Tafuta

Vatican News
Tahariri: Dr. Andrea Tornielli anachambua umuhimu wa Barua ya Baba Mtakatifu Francisko aliyowaaandikia Mapadre wote Duniani; miaka 160 tangu afariki Mtakatifu Yohane. M. Vianney. Tahariri: Dr. Andrea Tornielli anachambua umuhimu wa Barua ya Baba Mtakatifu Francisko aliyowaaandikia Mapadre wote Duniani; miaka 160 tangu afariki Mtakatifu Yohane. M. Vianney.  Tahariri

TAHARIRI: Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Mapadre Duniani kote!

Baba Mtakatifu Francisko ametumia maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 160 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney kuwashukuru Mapadre kwa huduma ya: Neno, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya huruma. Kuna umati mkubwa wa Mapadre sehemu mbali mbali za dunia, wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa watu wa Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 160 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney, Msimamizi wa Maparoko duniani, amewaandikia barua mapadre wote duniani, kuwaonesha upendo na mshikamano wake wake wa kibaba. Katika barua hii anagusia mateso wanayokabiliana nayo kutokana na changamoto mbali mbali za: wito, maisha na utume wa Kipadre. Baba Mtakatifu anataka kuwatia shime, ari na moyo mkuu Mapadre ili waweze kusonga mbele, huku wakiendelea kupandikiza mbegu ya matumaini inayofumbatwa katika toba, wongofu wa ndani, upya na utakatifu wa maisha. Baba Mtakatifu anasema, katika shida na magumu ya maisha, Mapadre wajenge utamaduni wa kufarijiana na kutiana shime, ili kuweza kupambana na changamoto hizi uso kwa uso badala ya kuzikimbia na kutaka kuzigeuzia kisogo. Mapadre wasikubali kukata wala kukatishwa tamaa, bali waonje uwepo mwanana wa jirani zao, ili kuganga na kuponya uchungu wa moyo ili wasitumbukie katika upweke hasi!

Watambue kwamba, sala ya makuhani inaboreshwa kwa kumwilishwa katika huduma kwa waamini wao. Mapadre wajenge utamaduni wa kuwa na washauri wa maisha ya kiroho; wasumbukiane na kutaabikiana: wakati wa raha na wakati wa shida. Mapadre wajitahidi kuwa kati pamoja na watu wanaowahudumia. Mang’amuzi ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yawasaidie Mapadre na waamini katika ujumla wao kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati, tayari kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa ukuu na utukufu, kwa ajili ya: wito, maisha na utume wa Kipadre miongoni mwa watu wa Mungu. Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika Tahariri yake kuhusu Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Mapadre Wote Duniani.

Anasema, Papa Francisko ametumia maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 160 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney kuwashukuru Mapadre kwa huduma ya: Neno, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya huruma. Kuna umati mkubwa wa Mapadre sehemu mbali mbali za dunia, wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa watu wa Mungu! Kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa imesababisha madhara makubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Zimekuwa kama upanga wenye makali kuwili ambao umepenya kabisa katika undani wa maisha na utume wa Mapadre. Hali hii imezua wasi wasi na mashaka miongoni mwa waamini kwa Mapadre waliohusika na hata wale ambao hawakuhusika hata kidogo. Haya ni madonda ambayo yanaendelea kuchuruzika damu katika Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Mtakatifu Yohane Maria Vianney anawekwa mbele ya macho ya Mapadre kama mfano bora wa kuigwa, kutokana na sadaka pamoja na majitoleo yake yaliyomwezesha kujitosa kimasomaso kwa ajili ya huduma kwa Mungu na watu wake.

Baba Mtakatifu amesimama kidete kukemea na kuwaonya Mapadre pale walipokengeuka na kutopea katika dhambi. Lakini, anawapongeza Mapadre wote ambao wameendelea kuwa waaminifu na wenye imani thabiti katika maisha na utume wao kama Mapadre. Baba Mtakatifu ameandika Barua kwa Mapadre Wote Duniani kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma na kuitia mkwaju kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano mjini Roma, Makao Makuu ya Jimbo kuu la Roma. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa Mapadre, anataka kuwatia moyo na shime pamoja na kuwafariji kutokana na changamoto mbali mbali wanazokumbana nazo katika hija ya maisha na utume wao kama Mapadre. Hawa ndio wale Mapadre ambao asubuhi na mapema wako, tayari kufungua malango ya Kanisa ili kuwahudumia watu wa Mungu kwa Neno la Sakramenti za Kanisa. Kuna Mapadre ambao wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi; hawa ni wale wanaohitaji neno, faraja pamoja na kuwasindikiza katika hija ya maisha na utume wao ndani ya Kanisa.

Baba Mtakatifu anawakumbuka na kuwashukuru kutoka katika undani wa moyo wake, Mapadre ambao kila kukicha wanachakarika, kuwatembelea waamini wao, ili kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa pamoja nao; huku wakihuzunika na wale wanao huzunika; wakiomboleza na wale wanao omboleza na kufurahi na wale wanaokula “kuku kwa mrija”. Baba Mtakatifu anawakumbuka Mapadre ambao kutokana na huduma yao, wamekuwa wakihatarisha maisha yao kila kukicha! Bado anaendelea kuwakumbuka Mapadre wanaosafiri mwendo mrefu kwenda vijijini; pamoja na Mapadre wanaopiga kasia kila siku, kuwaendelea waamini walioko visiwani. Anawakumbuka Mapadre wanaopanda baiskeli na piki piki ili kuwaendea wagonjwa na kuwapatia huduma. Yote haya anasema Dr. Andrea Tornielli ni sadaka na majitoleo ya Mapadre. Huu ndio ukuu na utakatifu wa wito na maisha ya Kipadre, ambao si rahisi sana kuweza kuonekana na watu wa Mungu. Kwa bahati mbaya, watu wameyazoea kiasi kwamba, si sehemu ya habari tena.

Huu ni ukuu na utakatifu wa huduma ya Mapadre kwa watu wa Mungu hata kama haionekani kwa macho ya kibinadamu, lakini, watu wanaweza kuandika vitabu, kiasi hata cha kuujaza ulimwengu kama anavyosema Mwinjili Yohane kuhusu maisha na utume wa Kristo Yesu. Huu ni ukuu wa sadaka ya maisha inayotolewa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya jirani. Wadau wakuu wanaendelea kujiaminisha katika huruma, upendo na neema ya Mungu. Hawa ndio Mapadre “wadhambi, waliotubu na kusamehemewa dhambi zao”, kama hata ambavyo Baba Mtakatifu Francisko anavyojitambulisha mwenyewe. Hii ni kwa sababu ameonja huruma na upendo katika maisha na utume wake, kiasi hata cha kujiaminisha kwa Mungu na kuendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika Tahariri yake kuhusu Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Mapadre Wote Duniani anasema, baada ya mtikisiko uliowakumba Mapadre sehemu mbali mbali za dunia, kulikuwa na haja ya kuwapatia neno la kuwatia shime; kwa kuendelea kuthamini wito, maisha na utume wao, licha ya mapungufu ya kibinadamu yanayoweza kuwaandama katika maisha na utume wao. Uchungu na mateso yaliyosababishwa na Mapadre wachache waliotumbukia kwenye Kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa, kisiwe ni kisingizo cha kushindwa kutambua na kuthamini sadaka, uaminifu na majitoleo makubwa yanayotekelezwa na Mapadre katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa.

Mapadre licha ya udhaifu na mapungufu yao kibinadamu, lakini bado wanaendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko amechukua nafasi ya maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 160 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney, kuwashukuru Mapadre kwa kuendelea kuwahudumia watu wa Mungu; wawe na ari na mwamko mpya wa kuendelea kusema, “Mimi hapa Bwana nitume” kama sehemu ya kumbu kumbu ya siku ile walipoitwa na kuitikia kwa mara ya kwanza katika maisha!

Tornielli: Tahariri

 

05 August 2019, 12:10