Tafuta

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Kauli mbiu "Njia Mpya ya Kanisa na kwa ajili ya Ekolojia Fungamani: Maadhimisho: Vatican tarehe 6-27 Oktoba 2019. Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Kauli mbiu "Njia Mpya ya Kanisa na kwa ajili ya Ekolojia Fungamani: Maadhimisho: Vatican tarehe 6-27 Oktoba 2019. 

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia! Vipaumbele vya Kanisa!

Hati ya maandalizi ya Sinodi ya Amazonia ilikazia zaidi: kuona, kung'amua na kutenda! Ni Sinodi itakayopembu yafuatayo: haki jamii, malezi ya awali na endelevu, katekesi makini, liturujia na utambulisho wa Kanisa katika Ukanda wa Amazonia. Hati ya Kutendea Kazi: “Instrumentum Laboris” imepitishwa hivi karibuni na Wajumbe Washauri wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia yatafanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 6-27 Oktoba 2019 kwa kuongozwa na kauli mbiu "Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani". Hati ya maandalizi ya Sinodi ya Amazonia ilikazia umuhimu wa: kuona, kung'amua na kutenda! Ni Sinodi itakayopembua tema mbali mbali: kuhusu: haki jamii, malezi ya awali na endelevu, katekesi makini, liturujia na utambulisho wa Kanisa katika Ukanda wa Amazonia. Hati ya Kutendea Kazi: “Instrumentum Laboris” imepitishwa hivi karibuni na Wajumbe Washauri wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Katika muktadha huu, Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu, amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kumteua Kardinali Claudio Hummes, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Sao Paulo, Brazil, ambaye pia aliwahi kuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri kuwa ni Mwezeshaji mkuu wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia.

Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko amemteua pia Askofu David Martinez De Aguirre Guinea, O.P. wa Jimbo Katoliki la Puerto Maldonado nchini Perù, pamoja na Padre Michael Czerny, Katibu mkuu msaidizi, Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza ya Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu kuwa Makatibu Maalum wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Kardinali Baldisseri amebainisha hatua mbali mbali ambazo zimekwisha kufikiwa kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Kwenye Kikao cha kwanza,  wajumbe walipata nafasi ya kuchambua muswada wa hati ya maandalizi kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Huu ni muswada ulioandaliwa na Sekretarieti kuu ya Sinodi ya Maaskofu kwa msaada wa wataalam mbali mbali! Wajumbe wakatoa maoni yao ili kuuboresha zaidi. Wajumbe wakati wa majadiliano yao, wameonesha umuhimu wa Ukanda wa Amazonia katika mustakabali wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya yote!

Wajumbe walitumia fursa hii kufanya upembuzi yakinifu kuhusu hali ya shughuli za kichungaji, umuhimu na hitaji la kuanzisha mchakato wa safari mpya ya uinjilishaji inayofumbatwa katika dhana ya utamadunisho. Sehemu ya pili, imeangalia kwa namna ya pekee, changamoto na matatizo yanayotishia ekolojia katika Ukanda wa Amazonia na kuonesha umuhimu wa ekolojia fungamani kama inavyodadavuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Baba Mtakatifu aliwashukuru wataalam ambao wengi wao walikuwa wanatoka katika Mtandao wa Kanisa Amerika ya Kusini, (Pan-Amazon Ecclesial Network of the Latin American Church, REPAM). Mkutano huu ulifuatiwa na Semina iliyofanyika kuanzia tarehe 25-27 Februari 2019 kwa kuangalia umuhimu wa utekelezaji wa “Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa” mintarafu Katiba ya Kitume “Episcopais Communio” yaani “Kuhusu Sinodi za Maaskofu”.

Mambo yaliyopewa msukumo wa pekee niaAri na mwamko wa kimisionari pamoja na umuhimu wa Kanisa kusikiliza na kujibu kilio cha watu wa Mungu; vilipewa msukumo wa pekee; kwa kulinda na kudumisha kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amekabidhiwa kuilinda na kuiendeleza. Kubwa zaidi, lilikuwa ni maandalizi ya “Instrumentum Laboris” yaani “Hati ya Kutendea Kazi” ambayo imepembuliwa kwa kina na mapana na wajumbe, kama matunda ya kazi iliyotanguliwa na mchango kutoka kwa wadau mbali mbali. Lengo la hati hii ni kuwasilisha mpango mkakati wa shughuli za kichungaji zinazopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa katika Ukanda wa Amazonia mintarafu Waraka wake wa Kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”.

Wajumbe wamepongeza hati hii ya kutendea kazi pamoja na kuiboresha zaidi tayari kusambazwa kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia, ili iweze kujadiliwa na hatimaye, kufanyiwa kazi wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Ukanda wa Amazonia. Hatimaye, Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu amewashukuru wajumbe wote kwa mchango wao kama sehemu muhimu sana ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi kwa ajili ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia.

Sinodi ya Amazonia
17 July 2019, 14:24