Tafuta

Vatican News
Mpango Mkakati  wa Mwezi Oktoba 2019 unapania kuhamasisha ari na mwamko wa kimisionari katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuwashirikisha zaidi waamini walei! Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 unapania kuhamasisha ari na mwamko wa kimisionari katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuwashirikisha zaidi waamini walei!  (Vatican Media)

Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019: Mambo makuu ya kuzingatia!

Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 unaongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa: Kanisa la Kristo katika utume”. Kanisa linataka kuendeleza utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, agizo kutoka kwa Kristo Yesu mwenyewe kwa wafuasi wake. Maadhimisho haya ni muda wa: sala, katekesi, tafakari na matendo ya huruma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwezi Oktoba 2019, umetengwa maalum na Mama Kanisa kwa ajili ya kuhamasisha ari na mwamko wa kimisionari duniani, kwa mwaka huu 2019, Kanisa linapoadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume"Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari.” Papa Benedikto XV katika Waraka huu, alifungua rasmi ukurasa mpya wa maisha na utume wa Kanisa mintarafu shughuli za kimisionari, kwa kulitaka Kanisa kuanzisha mchakato wa majiundo na malezi kwa ajili ya kuyategemeza Makanisa mahalia kwa rasilimali watu, yaani mihimili ya uinjilishaji! Huu ni ufafanuzi uliotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Giampietro Dal Toso,  Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Rais wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, wakati wa ufunguzi wa Kitivo cha Taalimungu cha Burgos, mjini Madrid, Hispania kama sehemu ya maadhimisho ya Juma la 72 la Kimisionari nchini Hispania na kukaza kwamba, wito na utume wa Mkristo mbatizwa hauna mbadala, yaani kwa kuwaachia watu wengine wachakarike kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa niaba ya Wakristo wenzao!

Anakaza kusema kwamba, hilo halipo, kila Mkristo anawajibika barabara kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa watu wa Mataifa, wito ambao unabubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo inayokita mizizi yake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kumbe, kwa njia ya neema ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wanageuzwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa maisha na utume wa Kanisa, na hivyo wanatumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo! Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 unaongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa: Kanisa la Kristo katika utume”.  Kanisa linataka kuendeleza wito na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, agizo kutoka kwa Kristo Yesu mwenyewe kwa wafuasi wake. Maadhimisho haya ni muda wa: sala, katekesi, tafakari na matendo ya huruma! Ni wakati muafaka kwa waamini walei kutambua haki, dhamana na wajibu wao katika maisha na utume kwa Kanisa tayari kutoka kifua mbele ili kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Askofu mkuu Giampietro Dal Toso, anaendelea kufafanua kwamba, maadhimisho ya Mbinu Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 yatafunguliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko, kwa njia ya mkesha utakaoadhimishwa tarehe 1 Oktoba 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Tarehe 7 Oktoba 2019 kutakuwa na Rozari ya Kimisionari Kimataifa, itakayotangazwa moja kwa moja kutoka kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Roma na kilele cha maadhimisho haya ni tarehe 20 Oktoba 2019, kwa Ibada ya Misa Takatifu inayotarajiwa kuongozwa na Baba Mtakatifu Francisko. Ni katika muktadha huu, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu linawahamasisha waamini kutoka katika Majimbo mbali mbali kufanya hija katika ngazi za kiparokia, kijimbo na kitaifa ili kukuza na kuimarisha ari na mwamko wa kimisionari kati ya watu wa Mungu. Iwe ni fursa ya kusali, kutafakari na kusikiliza shuhuda za kimisionari kutoka katika mihimili ya uinjilishaji sehemu mbali mbali za dunia.

Hii ni fursa ya kuwahimiza waamini kujiwekea sera na mikakati ya kuyategemeza Makanisa mahalia: kwa njia ya rasilimali watu, vitu na fedha, ili Kanisa liendelee kutangaza Injili ya huruma na upendo hadi miisho ya dunia! Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kujikita zaidi katika utekelezaji wa mambo makuu manne: Mosi, waamini wajitahidi kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Tafakari ya Neno la Mungu na Maisha ya Sala. Pili ni ushuhuda wa wamisionari watakatifu, wafiadini na waungama imani, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Tatu ni majiundo makini, endelevu na fungamani ya kimisionari kwa kujikita katika: Biblia, Katekesi, Tasaufi na Taalimungu. Nne ni huduma ya upendo kama kielelezo cha Injili ya upendo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, kama kielelezo makini cha imani tendaji!

Askofu mkuu Giampietro Dal Toso anaendelea kufafanua kwamba, tayari nchi kadhaa zimekwisha kutangaza sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kama sehemu ya maadhimisho ya Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019. Baadhi ya nchi hizi ni pamoja na: Malawi, Kenya, Ureno, Poland, Australia, Haiti, Ufilippini na Hispania. Waamini wasaidiwe kufahamu taalimungu ya kimisionari, umuhimu wa waamini kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na kutambua kwamba, Kanisa, kimsingi ni Sakramenti ya Wokovu. Iwe ni fursa ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene. Waamini wasaidiwe kufahamu Mafundisho Tanzu ya Kanisa, tayari kuyatetea na kuyashuhudia katika uhalisia wa maisha yao, daima wakifahamu kwamba, wao ni vyombo na wajenzi wa Ufalme wa Mungu. Waamini wakitambua kwamba, utume wa Kanisa unapata chimbuko lake kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na mhusika mkuu ni Roho Mtakatifu. Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu na msingi thabiti wa imani ya Kanisa kwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai!

Ni katika mazingira haya, Mama Kanisa anaendelea kuhimiza mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, ili kuamsha uzuri na utakatifu wa Injili ya Kristo kwa watu wanaosinzia kiimani na kimaadili. Kuna ongezeko kubwa la wakanimungu na watu wanaotopea katika imani. Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa ni vyombo vya huduma ya kimisionari kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Huduma hii inatekelezwa kwa njia ya sala, sadaka na majitoleo kwa ajili ya kueneza Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya huduma makini kama kielelezo cha imani tendaji. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna kurugenzi 118 za Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari zinazotekeleza dhamana na utume wake katika mataifa 140 na hivyo kuunda mtandao wa mashirika haya kimataifa. Huduma hii inaweza kuimarishwa na kuendelezwa zaidi kwa kuzingatia mambo makuu matatu: Sala, Ushuhuda na Upendo. Changamoto na mwaliko kwa waamini kushirikishana imani yao kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa kuondokana na uchoyo pamoja na ubinafsi.

Mwezi Oktoba 2019

 

09 July 2019, 15:16