Tafuta

Vatican News
Mtakatifu Paulo VI anasema, maendeleleo ya kweli ya binadamu yanafumbatwa katika: Udugu wa kibinadamu, haki, amani, utu na heshima ya binadamu! Mtakatifu Paulo VI anasema, maendeleleo ya kweli ya binadamu yanafumbatwa katika: Udugu wa kibinadamu, haki, amani, utu na heshima ya binadamu! 

Mtakatifu Paulo VI: Maendeleo ya kweli: Udugu & Amani duniani

Mtakatifu Paulo VI katika tafakari yake alionesha uhusiano wa karibu kati ya sayansi na maendeleo ya teknolojia. Huu ni mradi mkubwa ambao umeunganisha akili za watu, rasilimali fedha na vitu; watu wakachakarika kufanya majaribio mbali mbali na matokeo yake yamedhihirisha kwamba, hekima, ujuzi na maarifa vikitumika vyema, mwanadamu anaweza kupata maendeleo ya kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ilikuwa ni tarehe 21 Julai 1969 Neil Armstrong, mwana anga kutoka Marekani alipokanyaga kwa mara ya kwanza mwezini, akawa ni binadamu wa kwanza kutia guu lake mwezini! Mtakatifu Paulo VI katika Sala ya Malaika wa Bwana tarehe 13 Julai 1969 alisema kwamba, alikuwa anafuatilia tukio hili ambalo kimsingi lilikuwa ni ushahidi mkubwa wa maendeleo ya teknolojia katika maisha ya mwanadamu. Neil Armstrong akiwa amepanda Apollo 11 aliondoka ardhini tarehe 16 Julai 1969 na baada ya siku tano, mwanaume akatia mguu mwezini, yaani tarehe 21 Julai 1968. Hii ilikuwa ni hatua kubwa katika maendeleo ya mwanadamu. Mtakatifu Paulo VI katika tafakari yake alionesha uhusiano wa karibu kati ya sayansi na maendeleo ya teknolojia. Huu ni mradi mkubwa ambao umeunganisha akili za watu, rasilimali fedha na vitu; watu wakachakarika kufanya majaribio mbali mbali na matokeo yake yamedhihirisha kwamba, hekima, ujuzi na maarifa vikitumika vyema, mambo makubwa yanaweza kutendeka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya binadamu wote.

Maendeleo haya yanaonesha kwamba, binadamu anao uwezo wa kuendelea kuitawala dunia na kuifanya kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Mtakatifu Paulo VI anaungana na Mzaburi kuimba ile Zaburi isemayo: “Wewe, Mungu, Bwana wetu, jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote! Wewe umeuweka utukufu wako mbinguni. Vinywani mwa watoto wachanga na wanyonyao  umeiweka misingi ya nguvu; kwa sababu yao wanaoshindana nawe; … Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako, mwezi na nyota ulizoziratibisha; mtu ni kitu gani hata umkumbuke, na binadamu hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; umemvika taji ya utukufu na heshima; umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; umevitia vitu vyote chini ya miguu yake”. Zaburi ya 8: 4-8; Rejea Waraka kwa Waebrania 2: 6-8). Mtakatifu Paulo VI, alitumia fursa hii kumtafakari mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, ambaye sasa anakuwa ni kiini cha maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia.

Hiki ni kielelezo cha heshima kubwa kwa utu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kanisa likawakumbuka mashuhuda wa maendeleo ya mwanadamu. Tarehe 20 Julai 1969 Mtakatifu Paulo VI akarejea tena na tafakari ya kina kuhusu binadamu; Ujasiri na Maendeleo yake yaliyomwezesha hata kufikia malengo makubwa ambayo kimsingi yalionekana kuwa ni jambo ambalo haliwezekani na kwa miaka mingi, mwanadamu “kukanyaga guu lake” mwezini ilikuwa ni ndoto ya mchana! Mtakatifu Paulo VI kwa hekima, busara na maono yake ya kinabii, alisikika akisema kwamba, ikiwa kama mwanadamu ataghafilika na kukengeuka, kiasi cha kuona kwamba, maendeleo ya sayansi na teknolojia ndiye mungu wake, atakuwa anajichimbia shimo kubwa la maafa kwa siku za mbeleni. Je, maendeleo haya makubwa ya sayansi na teknolojia, yanachangia katika mchakato wa maboresho ya mtu: kiroho na kimwili, kwa kumwezesha kuwa ni mtu mwema zaidi? Je, teknolojia hii, imemjengea mwanadamu kiburi na majivuno kiasi cha kudhani kwamba, yeye ndiye mmiliki na hatima ya maisha yake?

Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, maendeleo ya sayansi na teknolojia yana mwezesha mwanadamu kuwa huru bila ya kumezwa na malimwengu; yamsaidie kuona kwamba, anaendelea kushiriki katika kazi ya uumbaji na wala si chombo cha uharibifu wa kazi ya uumbaji ambayo amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu ili kuilinda na kuitunza. Maendeleo makubwa ya sayansi yawe ni chachu ya kukuza na kudumisha utu, heshima, haki msingi za binadamu pamoja na kumwezesha mwanadamu kuwa mwenye Ibada na uchaji wa Mungu, kwani Mungu ni asili ya wema, uzuri na utakatifu wote wa maisha! Mtakatifu Paulo VI alisikitika kusema kwamba, maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yalikuwa yanahatarisha: maisha ya mwanadamu, mazingira, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii inatokana na ukweli kwamba, kwa maendeleo haya, mwanadamu ameendelea kuwa mstari wa mbele kuzalisha silaha za maangamizi ambazo zitasababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Kumbe, pamoja na mafanikio makubwa ambayo mwanadamu ameyapata kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Lakini, busara isipotumika, maisha ya mwanadamu yako hatarini. Lakini ikumbukwe kwamba, bado mwanadamu anapekenywa na: vita, magonjwa, umaskini, njaa na ujinga; changomoto zinazopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa. Maendeleo ya kweli yanasimikwa katika udugu wa kibanadamu, haki na amani, kwani amani ni jina jipya la maendeleo ya kweli! Maendeleo fungamani yanakita mizizi yake katika ustawi na mafao ya wengi: kiroho na kimwili; kiutu na kimaadili.

Mtakatifu Paulo VI

 

16 July 2019, 09:21