Vatican News
Watoto wanaoishi katika maeneo ya vita, kinzani na migogoro mbali mbali wanaathirika sana katika malezi na makuzi yao kwa sasa na siku za usoni. Watoto wanaoishi katika maeneo ya vita, kinzani na migogoro mbali mbali wanaathirika sana katika malezi na makuzi yao kwa sasa na siku za usoni.  (AFP or licensors)

Madhara kwa watoto wanaoishi katika maeneo ya vita na kinzani!

kuna umati mkubwa wa watoto ambao wamepelekwa mstari wa mbele kwenye mapambano kama chambo cha vita. Hawa ni watoto ambao haki zao msingi zimesiginwa kama “soli ya kiatu”. Kinachoangaliwa hapa ni malighafi na madini kutoka Barani Afrika yakayosaidia kuendesha viwanda katika nchi tajiri zaidi duniani. Watoto hawa wanapigana vita kama chambo tu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna maswali mengi ambayo mwanadamu anajiuliza katika safari ya maisha yake hapa duniani, lakini, anashindwa kupata majibu muafaka kwani, majibu makini yanafumbatwa katika Fumbo la Mwenyezi Mungu! Mwanadamu katika udhaifu na unyonge wake, anaweza kuyaangalia yote haya kwa jicho la huruma, mapendo na udadisi mkubwa! Anaweza kusikiliza kilio na mahangaiko ya watu, akabaki akiwa amepigwa butwaa na kujiuliza kwanini haya yanatendeka? Mwanadamu anapoguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya jirani zake, anaweza kuangua kilio na kuteseka pamoja nao, kama kielelezo cha ushuhuda wa upendo na mshikamano. Anaweza pia kuamua kutojali na hatimaye, kupitia kando kama inavyojionesha katika mfano wa Msamaria mwema!

Kisheria mtoto ni mtu mwenye umri walau chini ya miaka 18 na kwamba, kuna haki msingi ambazo mtoto anapaswa kupewa kwa kuzingatia sheria za kitaifa na kimataifa. Kimsingi, ustawi wa mtoto: yaani furaha, amani na utulivu ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee na taasisi, serikali na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake. Mtoto anayo haki ya kuishi huru, bila kutengwa kutokana na jinsia, rangi, umri au dini yake! Lakini si ajabu kukutana na watoto ambao wanaishi katika mazingira ya vita na machafuko ya kila aina kiasi kwamba, watoto hawa wanajikuta wakikabiliwa na matatizo na changamoto mbali mbali katika maisha, malezi na makuzi yao. Wakati mwingine watoto hawa wanalazimika kuzikimbia familia zao, hali inayohatarisha matumaini yao kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, inabuni mbinu mkakati wa kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ya vita na kinzani. Huu ni mchango uliotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, wakati alipokuwa akichangia mada kuhusu mbinu mkakati wa kuwalinda watoto wanaoishi katika mazingira ya vita, yanayopelekea mara kwa mara watoto kama hawa kunyimwa haki zao msingi na matokeo yake wanawakuwa ni watu wanaonyanyasika na kudhalilishwa utu na heshima yao kama binadamu. Vita haina macho, kumbe, katika mazingira ya vita, hata watoto pia wanajikuta wakipoteza maisha. Licha ya asilimia kubwa ya watoto hawa kupatwa na athari kubwa za kisaikolojia, majeraha na madonda makubwa mwilini wao, hata familia pamoja na jamii zao zinakumbwa na madhara makubwa!

Taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa inaonesha kwamba, kuna umati mkubwa wa watoto ambao wamepelekwa mstari wa mbele kwenye mapambano kama chambo cha vita. Hawa ni watoto ambao haki zao msingi zimesiginwa kama “soli ya kiatu”. Kinachoangaliwa hapa ni malighafi na madini kutoka Barani Afrika yakayosaidia kuendesha viwanda katika nchi tajiri zaidi duniani. Hawa ni watoto wanaolazimishwa kupigana vita si kwa ajili ustawi, maendeleo na mafao yao, bali kwa ajili ya wajanja wachache ndani ya jamii. Kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuchunguza dhamiri na hatimaye kubainisha chanzo kikuu cha watoto kupelekwa mstari wa mbele kama chambo cha vita. Hali ngumu ya uchumi na kijamii ni kati ya mambo yanayopelekea kuibuka kwa vita sehemu mbali mbali za dunia.

Udini, ukabila, siasa za chuki; uchu wa mali na madaraka ni kati ya mambo yanayoendelea kuchochea kasi ya vita na mipasuko duniani. Ukosefu wa kanuni maadili, utu wema pamoja na kumong’onyoka kwa maadili na utu wema ni kati ya mambo ambayo pia yamewapelekea vijana kukosa dira na msimamo thabiti wa maisha, na matokeo yake wanakuwa wepesi sana kutekwa mawazo na hatimaye, kutumbukizwa katika mtego wa vita na kinzani. Askofu mkuu Bernardito Auza amekazia mambo makuu yafuatayo yanayopaswa kupewa kipaumbele na Jumuiya ya Kimataifa kama sehemu ya mbinu mkakati wa kuwahudumia watoto wanaoishi katika maeneo ya vita, kinzani na migogoro mbali mbali. Jumuiya ya Kimataifa ikumbuke kwamba, inawajibu wa kuwalinda watoto, kuhakikisha kwamba, watoto waliokuwa vitani wanarejeshwa tena kwenye familia na jamii zao pamoja na kuhakikisha kwamba, watoto wanapata nafasi ya masomo yatakayowajengea uwezo wa kupambana na hali pamoja na mazingira.

Mosi, wawajibishwe kisheria wale wote wanaowapelekea watoto mstari wa mbele kama chambo cha vita; wanaowatumbukiza watoto katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Sheria ishike mkondo wake kwa wale wote watakaokamatwa wakiwateka nyara watoto, kuwanyanyasa na kuwanyonya watoto. Jambo la msingi ni kuhakikisha haki msingi za binadamu zinalindwa na kudumishwa sanjari na kuzingatia sheria za kitaifa na kimataifa zinazowalinda watoto wadogo. Pili, Watoto waliokuwa mstari wa mbele vitani wanaporejea wasaidiwe kuingia katika jamii zao; kwa kupewa mafunzo maalum yatakayowasaidia kurekebisha tabia mbaya walizojifunza wakati wakiwa vitani. Juhudi hizi zifanywe kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya mtoto mwenyewe na jamii katika ujumla wake. Ilikufanikisha zoezi hili kuna haja ya kutenga rasilimali fedha na watu, ili hatimaye, kuwajengea watoto matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Tatu, Jamii ihakikishe kwamba, watoto wanapata elimu kama sehemu ya haki zao msingi, ili hatimaye, waweze kuwa ni wajenzi na mashuhuda wa haki na amani kwa siku zijazo. Elimu ni muhimu sana katika mapambano dhidi ukosefu wa usawa na umaskini kama inavyobainishwa kwenye Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Vita ina athari kubwa si tu kwa maisha ya watu, hata katika miundo mbinu ya elimu, afya na barabara. Mara nyingine maeneo haya yamekuwa yakishambuliwa sana wakati wa vita, kiasi cha kuwanyima watoto fursa ya kupata elimu na afya bora. Sheria za Kimataifa hazina budi kuwawajibisha wahusika wote. Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko alionesha masikitiko yake kuhusu madhara ya vita inayoendelea huko Yemen pamoja na hatma ya maisha ya watoto wa Yemen ambao kwa sasa wanakabiliwa na njaa pamoja na utapia mlo wa kutisha.

Watoto wanapaswa kulindwa dhidi ya mashambulizi ya makundi yenye silaha pamoja na kuendelea kuwasaidia kukuza na kudumisha ndani mwao utamaduni wa haki, amani na maridhiano. Jumuiya ya Kimataifa iwe na sera na mikakati makini ya kuzuia majanga ya vota kabla hayajatokea. Maamuzi mbali mbali yaliyokwisha kufikiwa na Jumuiya ya Kimataifa hayana budi kutekelezwa ili kulinda na kudumisha haki msingi za watoto sehemu mbali mbali za dunia. Protokali ya ulinzi, usalama na haki msingi za watoto walioko kwenye mstari wa mbele vitani inapaswa kutekelezwa kwa vitendo. Askofu mkuu Bernardito Auza anahitimisha mchango wake kuhusu mpango mkakati wa Jumuiya ya Kimataifa kuwalinda watoto wanaoishi katika mazingira ya vita, kinzani na migogoro mbalimbali duniani, kwa kuhakikisha kwamba, watoto hawa wanakombolewa kutoka katika mazingira ha ya vita. Wajengewe uwezo wa kurejea na hatimaye, kushirikishwa tena katika maisha ya kijamii na kifamilia. Utu, heshima na haki zao msingi zinapaswa kulindwa na kudumishwa na wote!

Watoto Vitani
06 August 2019, 15:15