Tafuta

Vatican News
SECAM: Jubilei ya Miaka 50 ya maisha na utume wake Barani Afrika: Changamoto mamboleo kwa Kanisa Barani Afrika! SECAM: Jubilei ya Miaka 50 ya maisha na utume wake Barani Afrika: Changamoto mamboleo kwa Kanisa Barani Afrika! 

SECAM: Changamoto mamboleo kwa Kanisa Barani Afrika!

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa SECAM yanapaswa kupembuliwa kwa kuangalia changamoto zilizotolewa na Mtakatifu Paulo VI wakati wa hija yake ya kitume nchini Uganda, Wosia wa Kitume wa Mtakatifu Yohane Paulo II, Kanisa Barani Afrika pamoja na Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, Dhamana ya Afrika. Changamoto endelevu?

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM tarehe 29 Julai 2018 lilizindua rasmi mchakato wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu lilipoanzishwa, wakati wa hija ya kitume ya Mtakatifu Paulo VI, mwaka 1969 huko Kampala nchini Uganda. Kauli mbiu ya Maadhimisho haya ni “Kanisa, familia ya Mungu Barani Afrika; Sherehekea Jubilei yako! Mtangaze Kristo Yesu Mkombozi wako”. Mababa wa SECAM tangu tarehe 23 Julai wanaendelea na mkutano wao mkuu wa 18 na kilele cha maadhimisho haya ni hapo tarehe 28 Julai 2019 kwenye Madhabahu ya Mashahidi wa Uganda, Namgongo, Kampala, Uganda. Baada ya ufunguzi rasmi wa maadhimisho haya kwa Ibada ya Misa Takatifu pamoja na makaribisho kutoka kwa Rais Yower Kaguta Museveni wa Uganda, Mababa wa SECAM wanaendelea na mkutano wao ili kupembua kwa kina na mapana mafanikio ya SECAM katika kipindi cha Miaka 50 ya maisha na utume wake, changamoto mambaoleo, fursa na matumaini ya SECAM kwa miaka iyajo kwa Kanisa la Mungu Barani Afrika.

Kardinali Robert Sarah, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa kama sehemu ya mchango wake kwa wajumbe wa SECAM amesema, SECAM inapaswa kupembua changamoto za maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika kwa kupitia kwa umakini mkubwa Nyaraka kuu tatu kuhusu Kanisa Barani Afrika. Kwanza kabisa ni hija ya kitume ya Mtakatifu Paulo VI iliyotoa changamoto ya ari na mwamko wa kimisionari; umuhimu wa Kanisa katika kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika kwa kukazia amani kwani amani ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu bila kusahau umoja na mshikamano wa Maaskofu Barani Afrika. Wosia wa Kitume wa Mtakatifu Yohane Paulo II, “Ecclesia in Africa”, yaani “Kanisa Barani Afrika” ni Wosia unaopembua kwa kina na mapana kuhusu historia ya neema ya uinjilishaji Barani Afrika, Kanisa Barani Afrika; Umuhimu wa uinjilishaji na utamadunisho; Katika mwanga wa Kristo kuelekea Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, changamoto mamboleo.

Mtakatifu Yohane Paulo II anaitaka familia ya Mungu Barani Afrika kuwa ni shuhuda wa Kristo Mfufuka, tayari kujizatiti katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, amani, umoja, upendo na mshikamano wa dhati. Kanisa Barani Afrika linaendelea kuhamasishwa kuwa ni shuhuda wa Kristo Mfufuka hadi miisho ya dunia kwa kujikita zaidi katika ari na mwamko wa kimisionari, kwa kuendelea kushikamana katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, lakini zaidi kwa kukuza na kudumisha utakatifu unaomwilishwa katika huduma mbali mbali zinazotolewa na Mama Kanisa! Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI “Africae munus” yaani “Dhamana ya Afrika” unaihamasisha familia ya Mungu Barani Afrika kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu, kwa kujikita katika huduma ya upatanisho, haki na amani. Dhana hii inamwilishwa kwa namna ya pekee kwa kujali utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Kanisa Barani Afrika linapaswa kuendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika maisha na ushiriki mkamilifu wa waamini katika maisha ya Sakramenti za Kanisa hasa Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi Takatifu pamoja na kuendeleza utume kwa marika mbali mbali ndani ya Kanisa. Umoja na mshikamano wa viongozi wa Kanisa ni jambo lililopewa msukumo wa pekee na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Hapa, Kanisa Barani Afrika linapaswa kuonesha uwepo wake katika huduma ya: afya, elimu, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu. Kanisa Barani Afrika linapaswa kuwa ni shuhuda wa Injili ya matumaini kwa wale waliokata tamaa, ili kuwatia shime kusimama tena na kutembea kifua mbele! Kardinali Robert Sarah anakazia umuhimu wa kudumisha kanuni maadili na utu wema bila kukubali kumezwa na malimwengu pamoja na athari za utandawazi. Jambo la msingi analokazia Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu ni uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kutoka kwa watu wa Mungu.

Tunu msingi za Kiinjili hazina budi kufundishwa na hatimaye kutolewa ushuhuda na watu wa Mungu Barani Afrika. Umoja, upendo na mshikamano unaooongozwa na kauni auni ni muhimu sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika. Huu ni wakati anasema Kardinali Robert Sarah wa kumwilisha tunu msingi za kiinjili kama ushuhuda wa imani tendaji! Mababa wa SECAM wanawataka viongozi wa Kanisa kuwa ni mfano bora wa kuigwa kwani uongozi ndani ya Kanisa ni huduma inayomwilishwa katika upendo na unyenyekevu. Familia ya Mungu Barani Afrika haina budi kujizatiti katika kupambana na changamoto za utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengine ndani ya jamii, ili kudumisha umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii.

Athari za mabadiliko ya tabianchi zinazotokana na uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote zinahitaji toba na wongofu wa kiekolojia kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika mafundisho yake. Athari za mabadiliko ya tabianchi zinagusa na kutikisa utu, heshima na haki msingi za binadamu; zinagusa hata masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Familia ya Mungu Barani Afrika inapaswa kutambua athari hizi na kuzivalia njuga kwa ujasiri mkubwa! Familia ya Mungu Barani Afrika inaendelea kupambana na hali ngumu ya uchumi, umaskini wa hali na kipato, elimu duni kwa baadhi ya nchi pamoja na watu wengi kushindwa kumudu gharama za huduma ya afya, hali ambayo inarudisha nyuma maendeleo yaliyokuwa yamekwisha kufikiwa katika sekta ya afya. Matokeo yake hapa ni kuibuka kwa kasi kubwa imani za kishirikiana na ukanimungu pamoja na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia!

Kanisa liendelee kuwajengea watu dhamiri nyofu ili kupembua mema na mabaya, daima likitoa kipaumbele cha pekee kwa uwepo wa Mungu kati yao. Ulaji wa kupindukia na madhara yake katika afya za watu wa Afrika, athari za maambukizi ya Ugonjwa wa Ukimwi; Utumwa mamboleo, biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; matumizi haramu ya dawa za kulevya, vita, ghasia na mipasuko ya kidinia, kijamii na kisiasa ni kati ya changamoto ambazo zinapaswa kuvaliwa njuga na familia ya Mungu Barani Afrika. Kumekuwepo na mmong’onyoko mkubwa wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia Barani Afrika na matokeo yake, ni kuendelea kuibuka kwa familia  na malezi tenge ya watoto. Kuna watu ambao wamekata na kukatishwa tamaa kutokana na sababu mbali mbali na matokeo yake, utamaduni wa kifo, kwa watu kutema zawadi ya maisha unaendelea kushika kasi sehemu mbali mbali za Bara la Afrika! Utawala bora unaozingatia katiba ya nchi, sheria na kanuni bado ni changamoto kubwa kwa nchi nyingi Barani Afrika.

Vitendo vya kigaidi vinaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao pamoja na kuharibu misingi ya umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii. Uhusiano kati ya Serikali na Kanisa ni jambo linalopaswa kuangaliwa kwa umakini zaidi, ili Kanisa liendelee kuwa ni sauti ya watu wasiokuwa na sauti Barani Afrika. Kanisa lisaidie kukuza na kudumisha demokrasia shirikishi kwa kuendeleza Mafundisho Jamii ya Kanisa miongoni mwa watu wa Mungu! Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM linasema, linapania kuwajengea vijana uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kama anavyofafanua Baba Mtkatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi”, ambao umeandikwa katika mfumo wa barua kwa vijana. Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya!

SECAM inataka kuwajengea vijana uwezo ili wawe kweli ni mfano bora wa kuigwa katika masuala ya uongozi. Kanisa Barani Afrika kama ilivyokuwa wakati wa wamisionari waliowekeza katika elimu makini kiasi cha kuwafunda wapigania uhuru, hata leo hii, Kanisa lina dhamana na wajibu wa kuwafunda vijana ili waweze kuwa ni viongozi bora zaidi, watakaoweza kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vijana wanakumbushwa kwamba, wao ni leo ya Kanisa na Mungu katika ujumla wake! Kanisa Barani Afrika halina budi kujenga na kudumisha utamaduni wa kuwasikiliza vijana kwa makini. Vijana wanaunda sehemu kubwa ya familia ya Mungu Barani Afrika. Kumbe, umefika wakati kwa SECAM kuunda Jukwaa la Vijana wa Bara la Afrika, ili kusimamia na kuratibu shughuli za vijana wa kizazi kipya kutoka Barani Afrika. Kwa njia hii, vijana wataendelea kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa na jamii katika ujumla wake. Vijana wanahimizwa kuhakikisha kwamba, wanakuwa na matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii pamoja na vyombo vya mawasiliano ya jamii.

SECAM: Changamoto

 

25 July 2019, 13:56