Tafuta

Tarehe 14 Julai 2019: Utume wa Bahari: Mchango wa Mabaharia katika medani mbali mbali za maisha; Matatizo, changamoto na umuhimu wa kuzingatia: utu, heshima na haki zao msingi! Tarehe 14 Julai 2019: Utume wa Bahari: Mchango wa Mabaharia katika medani mbali mbali za maisha; Matatizo, changamoto na umuhimu wa kuzingatia: utu, heshima na haki zao msingi! 

Ujumbe wa Utume wa Bahari kwa mwaka 2019: Mabaharia & Wavuvi

Ujumbe wa Jumapili ya Utume wa Bahari: Mkazo: Umuhimu wa mabaharia na wavuvi katika ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya binadamu ulimwenguni. Hawa ni watu wanaofanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi na kwamba, kuna umuhimu wa kutekeleza kwa vitendo, itifaki na mikataba mbali mbali ya kimataifa kwa ajili ya mabaharia na wavuvi sehemu mbali mbali za dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni, amewataka Mapadri washauri wa kiroho pamoja na watu wa kujitolea kuendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa mabaharia pamoja na wavuvi sehemu mbali mbali za dunia, wakijaribu kuiga na kufuata mifano ya watangulizi wao. Mama Kanisa anajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Pio XI alipoanzisha Utume wa Bahari, “Stella Maris” sanjari na Kongamano la 25 la Utume wa Bahari litakaloadhimishwa huko Glasgow, nchini Scotland. Huu ni utume ulioasisiwa na waamini walei ndani ya Kanisa kama sehemu ya mchango wao wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Baba Mtakatifu anasema, Mama Kanisa anapenda kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini! Papa Pio XI alitamani sana kuona kwamba, Utume wa Bahari unaendelezwa kwenye Bahari na fukwe mbali mbali za dunia. Roho Mtakatifu, kwa maombezi ya Bikira Maria aendelee kupyaisha utume na huduma hii mintarafu mahitaji ya ulimwengu mamboleo! Kuna mabaharia ambao dhamiri zao zinahangaika sana na mara nyingi Mapadre wa maisha ya kiroho kwa mabaharia na wavuvi wamekuwa ni msaada mkubwa. Mabaharia ni watu wanaofanya kazi zao mara nyingi nje ya nchi, makazi na familia zao!

Mapadre washauri wa kiroho katika muktadha kama huu, wanakuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya matumaini kwa mabaharia na wavuvi waliopondeka na kuvunjika moyo! Mapadre wanapaswa kuwa ni watu wenye huruma, wapole na wanyenyekevu! Kwa kutambua magumu yanayowakabili mabaharia na wavuvi, Baba Mtakatifu Francisko kama ilivyokuwa kwa Wamisionari wa Huruma ya Mungu, amewapatia madaraka Mapadre wote washauri wa maisha ya kiroho kwa mabaharia na wavuvi ili kuwaondolea watu dhambi zote hata zile ambazo kimsingi, zilikuwa zimehifadhiwa kwa ajili ya Kiti Kitakatifu tu! Baba Mtakatifu anasema, lengo ni kuweza kuwapatia watu amani na utulivu wa maisha ya kiroho huko baharini!

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu anakumbusha kwamba, Jumapili ya Pili ya Mwezi Julai ya kila Mwaka, Mama Kanisa anaadhimisha Jumapili ya Utume wa Bahari na kwa mwaka 2019 imeadhimishwa tarehe 14 Julai 2019. Katika ujumbe wake amekazia mambo yafuatayo: Umuhimu wa mabaharia na wavuvi katika ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya binadamu ulimwenguni. Hawa ni watu wanaofanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi na kwamba, kuna umuhimu wa kutekeleza kwa vitendo, itifaki na mikataba mbali mbali ya kimataifa kwa ajili ya mabaharia na wavuvi sehemu mbali mbali za dunia!

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson anafafanua kwa kusema kwamba, mabaharia na wavuvi ni watu muhimu sana wanaochangia ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu ulimwenguni. Ni kundi linalosafirisha bidhaa mbali mbali zinazowaletea watu faraja, huduma, starehe pamoja na mafao yao kama watu binafsi na jamii katika ujumla wake. Jumapili ya Utume wa Bahari ni fursa ya kutafakari kwa kina na mapana mchango na huduma inayotolewa na mabaharia pamoja na wavuvi.

Waswahili wanasema eti, ukiona vinaelea ujue vimeumbwa! Watu wengi wanaweza kudanganyika na kuvutwa na hali pamoja na maisha ya mabaharia wanaosafiri sana kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine! Lakini, watu wasisahau kwamba, ni kundi la watu ambalo linafanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi na daima linakabiliwa na changamoto pevu katika utume wale. Mabaharia ni watu wanaotekeleza shughuli zao kwa sehemu kubwa wakiwa nje ya nchi na familia zao. Ni watu ambao mishahara yao inawafikia kwa kuchelewa sana na hata wakati mwingine hawapewi mishahara hadi pale wanapomaliza mikataba yao.

Vitendo vya kigaidi na uharamia baharini vimekuwa ni tishio kubwa kwa usalama wa maisha ya mabaharia na wavuvi pamoja na vyombo vyao vya kazi. Wamekuwa wakitekwa nyara na hata wakati mwingine kufunguliwa mashtaka ya uhalifu, bila kupata msaada wa kisheria wala kufaidika na mikataba pamoja na itifaki mbali mbali ambazo zimetiwa mkwaju na Jumuiya ya Kimataifa! Mabaharia na wavuvi ni watu kutoka katika mataifa, tamaduni na dini mbali mbali duniani, kiasi kwamba, ule mwingiliano na mafungamano ya kijamii yanaendelea kupungua kila kukicha.

Matokeo yake ni mabaharia na wavuvi kutumbukia katika upweke hasi unaoweza kuwasababishia kushindwa kuona umuhimu wa kazi na maisha katika ujumla wake na huu ni mwanzo wa ugonjwa sonona, kuteteleka kwa afya ya akili pamoja na kuvunjika moyo na hivyo kubomoa uhusiano mwema na familia zao, mabaharia na wamiliki wa vyombo vya kazi. Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson anakiri kwamba, katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na maboresho makubwa ya mazingira ya kazi na hali ya maisha katika ujumla wake. Lakini, bado kuna sehemu mbali mbali za dunia, ambako wamiliki wa vyombo hivi bado wanaendelea kusua sua kutekeleza sheria, mikataba na itifaki zilizokubaliwa na Jumuiya ya Kimataifa, hali inayowaathiri mabaharia na wavuvi pamoja na familia zao.

Kwa mara nyingine tena, Mama Kanisa anapenda kuchukua fursa hii ya maadhimisho ya Jumapili ya Utume wa Bahari kuyahamasisha Mashirika ya Kimataifa pamoja viongozi wa Serikali mbali mbali duniani bila kuwasahau wadau wa shughuli mbali mbali baharini kuhakikisha kwamba, wanajizatiti kikamilifu kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za wafanyakazi baharini. Mapadri washauri wa kiroho pamoja na watu wa kujitolea waendelee kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa mabaharia pamoja na wavuvi sehemu mbali mbali za dunia, wakijaribu kuiga na kufuata mifano ya watangulizi wao takribani miaka 100 iliyopita, yaani tarehe 4 Oktoba 1920.

Waamini walei wakajitosa kimasomaso kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya huduma makini kwa mabaharia na wavuvi sehemu mbali mbali za dunia. Wahudumu hawa wawe na ujasiri wa kutambua Uso wa Kristo Yesu kati ya mabaharia na wavuvi wanaokutana nao katika hija ya maisha na utume wao Baharini. Wasimame kidete: kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za mabaharia na wavuvi baharini kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko. Wawe ni mashuhuda na vyombo vya upendo wa Kristo kwa waja wake. Waendelee kushirikiana na kushikamana na wale wote wanaosimama usiku na mchana kuboresha mazingira ya kazi, kwa kuheshimu na kuthamini: utu, heshima na haki msingi za binadamu; mambo yanayoleta mafao kwa wafanyakazi wenyewe, wamiliki wa makampuni na watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu anahitimisha ujumbe wake kwa Jumapili ya Utume wa Bahari kwa kuwaweka mabaharia, wavuvi na wadau wengine wote, chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Nyota ya Bahari, ili aendelee kuwatia shime na nguvu katika utume wao!

Jumapili: Utume wa Bahari
15 July 2019, 10:28