Kardinali Pietro Parolin: Mkataba wa Lateran kati ya Kanisa Katoliki na Serikali ya Italia: Muhimu: Uhuru na Utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro: Kiroho, Kimaadili na Kiutu! Kardinali Pietro Parolin: Mkataba wa Lateran kati ya Kanisa Katoliki na Serikali ya Italia: Muhimu: Uhuru na Utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro: Kiroho, Kimaadili na Kiutu! 

Mkataba wa Lateran: Uhuru na utume wa Khalifa wa Mt. Petro: Kiroho, Kimaadili & Kiutu!

Kwa njia ya Mkataba wa Lateran kati ya Kanisa Katoliki na Serikali ya Italia: Khalifa wa Mtakatifu Petro na Vatican katika ujumla wake, ikapata uhuru kamili wa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili ulimwenguni kote bila ya kuingiliwa na nchi yoyote ile. Tafiti za kisayansi zimebainisha uhuru kamili wa nchi ya Vatican kujiamria mambo yake yenyewe.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Vatican ni kati ya nchi ndogo kabisa duniani na hapo tarehe 11 Februari, 2019 ilitimiza miaka 90 tangu Kanisa Katoliki lilipotiliana sahihi Mkataba na Serikali ya Italia, mkataba unaojulikana kama “Patti Lateranensi” yaani “Mkataba wa Lateran” uliotenganisha shughuli za Kanisa na Serikali ya Italia. Tangu wakati huo mambo makuu yafuatayo yamepewa kipaumbele cha kwanza:  huru wa kuabudu na wa kidini, utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Hizi ni changamoto ambazo zimepewa kipaumbele cha pekee na Vatican katika kipindi cha miaka 90 ya uwepo na utume wake. Mkataba wa Lateran uliifanya Vatican kutambuliwa rasmi kama nchi huru yenye uwezo wa kujiamria mambo yake yenyewe katika medani za kimataifa bila kuingiliwa na Serikali ya Italia. Papa Pio XI alilitaka Kanisa kuendelea kushiriki kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini Italia: kiroho na kimwili; kwa kutumia amana na utajiri wake wa kihistoria, kitamaduni na kisanaa; mambo yanayofumbatwa katika ukristo.

Kama sehemu ya kumbu kumbu ya Miaka 90 ya Mkataba wa Lateran, yaani kuanzia mwaka 1929 hadi mwaka 2019, Kitengo cha Uchapaji cha Vatican, LEV kimechapisha kitabu kinachodadavua kisayansi historia ya Mkataba wa Lateran. Kitabu hiki kimeandikwa na Kamati ya Kipapa ya Sayansi za Historia na kuhaririwa na Padre Bernard Ardura na utangulizi wake kutolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Huu ni uamuzi uliozingatia ukweli na hali ya mabadiliko yaliyokuwa yanajitokeza na Kanisa likasoma alama za nyakati, kwa kuangalia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Kardinali Parolin anafafanua kwamba, “Mkataba wa Lateran” umekuwa ni nguzo thabiti inayokita mizizi yake katika misingi ya haki, amani na maridhiano, kiasi cha kusaidia kupata suluhu ya kudumu ya mgogoro kati ya Kanisa na Serikali ya Italia kwa miaka hiyo!

Kwa njia ya Mkataba wa Lateran, Khalifa wa Mtakatifu Petro na Vatican katika ujumla wake, ikapata uhuru kamili wa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili ulimwenguni kote bila ya kuingiliwa na nchi yoyote ile. Tafiti za kisayansi zimebainisha uhuru kamili wa nchi ya Vatican kujiamria mambo yake yenyewe. Hii ikiwa ni pamoja na kutoa ulinzi na usalama kwa watu waliokuwa wanawindwa na utawala wa kifashisti wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Vatican ikasimama kidete na kuanza kutambulikana kama nchi huru kiasi hata cha kuanza kuchangia maoni katika majadiliano kuhusu: utu, heshima, haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ukawa pia ni mwanzo wa mchakato wa kukuza na kudumisha diplomasia ya Vatican katika medani mbali mbali za kimataifa.

Mtakaba wa Lateran ukawa ni msingi wa uhuru, ustawi na maendeleo ya Makanisa mahalia; viongozi wa Kanisa wakapewa dhamana na wajibu wa kuendelea kushirikiana kwa hali na mali na viongozi wa kisiasa kwa ajili ya huduma makini kwa binadamu. Papa Pio XI akalihamasisha Kanisa kusimama kidete katika maisha na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Hizi zilikuwa ni nyakati tete katika historia ya Italia iliyokuwa chini ya uongozi wa Kifashisti na viongozi wa Serikali ya Italia walilitambua fika jambo hili. Baadhi ya Makardinali kama ilivyokuwa kwa baadhi ya wanasiasa nchini Italia kwa wakati huo anasema Kardinali Parolin walikuwa wanapinga Kanisa kuwekeana mkataba na Serikali ya Italia, kila upande ukitetea masilahi yake. Lakini kwa ushuhujaa na ujasiri wa Papa Pio XI akaamua kuyakumbatia ya mbeleni kwa matumaini zaidi, ili kuimarisha uhusiano wa karibu kati ya Serikali ya Italia na Kanisa Katoliki.

Kardinali Pietro Parolin anakaza kusema katika kipindi cha miaka 90 iliyopita, Vatican imekazia umuhimu wa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuheshimu dhamiri nyofu za watu, mahali patakatifu sana katika maisha ya mwanadamu! Ikumbukwe kwamba, Haki msingi za binadamu zinazozungumziwa hapa ni zile zinavyofafanuliwa katika Tamko la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na wala si ukoloni wa kiitikadi unaotaka kupenyezwa kwa mataifa maskini duniani! Kardinali Parolin, hivi karibuni katika adhimisho la kumbu kumbu ya miaka 90 ya Mkataba huu alitumia fursa hiyo kufafanua vipengele mbali mbali vilivyomo kwenye Mkataba wa Lateran kwa kusema, kwamba, Mkataba huu, umekuwa ni ngome na ulinzi thabiti kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kuweza kutekeleza dhamana na utume wake kwa uhuru zaidi, bila kuingiliwa na chombo chochote kile!

Dhamana na wito wa Vatican katika diplomasia, unafumbatwa katika utume wake wa maisha ya kiroho, kimaadili na utu wema kwa ajili ya familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Vatican haipendi kuingilia mambo ya ndani ya nchi,  bali inapenda kusikilizwa kwa makini, kama chombo cha ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu, dhamana inayotekelezwa kwa unyoofu na unyenyekevu mkuu! Itakumbukwa kwamba, Mkataba wa Lateran, ulifanyiwa marekebisho ya msingi kunako tarehe 18 Februari 1984 wakati wa uongozi wa Mtakatifu Yohane Paulo II,  ili kuendana na Sheria, Kanuni na Taratibu zilizokuwa zimeibuliwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatican. Ushirikiano kati ya Serikali ya Italia na Vatican unajizatiti zaidi katika mchakato wa: kulinda, kudumisha na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni mkataba unaojipambanua kwa kukazia uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini.

Nchi ya Vatican inapaswa kuendelea kuwepo, ikiwa huru katika kujiamria mambo yake yenyewe, ili kutekeleza utume wake katika maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili ulimwenguni kote. Kumekuwepo na mifumo ya kisiasa na sera mbali mbali zinazogusa utu, heshima na maisha ya mwanadamu na hata wakati mwingine kuzama katika undani wake. Vatican imekuwa mstari wa mbele kukemea uhuru usiokuwa na mipaka wala uwajibikaji; imekazia majadiliano katika ukweli na uwazi na mshikamano wa kidugu. Vatican ni kati ya nchi ambazo ziko mstari wa mbele kutetea haki msingi za binadamu, kama mtu mmoja mmoja au taifa.Zote hizi ni kati ya sababu ambazo zinahalalisha uwepo wa Nchi ya Vatican ili iweze kutekeleza majukumu yake katika misingi ya ukweli na haki.

Kardinali Parolin anakaza kusema, Vatican kutokana na ushiriki wake kwenye Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kutoa mchango mkubwa unaofumbata maendeleo endelevu na fungamani binadamu pamoja na kuhakikisha kwamba, uhuru wa kuabudu na ule wa kidini unazingatiwa na kuheshimiwa na Jumuiya ya Kimataifa. Mama Kanisa anapenda kutekeleza wajibu na utume wake akiwa huru kabisa, ili kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Uhuru wa kidini ni haki ya kila dini au dhehebu lolote lile kadiri ya sheria, kanuni na taratibu za nchi husika. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wamekazia umuhimu wa Kanisa na Serikali kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya kuwahudumia watu wa Mungu: kiroho na kimwili. Uhusiano kati ya Kanisa na Serikali unategemea kwa kiasi kikubwa: hali ya kitamaduni, kijamii, kisiasa na kihistoria kwa nchi husika. Mahali ambapo utawala wa sheria unaheshimiwa, Kanisa limekuwa likitekeleza wajibu kwa ajili ya maendeleo ya watu kiroho na kimwili.

Lakini, katika baadhi ya nchi, Kanisa limekuwa likikumbana na madhulumu na sera za kibaguzi zinazolibeza Kanisa kwa kudhani kwamba, linaingilia mambo yake. Kanuni ya mpe Kaisari yaliyo ya Kaisari na Mungu yaliyo ya Mungu inapaswa kuwaongoza wanasiasa wenye misimamo mikali ya maisha. Kanisa, daima limeendelea kusoma alama za nyakati na kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro anapaswa kutekeleza dhamana na utume wake katika mazingira huru kabisa. Kamwe, Khalifa wa Mtakatifu Petro, hatasita kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; haki msingi za wakimbizi na wahamiaji pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na kwamba, misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu ni muhimu sana katika ustawi na maendeleo ya wengi! Biashara haramu ya silaha duniani, biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo ni kati ya mambo ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameyavalia njuga katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Mkataba wa Lateran

 

11 July 2019, 16:32