Papa Francisko amefanya mabadiliko makubwa kuanzia sasa shughuli zote za Kwaya ya Kikanisa cha Sistina itakuwa chini ya Idara ya Liturujia ya Baba Mtakatifu. Papa Francisko amefanya mabadiliko makubwa kuanzia sasa shughuli zote za Kwaya ya Kikanisa cha Sistina itakuwa chini ya Idara ya Liturujia ya Baba Mtakatifu. 

Ofisi ya Liturujia ya Papa kuratibu shughuli za Kwaya ya Sistina

Monsinyo Massimo Palombella hivi karibuni, amehitimisha utume wake kama Mwalimu na Mkurugenzi wa Kwaya ya Kikanisa cha Sistina. Monsinyo Palombella amewasilisha ombi lake la kung’atuka kutoka katika huduma hii kwa Papa Francisko, ambaye ameridhia, baada ya majadiliano ya kina kati ya Shirika la Wasalesiani wa Mtakatifu Bosco pamoja na Ofisi ya Liturujia ya Papa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Muziki mtakatifu ni chombo cha ibada na uinjilishaji; ni amana na utajiri wa Kanisa; dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa ibada, unyenyekevu na unyofu wa moyo!Hii inatokana na ukweli kwamba, nyimbo na muziki mtakatifu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa zinawasaidia waamini kuzamisha Neno la Mungu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Kimsingi anasema Baba Mtakatifu Francisko, muziki ni chombo cha imani, amana na utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa! Baba Mtakatifu katika Barua yake binafsi Motu proprio ijulikanao kama “Cappella Musicale Pontificia” yaani “Kwaya ya Muziki Mtakatifru wa Kipapa”, iliyochapishwa rasmi tarehe 19 Januari 2019  amefanya mabadiliko makubwa na kuanzia sasa Kwaya ya Kikanisa cha Sistina imeingizwa kwenye Ofisi ya Liturujia ya Baba Mtakatifu. 

Monsinyo Guido Marini, Mshereheshaji Mkuu wa Ibada za Kipapa kuwa Mkurugenzi wake mkuu na akapewa dhamana ya kuhakikisha kwamba, anasimamia na kuratibu shughuli zote za Kiliturujia, Kichungaji, Maisha ya Kiroho, Kisanii na Malezi awali na endelevu ya wanakwaya. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakaza kusema lengo kuu la Muziki Mtakatifu ni utukufu wa Mwenyezi Mungu na kutakatifuzwa kwa waamini. Ni katika muktadha huu, Monsinyo Massimo Palombella, S.D.B, hivi karibuni, amehitimisha utume wake kama Mwalimu na Mkurugenzi wa Kwaya ya Kikanisa cha Sistina. Monsinyo Palombella amewasilisha ombi lake la kung’atuka kutoka katika huduma hii kwa Baba Mtakatifu Francisko naye ameridhia. Uamuzi huu umefikiwa baada ya majadiliano ya kina kati ya Shirika la Wasalesiani wa Mtakatifu Bosco pamoja na Ofisi ya Liturujia ya Baba Mtakatifu. Kwa sasa Monsinyo Massimo Palombella, yuko tayari kupangiwa utume mwingine kadiri ya mahitaji ya Shirika lake!

Muziki Mtakatifu

 

10 July 2019, 15:05