Tafuta

Vatican News
Mkutano wa Baba Mtakatifu Francisko na Viongozi wakuu wa Sinodi ya Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine umekuwa na mafanikio makubwa kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Mkutano wa Baba Mtakatifu Francisko na Viongozi wakuu wa Sinodi ya Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine umekuwa na mafanikio makubwa kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Viongozi wa Kanisa la Ukraine: Mafanikio makubwa

Papa amewapongeza kwa historia ya maisha na utume wa Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine; amana na utaji wake wa maisha ya kiroho; maadhimisho ya Liturujia Takatifu, bila kusahau utajiri unaobubujika kutoka katika Taalimungu, Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa. Amewapongeza watu wa Mungu nchini Ukraine kwa udumifu na uaminifu wao kwa Kristo, Kanisa na kwa Papa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, viongozi waandamizi kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican wanaohusika na eneo la Ukraine, Askofu mkuu, wajumbe wa kudumu wa Sinodi pamoja na Maaskofu wakuu wa Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine, kuanzia tarehe 5-6 Julai 2019 wamekutana mjini Vatican. Mkutano huu umekuwa ni alama ya uwepo na mshikamano wa karibu kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa familia ya Mungu ndani na nje ya Ukraine. Imekuwa ni  nafasi ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu: hali ya maisha na mahitaji halisi ya Ukraine kwa wakati huu, kama sehemu ya mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Hii inatokana na ukweli kwamba, Kanisa linataka kuchangia kwa hali na mali, ili kuwasaidia wale wote wanaoteseka kutokana na vita, kwa kushirikiana na Makanisa pamoja na Jumuiya mbali mbali za Kikristo, kielelezo cha uekumene wa huduma ya Injili na mshikamano wa upendo kwa maskini! Baba Mtakatifu katika hotuba yake elekezi kwa viongozi wa Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine amekazia umuhimu wa sala na maisha ya kiroho kama chemchemi ya faraja kutoka kwa Mungu. Amelitaka Kanisa liendelee kuwa ni shuhuda wa matumaini ya Kikristo kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo. Kwa namna ya pekee kabisa, Kanisa lioneshe ukaribu kwa watu wa Mungu wanaoteseka na kwamba, kuna haja ya kuendelea kukazia dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa!

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, Ukraine katika kipindi cha miaka mitano iliyopita imejikuta ikitumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe; vita ambayo imepelekea wananchi wa kawaida kulipa gharama kubwa. Hii ni kampeni inayochochea vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kisiasa na hata kidini. Lakini katika yote haya, watambue kwamba, daima ameendelea kuwabeba na kuwahifadhi katika sakafu ya moyo wake kwa njia ya sala na sadaka yake ya kila siku. Taarifa iliyotolewa na Vatican inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee kabisa ameonesha uwepo wake wa karibu kwa familia ya Mungu nchini Ukraine inayoendelea kuteseka na kunyanyasika kutokana na vita na hali ngumu ya maisha.

Baba Mtakatifu amewapongeza kwa historia ya maisha na utume wa Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine; amana na utaji wake wa maisha ya kiroho; maadhimisho ya Liturujia Takatifu, bila kusahau utajiri unaobubujika kutoka katika Taalimungu, Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa. Baba Mtakatifu amewapongeza watu wa Mungu nchini Ukraine kwa udumifu na uaminifu wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake pamoja na kuendelea kuonesha umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Uaminifu huu umeshuhudiwa na kufungwa kwa damu ya mashuhuda na wafiadini kutoka Ukraine. Mkutano huu umeadhimishwa katika hali ya amani na utulivu, kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama  ndugu katika Kristo Yesuò.

Wajumbe wamesikilizana na kujadiliana katika ukweli na uwazi na hatimaye, wakabainisha mambo msingi yanayopaswa kuvaliwa njuga kama kikolezo cha ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Ukraine. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kuchanua na kustawi kama “Mwerezi wa Lebanon” nchini Ukraine na katika ulimwengu katika ujumla wake. Sehemu kubwa ya majadiliano yao imejikita kwa namna ya pekee katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji; uinjilishaji, majadiliano ya kiekumene; wito na utume maalum wa Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine. Wameangalia utume huu mintarafu hali ya kisiasa na kijamii, kwa kuangalia madhara ya vita na hali ngumu inayoendelea kuwasibu wananchi wa Ukraine bila kusahau huduma inayotolewa na Kanisa kwa waamini wake waliotawanyika sehemu mbali mbali za dunia.

Ni matumaini ya wajumbe wote waliohudhuria mkutano huu kwamba, mtindo na mfumo wa majadiliano haya utaweza kuendelezwa na kudumishwa kwa siku za usoni, ili kusaidia mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini Ukraine, kama ilivyo hata kwa Makanisa mengine ya Kikristo huko Mashariki ya Kati, mintarafu utambulisho na wito wake.

Papa: Ukraine
10 July 2019, 15:34