Tafuta

Mahakama, Vikosi vya ulinzi na usalama vya Vatican vimejiridhisha kwamba, Kaburi lililoshukiwa kuwa na masalia ya Emanuela Orlandi, ni tupu: Vatican huu ni ukweli na uwazi! Mahakama, Vikosi vya ulinzi na usalama vya Vatican vimejiridhisha kwamba, Kaburi lililoshukiwa kuwa na masalia ya Emanuela Orlandi, ni tupu: Vatican huu ni ukweli na uwazi!  Tahariri

TAHARIRI: Kaburi ni tupu, hakuna masalia ya Emanuela Orlandi!

Vatican: Ukweli na uwazi: Zoezi hili limefanywa kwa ushuhuda wa ndugu na jamaa ya Emanuela Orlandi, viongozi wa Mahakama pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama vya Vatican. Hakuna masalia ya binadamu yaliyokutwa kwenye Makaburi ambayo yalitumika pia kwa maziko ya Malkia Carlotta Federica wa Mecklemburg pamoja na Sophie Von Hohenlohe. Uchunguzi unaendelea.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Makaburi yaliyokuwa yanahisiwa kuhifadhi mwili wa Emanuela Orlandi aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha hapo tarehe 22 Juni 1983, yaani miaka thelathini na sita iliyopita, Alhamisi tarehe 11 Julai 2019 yamefunguliwa. Zoezi hili limefanywa kwa ushuhuda wa ndugu na jamaa ya Emanuela Orlandi, viongozi wa Mahakama pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama vya Vatican. Hakuna masalia ya binadamu yaliyokutwa kwenye Makaburi hayo ambayo yalitumika pia kwa maziko ya Malkia Carlotta Federica wa Mecklemburg pamoja na Sophie Von Hohenlohe. Familia ya Emanuela Orlandi imejulishwa matokeo ya uchunguzi huu. Uchunguzi wa kina unaendelea ili kubainisha wapi mahali ambapo miili ya Malkia Carlotta Federica wa Mecklemburg pamoja na Sophie Von Hohenlohe ilihamishiwa wakati wa ukarabati mkubwa wa Makaburi haya mwishoni mwa mwaka 1800 na baadaye kati ya Mwaka 1960 hadi mwaka 1970.

Dr. Alessandro Gisoti, Msemaji mkuu wa muda wa Vatican baada ya zoezi hili kukamilika amefafanua kwamba, daima Vatican imeonesha utashi mwema wa kushirikiana na familia ya Emanuela Orlandi na kwamba, iko karibu nao, lakini kwa namna ya pekee na Mama mzazi wa Emanuela anayetaka kufahamu ukweli kuhusu mahali alipo Mtoto wake, ndiyo maana Vatican ikaruhusu Makaburi hayo yafunguliwe ili kujiridhisha dhidi ya shutuma zilizokuwa zimezagaa kwenye vyombo vya habari! Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika Tahariri yake anakaza kusema, Mahakama pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama vya Vatican, vimeonesha utashi wa kutaka kushirikiana na Familia ya Emanuela Orlandi ili kupata ukweli juu ya kifo cha mtoto wao, kilichotokea kunako mwaka 1983. Kuna barua ya siri iliyotumwa kwa Familia ya Emanuela Orlandi ilitaja kwamba, kati ya makaburi yaliyokuwa mjini Vatican, moja wapo lilikuwa linahifadhi maiti ya Emanuela Orlandi.

Kazi hii imefanywa kwa utaalam mkubwa pamoja na kutumia vifaa kwa kisasa ili kuhakikisha kwamba, ukweli unapatikana na mashaka yanaondoka. Huu ni ushuhuda wa utu, heshima na Ukristo mbele ya Familia ya Orlandi inayotafuta ukweli kuhusu mtoto wao. Shutuma kwamba, pengine kuna baadhi ya watu mjini Vatican walihusika kwa namna moja au nyingine kuhamisha maiti kutoka kwenye kaburi hili hazina ukweli wowote, uchunguzi wa awali umedhihirisha kwamba, makaburi haya hayakuwa na masalia ya mwili wa Emanuela Orlandi. Watu wameanza kujiuliza maswali magumu, Je, imekuwaje makaburi haya mawili yasiwe na masalia ya miili iliyozikwa ndani mwake? Lakini, hapa ikumbukwe kwamba, kilichokuwa kinatafutwa ni mwili wa Emanuela Orlandi kadiri ya shutuma zilizotolewa! Huyu ni kijana aliyetoweka katika mazingira ya kutatanisha kunako mwaka 1983, lakini uchunguzi haukufanikiwa kupata masalia ya mwili wake!

Mahakama ya Vatican pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama vimeamua kuendelea na uchunguzi wa kina ili kubainisha mahali walipozikwa hawa Malkia wawili ambao majina yao yameandikwa kwenye makaburi haya. Kuna uwezekano mkubwa kwamba, wakati wa ujenzi wa msingi wa ukuta uliopo, masalia ya miili iliyokuwemo kaburi humo yalihamishwa na kuhifadhiwa mahali pengine. Maswali yote haya yatapewa ufumbuzi, uchunguzi wa kina utakapokamilika anasema Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika Tahariri yake. Uchunguzi wa vinasaba vya masalia ya binadamu, nyaraka mbali mbali zilizokusanywa na hatimaye, kufanikisha zoezi zima la kufukua makaburi ili kujiridhisha ikiwa kama yalikuwa yanahifadhi masalia ya Emanuela Orlandi, hata kama shutuma hizi zilitolewa na watu wasiojulikana, imeiwezesha Mahakama ya Vatican pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kutoa tamko la uhakika kwamba, hakuna masalia ya Emanuela Orlandi kwenye makaburi haya na ushuhuda huu ni wa kweli wala hauna tena mashaka!

Tahariri: Orlandi

 

 

 

 

12 July 2019, 15:05