzima ya Zakaria, mpaka kitoto kichanga ndani ya tumbo la Elizabeti kikafikiwa na furaha hiyo. Katika Enjili tumesikia Elizabeti akishuhudia na kusema “sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu”. Nanyi mapadre wateule yawabidi muwe mashuhuda na chachu ya furaha kwa watu. Maisha yenu yanapaswa kuwa kama harufu nzuri ya ubani kwa Mungu na taifa lake, kama asemavyo Mt. Paulo Mtume katika barua yake ya pili kwa Wakorinto “Maana sisi ni kama harufu nzuri ya ubani ambayo Kristo anamtolea Mungu, harufu nzuri inayofikia wote, wanaookolewa na wanaopotea. Kwa wale wanaopotea, harufu hiyo ni kifo; lakini kwa wale wanaookolewa, harufu hiyo ni uhai. Nani basi, awezaye kushiriki katika kazi ya namna hiyo?” (taz. 2 Kor. 2:15,16).

Ni wazi, wito wowote una changamoto zake: hata Bikira Maria alikumbana na matatizo mengi. Mapema mwanzoni mwa wito wake, Wazee Simeoni na Anna walimwambia kwamba upanga utaingia moyoni mwake, wakiashiria changamoto nyingi ambazo angekumbana nazo. Hata sisi lazima tutambue na kujua tangu mwanzo kuwa pamoja na furaha za maisha na utume wa kipadre, kuna vilevile na magumu ambayo padre hana budi kuyakabili, hasa katika mazingira ya maisha ya leo. Tujiaminishe daima kwake yeye aliyetuita ambaye daima kama tutamtegemea atatulinda na kutuwezesha kuyakabili yale yatakayotaka kutuangusha na kutukatisha tamaa. Licha ya magumu na changamoto nyingi, Bikira Maria alibaki amejawa daima na matumaini na furaha. Kinga na tiba ya magonjwa ya kiroho katika maisha na utume wa Mapadre ni mahusiano ya karibu na ya moja kwa moja na Kristo, hasa katika maisha ya sala. Kristo mwenyewe anasema: kama vile tawi haliwezi peke yake kuzaa matunda lisipobaki katika mzabibu, hali kadhalika nanyi hamwezi kuzaa matunda msipokaa ndani yangu (Rej. Yoh. 15:4).

Wapendwa Waamini wote, nichukue fursa hii kuwakumbusha wajibu wenu wa kuwasindikiza Mapadri katika maisha na utume wao, hasa kwa njia ya sala, ushauri na ushirikiano, ili waweze kuwa wachunguaji wema na watakatifu. Katika Barua kwa Waebrania tunasoma kwamba kila kuhani amewekwa kwa manufaa ya watu katika mambo yamuhusuyo Mungu, kutolea zawadi na dhabihu kwa ajili ya dhambi zao, na kwamba huchaguliwa kutoka miongoni mwa watu (Rej. Waeb. 5:1). Ili waweze kuwa kweli wa manufaa kwenu na lengo la Mungu litimie, yawabidi ninyi kuwaombea daima na kuwasaidia kwa hali na mali. Sababu nyingine muhimu ya uwepo wetu hapa leo, ni kuhitimisha Jubilei ya Miaka 100 ya Parokia ya Bikira Maria Mshindaji. Japo kwa Mkristo kumshukuru Mungu ni wajibu wa kila siku, Jubilei kama hii ni fursa ya pekee kabisa ya kutazama nyuma tulikotoka na kumtolea Mwenyezi Mungu shukrani za dhati kwa mema mengi ambayo amelijalia Jimbo la Kigoma. Yatubidi kuyakumbuka na kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa, na kuyakabili ya mbeleni kwa imani na moyo wa matumaini.

Katika kipindi cha miaka 100 tangu Parokia ya Kigoma ianzishwe, Mungu ametenda makuu mengi kwa ajili ya watu wake; amewakirimia neema mbalimbali, hususan paji la imani Katoliki. Matunda ya uwepo wa Parokia hii kwa kipindi hicho cha miaka 100 hayakuwa ya kiroho tu bali hata ya kimwili na kijamii. Kumbe tunazo sababu nyingi sana za kumshukuru Mungu katika adhimisho hili, ikiwa ni pamoja na miito mbali mbali ambayo huchipua na kukua katika Parokia hii: yaani miito ya Upadre, miito ya Utawa, miito ya Ndoa, Makatekista, familia nzuri za kikristo, n.k. Tunapomshukuru Mungu, ni vizuri pia kuwakumbuka, kuwaenzi na kuendelea kuwaombea waanzilishi wa Parokia hii, mapadre (Wamisionari na wazalendo), watawa na walei, ambao walitolea maisha yao kwa ajili ya kufundisha imani na kujenga miundombinu ambayo sisi tumeikuta na mingi tunaendelea kuitumia. Wengi walishatutangulia mbinguni, lakini baadhi bado tunao kati yetu. Wale ambao tayari wamelala katika Kristo Mungu awajalie pumziko jema na thawabu awatengeayo watumishi wake waaminifu. Wanaoishi bado, tunawaombea baraka tele katika maisha yao ya hapa duniani na baadae tuzo mbinguni kwa kazi yao nzuri.

Jubilei hii imeangukia wakati ambapo Baba Mtakatifu Francisko anahimiza kwa nguvu zake zote mwamko mpya wa kimisionari. Miaka miwili iliyopita alitenga na kutangaza mwezi Oktoba 2019 uwe kipindi maalum kabisa cha kuhamasisha ari na moyo wa kimissionari katika Kanisa zima. Anatutaka sote, kila mmoja katika wito wake, kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya utume wa Kanisa. Alihimiza kuwa katika kipindi hicho cha mwezi wa kumi ujao, Waamini wote waweke mikakati mipya ya kuimarisha mahusiano yao na Kristo Yesu kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Neno la Mungu na Sala; wapange mbinu mpya za kuboresha elimu ya Biblia na Katekesi katika ngazi zote; wachochee na waboreshe huduma ya upendo kwa jirani na wahitaji kama kielelezo cha imani; na zaidi wadhamirie kwa dhati kuishi maisha ya ushuhuda ili waweze kuinjilisha hasa kwa njia ya matendo. Ikumbukwe kwamba imani katoliki imefika maeneo haya kwa njia ya Wamisionari walioitikia kwa ukarimu mwaliko wa Yesu: “… enendeni mkawafanye watu wa mataifa yote kuwa wanafunzi wangu: mkiwabatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu” (Mat 28:19). Kwa hiyo hata sisi inabidi tutoe mchango wetu wa hali na mali katika kumwagilia na kupalilia ile mbegu ya imani waliyoipanda wamissionari wa kwanza ili izidi kukua na kuwa mti mkubwa utakaooendelea kuzaa matunda ya kudumu katika eneo hili.

Katika Agano la Kale ambako tunakuta chimbuko la utamaduni na desturi ya kuadhimisha jubilei, jubilei ilikuwa fursa ya kutazama nyumba na kufanya tathmini ya maisha, ikiwa ni pamoja na kufanya toba na kuomba msamaha kwa makosa yaliyotendeka na pia kuweka mikakati kwa maisha mapya. Ukisoma sura ya 25 ya kitabu cha Walawi utakuta maelekezo kamili kuhusu mambo ambayo Waisraeli walipaswa kuyarekebisha katika maisha yao kila walipoadhimisha jubilei. Vivyo hivyo hata sisi wanafamilia ya Mungu ya Jimbo la Kigoma, Jubilei hii inapaswa kuwa fursa ya kutazama nyuma na kutathmini utume wetu kama Jimbo, kama Parokia, na kila mmoja wetu ajiulize ni jinsi gani amechangia katika kufanikisha au kukwamisha utume wa Kanisa hili mahalia. Kwa nguvu zetu, hatuwezi kitu kumbe yabidi baadaye tumrudie na tumuombe atuimarishe kwa nguvu ya Roho wake na hivyo atuwezeshe kuyafanya mapenzi yake kama atakavyo yeye. Nimalizie kwa kumpongeza tena kila mmoja wenu kwa siku hii ya furaha. Kwa namna ya pekee ninawapongeza sana Joseph Hulilo na Solomon Tuhoye, na kuwaweka chini ya ulinzi wa Mama Bikira Maria Mshindaji, Mama wa Kanisa na Mama wa Mapadri. Roho Mtakatifu awajaze nguvu ili daima muwe mashuhuda na mawakili waaminifu wa Kristo. Imana ishimwe!

Kigoma: Jubilei

 

 

 

16 August 2019, 15:09