Tafuta

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia ni tukio muhimu la maisha na utume wa Kanisa: Umuhimu wa kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu! Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia ni tukio muhimu la maisha na utume wa Kanisa: Umuhimu wa kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu! 

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Haki msingi, utu na heshima ya binadamu

Kardinali Pedro Ricardo Barretto anapembua kuhusu: Umuhimu wa Sinodi na Ukanda wa Amazonia kwa familia ya Mungu; dhamana na utume wa Kanisa. Wawekezaji kutoka nje: utu, heshima na haki msingi za wananchi wa Amazonia: changamoto ya watu waliojitenga, PIAV pamoja na jinsi ambavyo Kanisa linavyotaka kujizatiti katika utekelezaji wa changamoto hizi! Utu wa watu wa Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia yatafanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 6-27 Oktoba 2019 kwa kuongozwa na kauli mbiu: "Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani". Hati ya maandalizi ya Sinodi ya Amazonia ilikazia umuhimu wa: kuona, kung'amua na kutenda! Hii ni Sinodi itakayopembua tema mbali mbali kuhusu: haki jamii, malezi ya awali na endelevu, katekesi makini, liturujia na utambulisho wa Kanisa katika Ukanda wa Amazonia. Hati ya Kutendea Kazi: “Instrumentum Laboris” imepitishwa hivi karibuni na Wajumbe Washauri wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Hati hii imegawanyika katika Sehemu Kuu III, kwa kuwa na utangulizi pamoja na hitimisho lake. Sehemu ya kwanza inapembua kuhusu Sauti kutoka Amazonia kwa kujikita katika: Maisha, Ukanda wa Amazonia, Nyakati na Majadiliano.

Sehemu ya Pili ni kuhusu Ekolojia fungamani:Kilio cha Dunia Mama na Kilio cha maskini. Hapa wanaangaliwa watu mahalia waliojitenga, wahamiaji, ukuaji wa miji; familia na jumuiya za watu, rushwa na ufisadi; afya fungamani, elimu makini na wongofu wa kiekolojia. Sehemu ya Tatu: Kanisa Sauti ya Kinabii Ukanda wa Amazonia: Changamoto na matumaini. Sura ya Kanisa na Umisionari Ukanda wa Amazonia; changamoto za utamadunisho; maadhimisho ya fumbo la imani na liturujia iliyotamadunishwa. Muundo wa jumuiya; Uinjilishaji mijini; Majadiliano ya kidini na kiekumene pamoja na utume wa vyombo vya mawasiliano ya jamii. Utume wa kinabii wa Kanisa pamoja na mkakati wa maendeleo fungamani ya binadamu.

Kardinali Pedro Ricardo Barretto, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Huancayo nchini Perù katika makala yaliyochapishwa kwenye Jarida laCiviltà Cattolica” anasema, Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia ni muda muafaka wa kupembua kwa kina na mapana haki msingi za binadamu, watu mahalia, jumuiya pamoja na wajibu wa serikali katika mchakato wa kukuza na kudumisha majadiliano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia. Hatima ya mchakato huu ni  kuanza njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani. Kardinali Pedro Ricardo Barretto, katika tafakari yake, anapembua kuhusu: Umuhimu wa Sinodi Ukanda wa Amazonia; hali tete na umuhimu wa Ukanda wa Amazonia kwa familia ya Mungu; dhamana na utume wa Kanisa.

Wawekezaji kutoka nje: utu, heshima na haki msingi za wananchi wa Amazonia: changamoto ya watu waliojitenga, PIAV pamoja na jinsi ambavyo Kanisa linavyotaka kujizatiti katika utekelezaji wa changamoto hizi! Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia ni sehemu ya utume endelevu wa Kanisa na kamwe lisionekane kuwa ni tishio kwa uhuru wa nchi mbali mbali. Kanisa linataka kujizatiti ili kupembua changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika Ukanda wa Amazonia ili hatimaye, kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu. Jambo la msingi ni kulinda na kudumisha utambulisho wa wananchi wa Ukanda wa Amazonia, pili ni kulinda na kuendeleza ekolojia fungamani, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika Ukanda huu.

Tatu ni kuhakikisha kwamba, mazingira nyumba ya wote yanalindwa na kuendelezwa na wote na wala si kwa ajili ya mafao ya watu wachache katika jamii. Hapa kutokana na uzoefu na mang’amuzi ya muda mrefu, Kanisa linaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa ili kuibua mbinu mkakati wa maendeleo ya muda mfupi na muda mrefu. Kanisa linapenda kutumia kipindi hiki cha neema kupembua kwa kina na mapana umuhimu wa utamadunisho; kwa kuangalia changamoto mamboleo pamoja na zile zinazohitaji kuvaliwa njuga kwa haraka, ili hatimaye, kuwajengea watu matumaini, kama Hati ya Kutendea Kazi ya Sinodi inavyobainisha katika ile Sehemu ya III.

Kumekuwepo na hatua mbali mbali ambazo zimechukuliwa na Mama Kanisa kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia hadi kupitishwa kwa Hati ya Kutendea Kazi ya Sinodi, ambayo inaungwa mkono na wananchi wengi wa Ukanda wa Amazonia. Lakini, ikumbukwe kwamba, hili ni tukio la Kikanisa, lakini matunda ya maadhimisho haya yanawalenga watu wote wa Mungu, Ukanda wa Amazonia na kwamba, kilio cha Dunia Mama na Maskini wa Amazonia, lazima kisikilizwe na kupatiwa majibu muafaka! Kardinali Pedro Ricardo Barretto anasikitika kusema kwamba, kwa miaka mingi Ukanda huu umenyonyowa vya kutosha na hivyo kusababisha madhara makubwa kwa wazawa wa Ukanda huu.

Wawekezaji wengi kutoka ndani na nje ya Ukanda wa Amazonia walivutwa sana na utajiri wa madini na maliasili, bila kusahau amana na utajiri unaofumbatwa katika tamaduni za wananchi wa Ukanda wa Amazonia. Hili ni eneo linalopambwa kwa misitu mikubwa kwa ajili ya kilimo, bahari na mito mikubwa kwa ajili ya uvuvi. Kuna utajiri mkubwa wa kitamaduni ndiyo maana Kanisa linataka kukazia ekolojia ya kitamaduni, ekolojia ya maisha ya kila siku, mambo yanayohitaji umoja na mshikamano wa watu wa Mungu. Mama Kanisa katika Ukanda wa Amazonia anataka kujielekeza zaidi katika mchakato wa kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayofumbatwa katika misingi ya haki, amani, maridhiano; utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Kanisa linataka kusimama kidete kupambana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengine, kwa kukazia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kanisa linataka kujielekeza zaidi katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia, kwa kuwa ni chombo na shuhuda wa Injili ya matumaini kwa wale waliokuwa wamekata tamaa. Haki msingi za binadamu, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ustawi na maendeleo ya kiuchumi ni mambo msingi yanayopaswa kushughulikiwa kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mahitaji msingi ya binadamu. Kuendeleza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kama sehemu ya mchakato wa utamadunisho na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo.

Tunu msingi za kijamii, kiutu na kimataduni kutoka kwa wananchi wa Ukanda wa Amazonia ni utajiri na amana inayopaswa kuendelezwa na wengi. Ukanda wa Amazonia unaundwa na Serikali mbali mbali, wawekezaji kutoka ndani na nje, lakini pia hapa kuna wananchi wa Ukanda wa Amazonia ambao haki zao msingi zinapaswa kulindwa na kudumishwa katika medani mbali mbali za maisha ya kisiasa, kijamii, kitamaduni na kiuchumi. Wananchi wa Amazonia wanapaswa pia kushiriki katika mchakato wa kuamua, kupanga na kutekeleza sera na mikakati mbali mbali inayohusu maendeleo na hatima ya maisha yao. Nchi za Ukanda wa Amazonia zimeridhia kuhusu Itifaki ya 169 ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya wazawa.

Nchi za Ukanda wa Amazonia zinapaswa kushikamamna kwa dhati ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kutekeleza kwa vitendo makubaliano ya Mkutano wa 21 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, Cop21 uliofanyika mjini Paris, nchini Ufaransa mwaka 2015. Utu, heshima na haki msingi za wananchi waliojitenga kwa hiyari yao wenyewe (PIAV) zinapaswa kulindwa na kudumishwa na wote. Kumbe, kuna haja ya kuanza tena mchakato wa kuwajeresha katika maisha na jamii zao taratibu. Kardinali Pedro Ricardo Barretto, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Huancayo nchini Perù katika makala haya anasema, Mama Kanisa anataka kujizatiti zaidi ili kuhakikisha kwamba, anazivalia njuga changamoto za maisha na utume wa Kanisa Ukanda wa Amazonia, kwa kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Hapa kuna umuhimu wa kuheshimu utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kanisa linataka kuwa ni chombo na shuhuda wa imani, matumaini, mapendo na mshikamano wa dhati. Kanisa linataka kuendelea kutangaza na kushuhudia. Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

sinodi Amazonia
18 July 2019, 16:22