Tafuta

Vatican News
Kardinali Peter Turkson amewaambia Mababa wa SECAM kwamba, wanapaswa kuwa ni mfano bora wa uongozi Barani Afrika kwa kuzingatia: Uadilifu, ukweli na uwazi! Kardinali Peter Turkson amewaambia Mababa wa SECAM kwamba, wanapaswa kuwa ni mfano bora wa uongozi Barani Afrika kwa kuzingatia: Uadilifu, ukweli na uwazi! 

Jubilei ya Miaka 50 ya SECAM: Uongozi: Uadilifu, Ukweli & Uwazi

Viongozi wa Kanisa Barani Afrika wanakumbushwa kwamba, wanapaswa kujikita zaidi katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Vinginevyo, watasongwa sana na kilio cha familia ya Mungu Barani Afrika inayotamani kuona haki, amani, ustawi, maendeleo na haki msingi za binadamu zikidumishwa na wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Shirikisho la Mabaraza la Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM yaliofikia kilele chake Jumapili tarehe 28 Julai 2019 kwenye Madhabahu ya Mashahidi wa Uganda, Namgongo, Kampala, Uganda yameongozwa na kauli mbiu “Kanisa, familia ya Mungu Barani Afrika; Sherehekea Jubilei yako! Mtangaze Kristo Yesu Mkombozi wako”. Maadhimisho haya yamekwenda sanjari na mkutano mkuu wa 18 wa SECAM.  Imekuwa ni fursa kwa Mababa wa SECAM kupembua kwa kina na mapana Vipaumbele vya maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Mababa wa SECAM wamekazia kwa namna ya pekee, umuhimu wa kumwilisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, mwelekeo mpya wa utendaji wa Kanisa kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko. Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo zinapaswa kuimarishwa na kuendelezwa ili kujenga misingi ya umoja, udugu, upendo na mshikamano kati ya waamini kwani huu pia ndio mfumo na utambulisho wa Kanisa Barani Afrika, bila kusahau utume wa vijana na familia!

Ushiriki mkamilifu wa waamini katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, ili kuendelea kujenga na kuimarisha Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa, umesisitizwa zaidi. Hii iwe ni fursa ya waamini kusikiliza na kutafakari Neno la Mungu linalopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha, kielelezo cha imani tendaji. Katekesi ya awali na endelevu ni muhimu katika mchakato wa kupyaisha uelewa wa Mafundisho tanzu ya Kanisa, ili waamini waweze kuwa tayari kuyashuhudia, kuyalinda na kuyatetea pale inapobidi. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Barani Afrika ni changamoto changamani inayohitaji kuvaliwa njuga na Kanisa Barani Afrika. Familia ya Mungu Barani Afrika imetakiwa kuwa macho dhidi ya utamaduni wa kifo unafumbatwa katika sera na mikakati ya utoaji mimba, kifo laini pamoja na shinikizo la ndoa za watu wa jinsia moja; mambo ambayo kimsingi yanasigana na kanuni maadili, utu wema na mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu! Sanjari na hili, Mababa wa SECAM wanasema, haki msingi na ulinzi wa watoto wadogo ni kati ya changamoto na vipaumbele vya Kanisa Barani Afrika, kwa sasa na kwa siku za usoni.

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu katika mahubiri yake wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwa Mababa wa SECAM, Ijumaa, tarehe 26 Julai 2019 aliwataka viongozi wa Kanisa Barani Afrika kujielekeza zaidi katika uongozi shirikishi unaowajumuisha watu wa Mungu, daima wakijitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa uadilifu, ukweli na uwazi. Kama ilivyokuwa kwa Mtumishi wa Mungu Musa wakati wa safari ya kutoka utumwani Misri, aliwakirimia Waisraeli mahitaji yao msingi pamoja na kuwapatia Neno la Mungu. Viongozi wa Kanisa Barani Afrika wanakumbushwa kwamba, wanapaswa kujikita zaidi katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Vinginevyo, watasongwa sana na kilio cha familia ya Mungu Barani Afrika inayotamani kuona haki, amani, ustawi, maendeleo na haki msingi za binadamu zikidumishwa na wote.

Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa, iwe ni fursa kwa viongozi wa Kanisa kujichotea nguvu itakayowasaidia kupambana na changamoto mbali mbali zinazowakabili watu wanaowaongoza. Kama ilivyokuwa kwa Musa Mtumishi wa Mungu aliyewaokoa Waisraeli kutoka utumwani Misri, akawavusha jangwani kwa uwezo na matendo makuu ya Mungu; akawalisha manna jangwani na kuwanywesha asali kutoka mwambani, aliendelea kusali na kuwaombea huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu, pale walipokengeuka na kutopea katika dhambi kwa kumwabudu ndama wa kuchongwa. Viongozi wa Kanisa Barani Afrika kwanza kabisa watambue kwamba, wao ni watumishi wa Mungu na familia ya Mungu wanayopasa kuifundisha, kuiongoza na kuitakatifuza kwa kuendelea kusoma alama za nyakati.

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson amewakumbusha Mababa wa SECAM kwamba,  uongozi wa Kanisa ni huduma ya Neno, Upendo na Sakramenti za Kanisa, kielelezo na utambulisho wao kama watumishi wa Mungu. Kristo Yesu awe ni kielelezo na mfano bora wa kuigwa kama Mchungaji mwema aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti. Viongozi wa Kanisa wawe waaminifu na waadilifu katika utekelezaji wa shughuli na utume wao kwa watu wa Mungu Barani Afrika. Mwenyezi Mungu apewe kipaumbele cha kwanza na pili ni huduma makini kwa watu wa Mungu kwa kufanya haya yote kwa ari na moyo mkuu, Kanisa Barani Afrika litaendelea kumtangaza Kristo Yesu, kuwa ni mkombozi wa ulimwengu!

Kardinali Turkson: SECAM
29 July 2019, 11:12