Tafuta

Altare ni alama ya Kristo Yesu kati ya kusanyiko la waamini wake. Ni kafara inayotolewa kwa ajili ya upatanisho kati ya Mungu na binadamu! Kuna umoja kati ya Sadaka na Altare! Altare ni alama ya Kristo Yesu kati ya kusanyiko la waamini wake. Ni kafara inayotolewa kwa ajili ya upatanisho kati ya Mungu na binadamu! Kuna umoja kati ya Sadaka na Altare! 

Umuhimu wa Altare: Liturujia, Maisha & Utume wa Kanisa!

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Altare iliyo hai ni Kristo Yesu mwenyewe, hivyo, wanapoiangalia Altare wamwone Kristo aliyejitoa sadaka Msalabani kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika dhambi na mauti. Vivyo hivyo kama mwamini ni kiungo cha Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, anapaswa kutambua kuwa yeye ni sehemu ya Altare.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni ishara thabiti na sababu ya hali ya juu kabisa ya ushirika katika uzima wa kimungu na umoja wa Taifa la Mungu ambalo hulifanya Kanisa liwepo. Ekaristi Takatifu ni kilele cha tendo la Mungu la kuutakatifuza ulimwengu katika Kristo na kilele cha tendo la waamini kuliabudu Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kanisa ni mahali patakatifu panapowawezesha waamini kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, Kuabudu, Kusali na Kutafakari Matendo makuu ya Mungu katika maisha yao. Waamini wanapaswa kutambua kwamba, Liturujia ni chemchemi ya kwanza na ya lazima ambayo toka kwake waamini wanaweza kuchota roho ya kweli ya Kikristo. Liturujia kila siku inawajenga waamini ili wawe Hekalu takatifu na makao ya Mwenyezi Mungu katika roho hadi kuufikia utimilifu wa Kristo.

Liturujia inaimarisha nguvu za waamini kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu. Tendo la wokovu linaloendelezwa na Kanisa hutimizwa katika Liturujia kwa sababu Liturujia ni kilele na chemchemi ya maisha ya Kanisa. Altare inaonesha: sadaka na meza ya Bwana. Altare ni alama ya Kristo mwenyewe aliye kati ya kusanyiko la waamini wake, papo hapo akiwa kafara iliyotolewa kwa ajili ya upatanisho kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu. Altare ni sura ya mwili wa Kristo Yesu anasema Mtakatifu Ambrosi na kwamba, mwili wa Kristo uko juu ya Altare. Kumbe, Kanisa linafundisha kuhusu umoja kamili kati ya Sadaka na Altare. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walileta mageuzi makubwa katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa kuonesha umuhimu wa kuzunguka  Altare katika maadhimisho ya mafumbo ya Kanisa.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanawakumbusha waamini kwamba, Altare iliyo hai ni Kristo Yesu mwenyewe, hivyo, wanapoiangalia Altare wamwone Kristo aliyejitoa sadaka Msalabani kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Vivyo hivyo kama mwamini ni kiungo cha Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, anapaswa kutambua kuwa yeye ni sehemu ya Altare. Ndiyo maana kila mmoja anapaswa kuwa sadaka, kwa Mungu na kwa jirani yake. Aidha, chochote kinachotabarukiwa kinapaswa kutumika kwa ajili ya Mungu tu, kama vile kila mbatizwa anavyopaswa kuwa ni kwa ajili ya Mungu, kinyume chake ni kujiteketeza. Altare ina maana sana katika maisha ya mwamini. Altare ni kielelezo makini cha Kristo katika hali yake yote. Ni Kristo Yesu: anayeganga na kuponya, anayesamehe na kutakasa; Kristo anayefundisha, kuonya na kuongoza.

Huyu ni Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Altare ni meza ya karamu, hivyo waamini wanapokuwa na furaha, wakusanyike Altareni. Vivyo hivyo Altare ni Msalaba ambapo Kristo alijitoa sadaka, hivyo wanapokuwa na huzuni na mahangaiko mbalimbali, waizunguke Altare. Kwa kuwa Altare ni Kristo mzima, wamfuate wakiwa katika hali yoyote wanayoweza kuwa nayo, Yeye yupo siku zote katikati yao anawangoja, katika magumu, furaha, imani na matumaini! Ni katika muktadha huu, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, hivi karibuni aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu huko Chioggia, Venezia, nchini Italia na kutabaruku Altare ya Kikanisa cha Hospitali ya Serikali ya “Santa Maria della Navicella”. Ibada hii imehudhuriwa pia na Askofu Adriano Tessarollo wa Jimbo Katoliki la Chioggia, wagonjwa pamoja na wafanyakazi kutoka hospitalini hapo. Katika mahubiri yake, Kardinali Pietro Parolin amekazia umuhimu wa kumpenda Mwenyezi Mungu  kwa kushika na kuambata imani.

Upendo huu unajionesha kwa kumkiri Kristo Yesu na kushikamana naye katika maisha ili kuufikia utimilifu wa upendo halisi ambao ni Mungu mwenyewe aliyejifunua kwa njia ya Kristo Yesu, kama chemchemi ya huruma na upendo. Kristo Yesu ni mfano halisi wa Msamaria mwema ambaye ni kielelezo cha upendo unaojipambanua katika kiini chake cha kweli, huduma na wokovu. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, daima amekuwa akiwasindikiza, akiwahudumia na kuwafariji katika shida na mahangaiko yao: kiroho na kimwili. Kardinali Parolin anakaza kusema, kimsingi, Mama Kanisa anaitwa na kutumwa kutangaza Ufalme wa Mungu na kupoza wagonjwa kwa sababu amepewa nguvu zote za kuponya magonjwa na kupunga pepo. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alionesha ukaribu kwa wagonjwa.

Wagonjwa watumie fursa hii kumruhusu Yesu ili aweze kuyatumia magonjwa yao kama chemchemi ya neema inayowasogeza zaidi kwake katika wongofu wa ndani. Kwa kupitia udhaifu wao, awasaidie kukua na kukomaa katika hekima, busara na ufahamu wa kiroho na kwa kuungana na Kristo Yesu, mateso yao yatazaa matunda mema ya kiroho kwa faida ya Kanisa na Ulimwengu wote. Mtakatifu Yohane Paulo II anawataka wahudumu katika sekta ya afya kuiga mfano wa Kristo Msamaria mwema kwa kuwahudumia kikamilifu ndugu zao wanaoteseka. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huruma na upendo wa Mungu wanapotekeleza dhamana na wajibu wao kwa huruma, weledi, ustadi na uaminifu mkubwa. Wawapende na kuwaheshimu wagonjwa; wasimame kidete kulinda, kutunza na kutetea utu, heshima na haki zao msingi!

Kardinali Parolin anaendelea kufafanua kwamba, Fumbo la Pasaka yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ndicho kiini cha Liturujia ya Kanisa! Ndiyo maana Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema,  uchungu na fadhaa ya mwanadamu wa nyakati hizi na hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteseka, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu inayomwambata mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa ni chemchemi ya neema na baraka, si tu kwa kuponya, bali kwa kumpatia mwamini mwelekeo mpana zaidi unaopata utimilifu wake kwa Kristo Yesu aliyekuja humu duniani, ili binadamu aweze kupata maisha na uzima wa milele. Waamini wanahamasishwa na Baba Mtakatifu Francisko kuendelea kuwa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kwa njia ya huduma ya upendo kwa Mungu na jirani, kielelezo cha imani tendaji.

Huruma ni fadhila kubwa kushinda zote na nyingine zote huitegemea kama mhimili na kukamilisha yale mapungufu yaliyoko kwenye fadhila nyingine zote. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, asili ya Mungu ni huruma na kwa njia yake uwezo wake usiokuwa na mipaka unadhihirishwa kwa kiwango cha juu kabisa! Huduma kwa wagonjwa na maskini anasema Kardinali Pietro Parolin ni sehemu ya mbinu mkakati ya uinjilishaji wa kina, utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza. Kumbe, Kanisa linataka kupandikiza mbegu ya tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu katika sekta ya afya; kwa kukazia umoja, upendo na mshikamano wa kidugu; kwani huduma za kiroho na kimwili zinakwenda pamoja na kukamilishana kama inavyojionesha katika mfano wa Msamaria mwema!

Kutabaruku Altare
24 July 2019, 10:39