Tafuta

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher anasema, Jumuiya ya Ulaya haina budi kuendeleza yale mambo msingi ya waasisi wake kwa kujikita katika nidhamu, maadili na utu wema. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher anasema, Jumuiya ya Ulaya haina budi kuendeleza yale mambo msingi ya waasisi wake kwa kujikita katika nidhamu, maadili na utu wema. 

Mkutano wa Urafiki wa watu nchini Italia: Changamoto za Bara la Ulaya

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, katika hotuba yake amekazia umuhimu wa kuzingatia haki binafsi, haki jamii na haki za kimataifa sanjari na kutekeleza wajibu wake, kwani hakuna haki bila wajibu. Lakini, ikumbukwe kwamba, haki na wajibu ni mambo yanayofumbatwa katika maisha ya kijamii, kwa ajili ya ustawi, maendeleo ya mtu binafsi na jamii katika ujumla wake. HAKI & WAJIBU.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano wa Urafiki kati ya Watu Nchini Italia huko Rimini: “Meeting per l’amicizia fra i popoli” uliozinduliwa tarehe 18  umehitimishwa tarehe 24 Agosti 2019. Mkutano wa mwaka huu ambao umeongozwa na kauli mbiu “Jina lako linapata chimbuko lake kwa yale mambo msingi unayopania” ilikuwa ni sehemu ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 40 “XL” tangu kuanzishwa kwa mkutano huu. Hizi zilikua ni juhudi za Mtumishi wa Mungu Don Luigi Giussani ambaye alithubutu kuwakushanya waamini kutoka katika medani mbali mbali za maisha ili kutafakari mambo msingi katika maisha yao, kama ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican katika hotuba yake alijikita zaidi katika tafakari ya kina kuhusu: “Haki na Wajibu Barani Ulaya. Mwaka 1979 – 2019” kama sehemu ya mchakato wa maadhimisho ya kumbu kumbu ya Miaka 40 tangu Mkutano wa Urafiki  Kati ya watu Nchini Italia huko Rimini ulipoanzishwa.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, kama sehemu ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya Miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Ulaya aliwarejesha tena viongozi wa Umoja wa Ulaya katika mambo msingi yaliyopewa kipaumbele cha kwanza na waasisi wao hapo tarehe 25 Machi 1957, ili kujiwekea sera na mikakati ya kukabiliana na changamoto mamboleo katika masuala ya kisiasa, kiuchumi, kitamaduni. Walikazia zaidi umuhimu wa kuwekeza katika: ustawi, maendeleo, utu na heshima ya binadamu: kwa kulinda na kudumisha maisha, udugu na haki, kama chachu muhimu sana ya mabadiliko Barani Ulaya, baada ya patashika nguo kuchanika wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Waasisi wa Umoja wa Ulaya walikazia kwa namna ya pekee zawadi ya maisha ya binadamu na haki zake msingi sanjari na umuhimu wa ujenzi wa umoja, udugu na mshikamano unaosimikwa katika: ukweli na haki; msingi wa sera za kisiasa, kisheria na kijamii Barani Ulaya.

Umoja wa Ulaya utaweza kudumu na kushamiri, ikiwa kama utaendelea kujikita katika uaminifu kwa mshikamano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu ndani na nje ya Bara la Ulaya. Hii ilikuwa ni changamoto ya kuvunjilia mbali kuta za utengenano, ili kuokoa maisha ya familia zilizokuwa zinaogelea katika dimbwi la umaskini, vita na mipasuko ya kijamii, mambo yanayoendelea kushuhudiwa hata katika ulimwengu mamboleo. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, katika hotuba yake amekazia umuhimu wa kuzingatia haki binafsi, haki jamii na haki za kimataifa sanjari na kutekeleza wajibu wake, kwani hakuna haki bila wajibu. Lakini, ikumbukwe kwamba, haki na wajibu ni mambo yanayofumbatwa katika maisha ya kijamii, kwa ajili ya ustawi, maendeleo ya mtu binafsi na jamii katika ujumla wake. Jumuiya ya Umoja wa Ulaya ni matokeo ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, ambayo wakati wa kuanzishwa kwake, ilijikuta ikiwa na wajibu mkubwa kwa wananchi wake.

Lakini, raia wanakumbushwa kwamba, ili kulinda uhuru wa watu, kuna haja ya kutunza na kudumisha amani na demokrasia; kwa kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa watu wa Bara la Ulaya pamoja na haki, ili kweli umoja uweze kutawala na kuota mizizi yake katika maisha ya wananchi wa Ulaya. Huu ni wajibu msingi kwa kila raia Barani Ulaya; wajibu ambao kimsingi unabeba ndani mwake sadaka na majitoleo hata kwa kuthubutu kufanya maamuzi magumu katika maisha. Waasisi wa Umoja wa Ulaya waliwataka wananchi wa Ulaya kujenga Umoja wa Ulaya kwa kusimama kidete: Kulinda na kutetea haki, amani na uhuru wa kweli. Lakini, walipaswa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ujenzi wa mshikamano unaoongozwa na kanuni auni. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher anasema, mwelekeo wa sasa ni tofauti sana na mawazo ya waasisi wa Umoja wa Ulaya, leo hii kinachopewa msukumo wa pekee ni mshikamano wa fikra na hisia bila kukita mizizi yake yake katika asili, utu na heshima ya binadamu; tayari kusaidiana wakati wa raha, shida na changamoto mbali mbali za maisha. Katika mawazo ya namna hii, haki na wajibu ni mambo yanayosigana sana katika uhalisia wa maisha ya wananchi wa Bara la Ulaya.

Ni katika hali ya watu kukengeuka na watu kutopea katika ubinafsi, leo Barani Ulaya kumeibuka zile zinazodaiwa kuwa ni “Haki mpya” kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko, haki  zinazosigana kwa mbali kabisa na utu, heshima na haki msingi za binadamu kama zilivyobainishwa kwenye Tamko la Haki Msingi za Binadamu lililotolewa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Matokeo yake ni: maamuzi mbele; uchoyo na ubinafsi; ubaridi na kutopea kwa imani pamoja ya kuyakuza malimwengu. Upendo na mshikamano kwa watu wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali si tena kati ya vipaumbele vya wananchi wa Bara la Ulaya. Kumekuwepo na tabia ya upotoshaji wa makusudi kuhusu haki msingi za binadamu; tafsiri ambazo kimsingi zinakinzana na utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwa macho makavu kabisa kwamba, huu ndio ukoloni wa kiitikadi.

Mtakatifu Yohane Paulo II katika Wosia wake wa Kitume baada ya Sinodi ya Maaskofu wa Bara la Ulaya, “Ecclesia in Europa” anasema, katika miaka ya hivi karibuni, upweke hasi, ubinafsi na uchoyo ni mambo ambayo yameongezeka kwa kasi kubwa sana, kiasi cha kuathiri hata tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; utengamano na mafungamano ya kijamii. Leo hii, familia Barani Ulaya si mali kitu! Ubaguzi wa rangi, dini na mahali wanapotoka watu, vimeongezeka, kiasi kwamba, mambo haya ya ovyo yanaanza kuzoeleka, kiasi cha kudai haki zake. Umoja wa Ulaya ulishindwa kusoma alama za nyakati na matokeo yake uchoyo na ubinafsi vikapekenya Mabenki na Taasisi za fedha; uchumi wa Ulaya na dunia nzima, ukayumba na kuteteleka, leo hii watu wengi wanaendelea kuteseka kwa kukosa fursa za ajira, ukata pamoja na kuelemewa na athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa. Kuna baadhi ya wanasiasa wanajitafuatia umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko; matokeo yake ni kuanza kusambaratika kwa Jumuiya ya Ulaya, baadhi ya nchi zikitaka kujitegemea zenyewe.

Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia, linaonekana kuwa ni kero na wala si tena utajiri na amana ya jamii inayotoa hifadhi. Bara la Ulaya limepoteza mwelekeo kuhusu haki na wajibu kwa wakimbizi na wahamiaji na kusahau kwamba, kuna mamilioni ya wananchi wa Bara la Ulaya ambao pia “wamezamia na kuloea katika nchi za watu wengine”. Usalama wa raia na mali zao, anasema Askofu mkuu Paul Richard Gallagh, umewafanya baadhi ya viongozi wa Nchi za Ulaya kushindwa kuangalia na kuguswa na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji, wanaotafuta: usalama, hifadhi na maendeleo yao. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, utume wa Kanisa Katoliki kwa Wakimbizi na Wahamiaji unafumbatwa katika mambo makuu manne: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi. Hawa ni watu wanaokimbia vita, dhuluma, nyanyaso, majanga asilia na umaskini, changamoto na mwaliko wa kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano!

Kanisa linaangalia watu hawa ambao wana historia, utu na heshima yao na wala si tu kwa idadi inayovumishwa kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii. Kuna haja ya kutambua, kuheshimu na kuthamini utu wa binadamu na haki zake msingi. Mshikamano wa upendo ni wajibu msingi kwa watu wote bila upendeleo na kwa waamini hii ni sehemu ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Mshikamano huu unapaswa pia kuendelezwa kati ya serikali na mataifa mbali mbali, kwa kutambua kwamba, mataifa yote haya yanaunda familia ya Mungu duniani. Wakimbizi na wahamiaji wanapaswa pia kujenga ari na moyo wa mshikamano na mila, desturi, sheria, taratibu na kanuni za watu wanaowapokea na kuwapatia hifadhi. Wakimbizi na wahamiaji wana haki na wajibu wanaopaswa kuutekeleza, ili kweli uwepo wao, uwe ni wa manufaa kwa ajili yao wenyewe pamoja na wenyeji wao.

Rimini 40 Yrs
24 August 2019, 14:29