Tafuta

Vatican News
Kardinali Bertone: Tafakari ya Fumbo la Kifo: Injili ya uhai imening'inizwa katika udhaifu wa binadamu; Ukuu wa wito na maisha ya Daraja Takatifu: Changamoto ni kukesha daima! Kardinali Bertone: Tafakari ya Fumbo la Kifo: Injili ya uhai imening'inizwa katika udhaifu wa binadamu; Ukuu wa wito na maisha ya Daraja Takatifu: Changamoto ni kukesha daima!  (AFP or licensors)

Marehemu Kardinali Sardi: Fumbo la uhai & Kifo: Wakfu katika ukweli!

Kardinali Paolo Sardi alizaliwa mwaka 1934. Akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 29 Juni 1958. Mwaka 1976 akaanza kutekeleza utume wake kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Desemba 1996 akateuliwa kuwa Askofu mkuu na kuwekwa wakfu mwaka 1997. Tarehe 23 Oktoba 2004 akateuliwa kuwa ni “Camerlengo wa Kanisa Katoliki. Tarehe 20 Novemba 2010 akateuliwa kuwa Kardinali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kifo cha Kardinali Paolo Sardi, aliyefariki dunia tarehe 13 Julai 2019, akiwa na umri wa miaka 84 ya kuzaliwa ni fursa ya kuchunguza dhamiri na kutafakari kwa kina kuhusu maana ya maisha, udhaifu wa mwanadamu na ukuu wa wito wa Daraja takatifu, Sakramenti ya upendo wa Kristo Yesu, Mchungaji mwema. Fumbo la maisha limening’inizwa katika udhaifu wa binadamu, kiasi kwamba, kifo kinawakumba wote pasi na ubaguzi. Jambo la msingi kwa kila mwamini, lakini zaidi kwa wakleri ni kuhakikisha kwamba, kila siku ya maisha yao, wanajiandaa kikamilifu ili kuweza kukabiliana na fumbo la kifo na hatimaye, kukutana na Kristo Yesu, rafiki mwema, Mkombozi wa ulimwengu, ndugu, mfano bora wa kuigwa na Kuhani mkuu wa Agano Jipya na la Milele! Kifo cha Kardinali Sardi ni nafasi ya kukumbukia Injili ya uhai; kuzama na kuongozwa na Neno la Mungu kwa kutambua kwamba, kama wakleri wamewekwa wakfu katika ukweli!

Kwa muhtasari hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu mstaafu wa Vatican wakati wa Ibada ya Misa ya mazishi ya Kardinali Paolo Sardi, iliyoadhimishwa, Jumatatu, tarehe 15 Julai 2019 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kardinali Sardi katika maisha na utume wake alikuwa ni mtumishi mwaminifu wa Mtakatifu Paulo VI, akaonesha unyenyekevu, upendo na utii mkamilifu, kiasi hata kujisadaka katika huduma bila ya kujibakiza hata kidogo. Sasa Mwenyezi Mungu amemwita kwenye makao ya uzima wa milele kwani yote yamekamilika, “Consummatum est”. Fumbo la kifo, liwe ni changamoto kwa ajili ya tafakari, kukesha na kutekeleza dhamana na nyajibu mbali mbali kwa uaminifu na ukamilifu kwa kutambua kwamba, wameteuliwa ili kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Fumbo la kifo ni fursa ya kufakari kwa kina na mapana Injili ya uhai.

Kwa ufupi, Kardinali Paolo Sardi alizaliwa tarehe 1 Septemba 1934. Akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 29 Juni 1958. Mwaka 1976 akaanza kutekeleza utume wake kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Tarehe 10 Desemba 1996 akateuliwa kuwa Askofu mkuu na kuwekwa wakfu kama Askofu tarehe 6 Januari 1997. Tarehe 23 Oktoba 2004 akateuliwa kuwa ni “Camerlengo wa Kanisa Katoliki. Tarehe 20 Novemba 2010 akateuliwa kuwa Kardinali. Baada ya kutafakari kuhusu Injili ya uhai, Kardinali Bertone amewaalika watu wa Mungu kupima maisha yao kadiri ya mwanga wa Neno la Mungu, kwa kutambua kwamba, wamewekwa wakfu kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia ukweli. Hekima anasifu tunu zake msingi, kwa kutambua uwepo wa Mungu katika hatua mbali mbali za maisha ya mwanadamu na anapokunja kilago cha maisha yake hapa duniani anatamani kukutana mubashara na Mwenyezi Mungu, ili utukufu wa Mungu uweze kung’aa zaidi na kama Kristo Yesu katika ile Sala yake ya Kikuhani anavyo waombea wafuasi wake ili waweze kutakaswa kwa ile kweli, Neno lake ndiyo kweli. Alijiweka wakfu mwenyewe, ili wafuasi wake watakaswe katika kweli.

Kardinali Paolo Sardi alikuwa Jaalimu wa maadili na utu wema. Alibahatika kufafanua kwa kina na mapana katika maisha na utume wake Wosia wa Kitume wa Mtakatifu Yohane Paulo II, “Veritatis splendor” yaani “Mng’ao wa Ukweli”. Kardinali Paolo alifafanua kwa kina maana ya: Ukweli, Uhuru, Dhamiri na Sheria na akaeleweka kwa wasikilizaji wake. Kwake, Ukweli angavu umemwilishwa katika Uso wa Kristo Yesu. Alifafanua uhuru kuwa ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Dhamiri ni mahali patakatifu ambapo Mwenyezi Mungu anazungumza na waja wake na hivyo wao kujisikia kuwa ni wana wateule wa Mungu. Sheria aliifafanua kuwa ni kielelezo cha Amri mpya ya upendo kwa Mungu na jirani! Huyu ndiye Kardinali Paolo Sardi, ambaye, Mama Kanisa amemsindikiza katika usingizi wa amani na maisha ya uzima wa milele!

kardinali Sardi
15 July 2019, 16:21