Tafuta

Vatican News
Mkataba wa Usalama wa Wahamiaji wa Mwaka 2018 yaani "Global Compact 2018" Unapania kulinda, kudumisha haki msingi za binadamu; utu na heshima yao kama binadamu! Mkataba wa Usalama wa Wahamiaji wa Mwaka 2018 yaani "Global Compact 2018" Unapania kulinda, kudumisha haki msingi za binadamu; utu na heshima yao kama binadamu!  (AFP or licensors)

Vatican: Usalama wa wakimbizi, utu, heshima na haki zao msingi!

Kimsingi “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji” unapania kutokomeza ubaguzi na maamuzi mbele; kuongeza fursa za ushirikishwaji wa wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani; kupunguza gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji pamoja na kuangalia umuhimu wa kutumia nguvu ya wakimbizi katika shughuli za kiuchumipamoja na suala la udhibiti wa mipaka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican

Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji wa mwaka 2018, yaani “Global Compact 2018”. Ni Mkataba unaolenga kuratibu na kuboresha mchakato wa wahamiaji na wakimbizi duniani, ili kulinda na kudumisha haki msingi, utu na heshima ya wahamiaji! Unakazia umuhimu wa jamii kusikiliza na kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji duniani; kwa kukusanya maoni; kwa kupunguza gharama za kuwahudumia wahamiaji sanjari na kudumisha usalama na kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao. Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa wahamiaji unapania pamoja na mambo mengine kuboresha: ulinzi na usalama; haki msingi za binadamu pamoja na kupatiwa huduma ya msaada wa kisheria pale haki zao zinapovunjwa. Mkataba huu unawatupia jicho wakimbizi na wahamiaji hatari kwa maisha na usalama wa raia wengine. Watu hatari wanaweza kurejeshwa makwao; uwezekano wa kudhibiti uhuru wa wakimbizi.

Kimsingi “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji” unapania kutokomeza ubaguzi na maamuzi mbele; kuongeza fursa za ushirikishwaji wa wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani; kupunguza gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambazo kwa sasa umekuwa ni mzigo mkubwa kwa baadhi ya serikali pamoja na kuangalia umuhimu wa kutumia nguvu ya wakimbizi katika kuzalisha na kutoa huduma, mwishoni ni suala la udhibiti wa mipaka! Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete kupambana kufa na kupona na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, mambo yanayonyanyasa na kudhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, hivi karibuni amesema kwamba, Mkataba wa Usalama wa Wahamiaji hauna budi kwanza kabisa kujikita katika kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji duniani.

Mkataba huu hauna budi kuboreshwa zaidi kwa kuhakikisha kwamba, Serikali husika zina kuwa na nyenzo za kisiasa ili kuweza kuratibu vyema wimbi la wakimbizi na wahamiaji duniani; kwa kuhakikisha kwamba, Serikali zinatekeleza dhamana na wajibu wake katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji. Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji kwa mwaka 2018 ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, kila upande unaweza kufaidika kwa wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kwa wakati huu. Hii inatokana na ukweli kwamba, kwa sasa wakimbizi na wahamiaji wanaonekana kuwa kama mzigo usioweza kubebeka na nchi wahisani ndiyo maana nchi kadhaa Barani Ulaya na Marekani zinaanza kufunga mipaka yake dhidi ya wakimbizi na wahamiaji. Kumbe, fursa za ajira kwa wahamiaji, ulinzi na usalama, haki msingi za wakimbizi na wahamiaji ni kati ya mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa, ili kuhakikisha kwamba, tatizo la wakimbizi na wahamiaji haramu linatoweka.

Askofu mkuu Auza anapongeza jitihada zinazofanywa na Jumuiya ya Kimataifa zinazopania pamoja na mambo mengine, kuratibu kikamilifu wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; umuhimu wa familia za wakimbizi na wahamiaji kuungana kwani tabia ya kuwatenganisha watoto na wazazi wao si kwa ajili ya ustawi wala mafao ya watoto na serikali husika kwani waathirika wakuu ni watoto na familia zao, jambo ambalo limekemewa vikali hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko. Askofu mkuu Auza anakazia mambo makuu matatu yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji kwa mwaka 2018: Mosi, Mkataba huu unapaswa kuridhiwa na nchi nyingi zaidi kwa kuzingatia kanuni sheria, taratibu na miongozo kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu, OHCHR na Shirika la Afya Duniani, WHO.

Pamoja na kuzingatia mwingiliano na ushirikiano kati ya serikali za mataifa mbali mbali duniani, mchakato unaopaswa kuzingatia misingi ya ukweli na uwazi. Pili, ni kutambua kwamba, wakimbizi na wahamiaji wote wana haki ya uhuru, unaopaswa kuheshimiwa, kulindwa na kudumishwa bila ubaguzi. Watu hawa wana haki ya kupewa huduma ya: makazi, elimu, afya pamoja na kuhakikisha kwamba, wanatendewa haki. Tatu, wakimbizi na wahamiaji wanapaswa kulindwa, kisheria, neno ambalo limeondolewa kwenye Muswada wa Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji kwa mwaka 2018. Angalisho hili linapaswa kujitokeza katika Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji wa mwaka 2018, yaani “Global Compact 2018”.  Wakimbizi na wahamiaji wanayo haki ya kubaki nchini mwao, ikiwa kama kuna amani, ulinzi na usalama pamoja na maendeleo endelevu huko wanakotoka. Mambo haya yanaweza kufikiwa, ikiwa kama yatavaliwa njuga na ikiwa kama kutakuwepo na ushirikiano kwenye Jumuiya ya Kimataifa kwa kuwajibika na kushirikishana nyajibu!

Wakimbizi: Usalama

 

09 July 2019, 07:29