Tafuta

Utambulisho wa Elimu Katoliki: Majadiliani ya kidini, kiekumene na kitamaduni; Huduma makini kwa binadamu na ni sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina! Utambulisho wa Elimu Katoliki: Majadiliani ya kidini, kiekumene na kitamaduni; Huduma makini kwa binadamu na ni sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina! 

Utambulisho wa taasisi za elimu na vyuo vikuu vya kikatoliki duniani

Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki linasema, utambulisho wa taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za duniani unasimikwa katika: Elimu makini; Jukwaa la majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni na kwamba, elimu ni jukwaa la uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ubora na umakini wa elimu, maadili mema na tafiti za kisayansi ni kati ya mambo msingi yanayozitambulisha taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia. Lengo ni kumwandaa mwanafunzi kiutu na kimaadili, ili aweze kuwa: mwaminifu, mwadilifu na mzalendo kwa nchi yake na balozi mwema kwa Kanisa. Wasomi wanaohitimu kutoka katika taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa wanapaswa kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Kanisa Katoliki linapenda kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu kwa kutoa kipaumbele cha pekee katika mwono chanya na utambulisho wake katika sekta ya elimu, kwa kuonesha ushuhuda wenye mvuto na mashiko, unaojikita katika elimu makini inayopania kumpatia mwanadamu ukombozi kamili: kiroho na kimwili.

Kanisa linataka kuondoka na mwelekeo wa kujitafuta na kujilinda, ili kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi. Mchakato wa elimu makini pamoja na mambo mengine unakazia umuhimu wa: majiundo awali na endelevu; imani, majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; ushuhuda kutoka katika maeneo ambayo hayana uhuru kamili kuhusiana na masuala ya uhuru wa kidini; wajibu wa kuzungumza ukweli katika uwazi pasi na woga; umuhimu wa elimu katika maeneo yaliyoko pembezoni mwa jamii kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, ili elimu iweze kuwapatia ukombozi wa kweli. Kanisa linatambua kwamba elimu kimsingi, ni ufunguo wa maisha na ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu inayotekelezwa katika upendo kwa Mungu na jirani.

Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kufundwa kikamilifu ili hatimaye, waweze kujikita katika elimu inayowajengea utamaduni wa watu kukutana na kushirikiana kwa dhati katika mchakato wa maendeleo fungamani. Kanisa linataka kukuza majadiliano ya kina na wadau mbali mbali katika sekta ya elimu pasi na kupoteza utambulisho wake na badala yake kuwa kweli ni kielelezo cha ushuhuda wa huduma ya upendo inayovunjilia mbali kuta zinazowatenganisha watu kwa sababu mbali mbali. Hayo yamefafanuliwa hivi karibuni na Kardinali Giuseppe Versaldi, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki wakati wa ziara yake ya kichungaji mjini Lima, nchini Perù, wakati wa kuwasimika viongozi wakuu wapya wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Perù hivi karibuni.

Prof. Carlos Garatea Grau ndiye aliyesimikwa kuwa Mkuu mpya wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki nchini Perù. Uwepo wa Kardinali Versaldi ulipania kuimarisha ushirikiano na mshikamano kati ya Vatican na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Perù baada ya mwaka 2012, Sekretarieti kuu ya Vatican kukiondolea hadhi ya kuitwa Chuo Kikuu cha Kikatoliki. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Chuo hiki kilishindwa kuzingatia kanuni, sheria na utambulisho wa taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki. Baada ya tafakari ya kina na hatimaye, Katiba ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki Perù iliandikwa upya na kupitishwa rasmi tarehe 3 Novemba 2016 na tarehe 1 Juni 2018, hadhi yake kama Chuo Kikuu cha Kikatoliki Perù ikarejeshwa tena.

Vyuo vikuu vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki vinapaswa kuwa ni mahali pa ujenzi na ushuhuda wa upendo; mahali pa kutangaza na kumwilisha Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya uhalisia wa maisha. Jumuiya ya Chuo kikuu cha Kikatoliki iwe ni mashuhuda wa huduma ya upendo, majadiliano, heshima na kielelezo cha utambulisho wa imani inayomwilishwa katika matendo, tayari kuvunjilia mbali kuta za utengano kati ya watu! Chuo kikuu si mahali pa kupika majungu na kinzani za kijamii, bali ni eneo la kutangaza na kushuhudia kweli za Kiinjili katika maisha ya watu, tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ukombozi. Watu wanaweza kuwa na maoni na mielekeo tofauti katika maisha, lakini wote hawa wanaunganishwa na kufumbatwa na huduma na ushuhuda wa upendo!

Kardinali Giuseppe Versaldi, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki kwa muhtasari anasema: Majadiliano ya imani na kidini; huduma makini kwa binadamu; ushuhuda wa Injili ya upendo na mshikamano ni mambo msingi yanayotoa utambulisho wa taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki. Kuna umuhimu wa kukazia utambulisho wa elimu Katoliki kwani hii ni sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kuna haja ya kuendelea kujikita katika: sheria, kanuni, taratibu na Mapokeo ya Kanisa Katoliki katika sekta ya elimu. Kumbe, kuna umuhimu kwa taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vya kikatoliki kuwa na ushirikiano wa karibu zaidi na Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki, ili kukuza na kudumisha imani na matumaini, kwa kuhakikisha kwamba, elimu inayotolewa na Kanisa Katoliki inakidhi vigezo na viwango vya ubora.

Ushirikiano huu unapaswa pia kudumishwa kwa kuwashirikisha viongozi wa Makanisa mahalia, kwa kuheshimiana na kuthaminiana katika utekelezaji wa dhamana na majukumu ya taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vya Kikatoliki. Tukio hili limehudhuriwa na viongozi wakuu kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Perù pamoja na Askofu mkuu Carlos Castillo Mattasoglio wa Jimbo kuu la Lima, ambaye ameteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko.

Elimu Katoliki
20 July 2019, 10:28