Siri ya Maungano ni kiini cha Utakatifu wa Sakramenti ya Upatanisho. Siri ya Maungano ni kiini cha Utakatifu wa Sakramenti ya Upatanisho. 

Siri ya Maungamo ni kiini cha Utakatifu wa Sakramenti ya Kitubio

Upatanisho kwa wenyewe umesimamiwa kikamilifu kwa hekima na busara ya Kanisa; kwa kutumia nguvu zake zote za kimaadili na kisheria, ili kulinda na kudumisha "Siri ya Maungamo”. Hiki ni kiini cha utakatifu wa Sakramenti ya Upatanisho na kielelezo makini cha uhuru na dhamiri ya muungamaji. Mazungumzo yote yanayofanyika wakati wa maungamo yanabaki kuwa ni Siri ya Maungamo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sakramenti ya Upatanisho ni muhimu sana katika safari ya maisha ya kiroho na wongofu wa ndani unaodai toba na malipizi ya dhambi, ili hatimaye, kukiri sifa ya utakatifu wa Mungu na huruma yake kwa binadamu mdhambi. Ni kwa njia ya Sakramenti hii, mwamini hupata msamaha na amani rohoni mwake, baada ya kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zake. Lengo kuu la Sakramenti ya Upatanisho ni upatanisho na Mungu pamoja na Kanisa ambalo ni Funbo la Mwili wa Kristo. Ni katika Sakramenti ya Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu, mwamini anaonja huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu; hapa ni mahali ambapo mwamini kutoka katika undani wake, anaguswa na kupyaishwa, huku akitiwa shime ya kusonga mbele katika hija ya maisha ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.  

Hii ni Sakramenti inayopania kujenga na kudumisha mahusiano ya ndani kabisa na Mwenyezi Mungu. Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Toba ya Kitume kwa kushirikiana na Monsinyo Krzysztof Nykiel, Hakimu wa Idara ya Toba ya Kitume wametoa angalisho kuhusu umuhimu wa kuzingatia “Siri ya Mauangamo katika Sakramenti ya Upatanisho na katika maongozi ya maisha ya kiroho yanayomfunga mhudumu kimaadili, kwani hata katika huduma hii, Mama Kanisa anatekeleza kwa dhati kabisa utume unaookoa. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu ni matukio ambayo yanamwonesha Kristo Yesu kuwa ni mshindi dhidi ya dhambi na mauti.

Kwa wale wote wanao mwamini amewajengea  mahusiano thabiti na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu na hivyo kushiriki katika: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini waweze hata wao kutangaza na kushuhudia ukweli unaobubujika kutoka katika upya wa maisha kutoka kwa Yesu. Inasikitikisha kuona kwamba, ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknoloji, hayajamsaidia sana watu wengi katika maboresho ya maisha ya kijamii na kiroho, kiasi kwamba, wameanza kumsahau na kumweka Mwenyezi Mungu pembezoni kabisa mwa vipaumbele vyao. Matokeo yake ni watu kudumaa katika maisha ya kiroho, kanuni maadili na utu wema.

Haya ni maendeleo yanayotishia: maisha, utu na heshima ya binadamu. Kumekuwepo na maboresho makubwa ya mawasiliano ya jamii katika kiwango cha teknolojia, lakini kwa kiasi kikubwa hakuna upendo, kiasi kwamba, mchakato wa mawasiliano ya kijamii unakinzana na ukweli na matokeo yake ni kupingana na Mwenyezi Mungu, binadamu na Kanisa lake, ambalo ni alama ya uwepo wake endelevu. Ulimwengu wa mawasiliano unataka kujitwalia madaraka makubwa katika maisha ya watu. Haya ni mawasiliano yanayotafuta “Scoop na Breaking news” kwa kutafuta kashfa mbali mbali ili kuweza kuzianika hadharani” hasa kashfa zinazohusu maisha na utume wa Kanisa.

Hii ni mbinu mkakati inayopania kudhohofisha mchakato wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia pamoja na kusambaratisha utume wa Kanisa. Inasikitisha kuona kwamba, hata wakati mwingine, viongozi wa Kanisa wanajikuta wametumbukia katika mtego huu kwa kujiweka hadharani ili kuhukumiwa na walimwengu pamoja na kuwachafulia majina jirani zao. Mtume Paulo anawakumbusha kwamba, wameitwa ili wapate kuwa huru, lakini uhuru wao usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali watumikiane kwa upendo. Lakini wakiumana na kulana, waangalie wasije wakaumizana. Ni katika muktadha huu, Idara ya Toba ya Kitume inasikitika kusema kwamba,  kumekuwepo na mawazo potofu pamoja na maamuzi mbele dhidi ya Kanisa Katoliki hasa kutokana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia iliyolikumba Kanisa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.

Kashfa hii imewafanya baadhi ya watu kusahau asili, historia na mchango wake katika ustawi wa mtu mzima: kiroho na kimwili. Baadhi ya watu wanalitaka Kanisa litende kama Mahakama za kiraia. Idara ya Toba ya Kitume inatoa Angalisho ili kusaidia mchakato wa maboresho na uelewa makini wa mawasiliano ya kikanisa na kijamii pamoja na kuzingatia tofauti zake. Ikumbukwe kwamba, Mahakama haina haki ya kufahamu “Siri za Maungamo”; Maongozi ya maisha ya kiroho pamoja na siri ya kitaaluma. Siri ya Maungamo: Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko amekazia umuhimu wa kulinda na kutunza Siri ya Maungamo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Upatanisho kwa wenyewe umesimamiwa kikamilifu kwa hekima na busara ya Kanisa; kwa kutumia nguvu zake zote za kimaadili na kisheria, ili kulinda na kudumisha Siri ya Maungamo”.

Hiki ni kiini cha utakatifu wa Sakramenti ya Upatanisho na kielelezo makini cha uhuru na dhamiri ya muungamaji. Mazungumzo yote yanayofanyika kwenye kiti cha huruma ya Mungu; wakati wa maungamo yanabaki kuwa ni Siri ya Maungamo na kamwe hayapaswi kutoka katika kiti cha maungamo. Mwamini anapomuungamia Mwenyezi Mungu dhambi zake kwa njia ya Padre, anafunua dhamiri yake kwa Mwenyezi Mungu ili kupokea neema, utakaso na maondoleo ya dhambi. Siri ya Maungamo haiwezi kufunuliwa kwa mamlaka yoyote ya kibinadamu hapa duniani! Utunzaji wa Siri ya Maungamo unabubujika kutoka katika nguvu ya ufunuo wa Kimungu na kukita mizizi yake katika Sakramenti ya Upatanisho, kiasi kwamba, hakuna mwanya unaoweza kulegeza msimamo huu, iwe katika Kanisa  na hata katika masuala ya kiraia. Sakramenti ya Upatanisho inafumbata maana ya Ukristo na Kanisa.

Neno wa Mungu amefanyika mwili, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kanisa kama Sakramenti na chombo cha wokovu linashiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi, kwa kuwateua baadhi ya viongozi wake kuwa wahudumu wa huruma ya Mungu kwa binadamu. Mapadre wanapokuwa  wanaungamisha wanatenda kwa “In persona Christi captis” yaani “Wanatenda kwa niaba ya Kristo” ili kuwaondolea watu dhambi zao na hivyo kurejesha tena uhusiano na mafungamano yaliyovunjika kutokana na uwepo wa dhambi. Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu anawaondolea watu wake dhambi zao. Mwamini anayekimbilia kwenye kiti cha huruma ya Mungu ili kutubu na kumuungamia Mungu dhambi zake anakiri na kutambua Ukuu wa Fumbo la Umwilisho, Neema za Kanisa na Padre kama Mhudumu wa Sakramenti ya Upatanisho ambaye anatumiwa na Kristo Yesu kama chombo cha neema kwa ajili ya wadhambi wanaotubu na kumwongokea Mungu.

Kwa njia hii, Mwenyezi Mungu anagusa undani wa maisha yao na kuwaokoa. Ndiyo maana Siri ya Maungamo italindwa na waungamishaji hata ikibidi kumwaga damu yao “Usque ad sanguinis effusionem” kama kielelezo cha ushuhuda wa Siri ya Maungamo”. Siri ya Maungamo inaratibiwa na Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa na katika Katekesimu ya Kanisa Katoliki. Kutokana na uangalifu na ukuu wa huduma hi ina heshima kwa watu, Kanisa latamka kwamba, kila padre anayesikiliza maungamo anawajibika kushika siri kamili, chini ya adhabu kali sana, kuhusu dhambi ambazo wenye kutubu wameungamana. Hawezi kutumia ujuzi alioupata katika maungamano juu ya maisha ya wenye kuungama. Siri hii isiyoruhusu tofauti yoyote ile huitwa “Muhuri wa Sakramenti” kwa sababu kile ambacho mwenye kuungama amekiweka wazi mbele ya padre hubaki “kimetiwa muhuri na Sakramenti “Sigillum Sacramentale” (Rej. KKK. 1467).

Padre Muungamishaji anasikiliza dhambi za wale wanaoungama kwa niaba ya Mungu “Non ut homo, sed ut Deus”. Hata wale wanaoshirikishwa kufanya tafsiri nao wanalazimika kulinda na kutunza Siri ya Maungamano. Tunza ya Siri ya Maungamo na Utakatifu wa muungamaji ni mambo yanayopewa uzito wa pekee, kama kielelezo cha mwamini kujiachilia katika upendo wa Mungu, unaomletea toba na wongofu wa ndani. Tendo lolote la kisheria au kisiasa linalotaka kuvunjilia mbali Siri ya Maungamo ni kwenda kinyume cha uhuru wa Kanisa “Libertas Ecclesiae” unaopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si kutoka kwa taifa au serikali fulani.

Idara ya Toba ya Kitume inakaza kusema, hata mazungumzo yanayofanywa wakati wa mashauri ya kiroho nje ya Sakramenti ya Upatanisho, kimsingi hayapaswi kutolewa nje ya wahusika. Kwani hata katika mazungumzo haya, Mama Kanisa anatekeleza utume wake kwa kutumia nguvu inayookoa. Ushauri wa maisha ya kiroho ni mchakato ambao mwamini anajiaminisha katika hija yake ya maisha ya kiroho mintarafu wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha kwa padre, mtawa au mwamini mlei. Mapadre hutekeleza dhamana na utume huu kutokana na Sakramenti ya Daraja Takatifu inayompatia fursa ya kushiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo.

Waamini wanashiriki utume huu kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na Mapaji ya Roho Mtakatifu. Hata hawa wanatekeleza dhamana na wajibu wao kwa niaba ya Kristo Yesu. Washauri wa maisha ya kiroho kwa watumishi wa Mungu na wenyeheri hawaruhusiwi kutoa ushuhuda wakati wa mchakato wa kutaka kutangazwa na Mama Kanisa. Katekisimu ya Kanisa Katoliki Namba 2491 inafafanua kuhusu Siri za kitaaluma kwa wenye ofisi za kisiasa, askari, waganga na wanasheria au maelezo yanayotolewa kwa muhuri wa siri lazima yashikwe, isipokuwa kwa masuala ya pekee ambamo kushika siri kungesababisha madhara makubwa sana kwa yule aliyeiaminisha, kwa yule anayeipokea au pale madhara yanapoweza kuzuiwa kwa kutoa ukweli.

Kuna siri pia ya kipapa inayopaswa kulindwa na kuheshimiwa. Kanuni ya dhahabu ndiyo inayolinda na kuongoza ukweli huu wa mambo. Idara ya Toba ya Kitume inawahamasisha waamini kukazia ukweli, upendo wa kidugu, ukimya pale inapobidi, mafao, ustawi na usalama wa jirani zako. Waamini warekebishane na kusahihishana kwa upendo; kwa kulinda na kuheshimu utu, heshima na maisha ya jirani zao. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi ya mawasiliano ya jamii, kuna haja ya kutambua nguvu ya maneno katika kuunda na kuangamiza. Wahudumu wa Sakramenti ya Upatanisho walinde na kudumisha Siri ya Maungamo kama sehemu ya ukweli fungamani.

Siri ya Maungamo
04 July 2019, 17:46