Tafuta

Vatican News
Vatican na Urussi, tarehe 4 Julai 2019 wametiliana sahihi Mkataba wa Makubaliano "MOU" ya Ushirikiano wa kitabibu na tafiti za kisayansi kwa ajili ya magonjwa ya watoto wadogo! Vatican na Urussi, tarehe 4 Julai 2019 wametiliana sahihi Mkataba wa Makubaliano "MOU" ya Ushirikiano wa kitabibu na tafiti za kisayansi kwa ajili ya magonjwa ya watoto wadogo! 

Vatican na Urussi watia sahihi Mkataba wa Makubaliano: Afya!

Serikali ya Urussi na Vatican, Alhamisi tarehe 4 Julai 2019 wametiliana sahihi Mkataba wa Makubaliano, “MOU” ya ushirikiano wa kitabibu na tafiti za kisayansi kati ya Vatican na Urussi. Makubaliano haya yanalenga kujenga ushirikiano wa dhati kati ya Hospitali ya Bambino Gesù maarufu sana kwa tiba ya magonjwa ya watoto duniani pamoja na Hospitali zinazoendeshwa na Serikali ya Urussi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa niaba ya Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican pamoja na Veronika Skvortsova, Waziri wa Afya, kwa niaba ya Serikali ya Urussi, Alhamisi tarehe 4 Julai 2019 wametiliana sahihi Mkataba wa Makubaliano, “MOU” ya ushirikiano wa kitabibu na tafiti za kisayansi kati ya Vatican na Urussi. Makubaliano haya yanalenga kujenga ushirikiano wa dhati kati ya Hospitali ya Bambino Gesù maarufu sana kwa tiba ya magonjwa ya watoto duniani pamoja na Hospitali zinazoendeshwa na Serikali ya Urussi.

Tukio hili limehudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka Vatican na Hospitali ya Bambino Gesù na upande wa Urussi, ujumbe wake umeongozwa na Veronika Skvortsova, Waziri wa Afya nchini Urussi. Mama Mariella Enoc, Rais wa Hospitali ya Bambino Gesù ameutembeza ujumbe wa Urussi na kujionea wenyewe tafiti mbali mbali zinazofanywa na Hospitali ya Bambino Gesù mintarafu magonjwa ya watoto. Wameoneshwa tafiti za hali ya juu zilizotekelezwa hivi karibuni kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu kabisa katika mapambano dhidi ya magonjwa yanayoshambulia chembechembe za mfumo wa kinga mwilini, magonjwa ya kurithi pamoja na saratani ya damu maarufu kama ugonjwa wa Leukemia.

Mkataba wa Makubaliano “MOU” unaendelea kuimarisha ushirikiano ambao umekuwepo kati ya Hospitali ya Bambino Gesù na baadhi ya Hospitali za Watoto nchini Urussi katika masuala ya mafunzo maalum kwa ajili ya madaktari bingwa wa magonjwa ya watoto pamoja na protokali ya uchunguzi na tiba ya ugonjwa wa kifafa kwa watoto nchini Urussi. Utiwaji wa sahihi wa Mkataba wa Makubaliaono “MOU” kati ya Vatican na Urussi pamoja na Veronika Skvortsova, Waziri wa Afya nchini Urussi kutembelea Hospitali ya Bambino Gesù ilikuwa ni sehemu ya utekelezaji wa ratiba ya ziara ya Rais Vladimir Putin wa Urussi kutembelea Vatican, kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko na hatimaye, kukutana na viongozi mbali mbali wa Serikali ya Italia.

Vatican: Urussi: Mkataba

 

05 July 2019, 15:11