Tafuta

Vatican News
Takwimu za Kanisa Katoliki zinaonesha kwamba, Idadi ya Mapadre wa Jimbo wanaokimbilia Ulaya na Marekani inaendelea kuongezeka kila mwaka. Takwimu za Kanisa Katoliki zinaonesha kwamba, Idadi ya Mapadre wa Jimbo wanaokimbilia Ulaya na Marekani inaendelea kuongezeka kila mwaka.  (Vatican Media)

Idadi ya Mapadre Jimbo wanaokimbilia Ulaya & USA inaongezeka!

Idara ya Takwimu za Kanisa Katoliki inaonesha kwamba, kumekuwepo pia na wimbi kubwa la Mapadre wa Majimbo kuhama kutoka Bara moja kwenda Bara jingine kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Takwimu hizi ni zile zinazohusu Mwaka 1978, mwaka 2005, Mwaka 2013 pamoja na Mwaka 2017. Ni takwimu za Mapadre wa Jimbo tu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, Kuwalinda, Kuwaendeleza na Kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, sera na mikakati hii inamwilishwa pia kwenye Makanisa mahalia, ili kuwasaidia watu hawa, ambao mara nyingi wanajikuta wakitumbukia katika biashara ya binadamu na viungo vyake, utumwa mamboleo na aina mbali mbali ya nyanyaso dhidi ya utu na heshima na haki zao msingi.

Kanisa halina budi kujipambanua kuwa ni Sakramenti ya Wokovu na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hiki ni kipindi cha kufanya mang’amuzi ya kina kwa kutambua kwamba, kuna sera na mpango mkakati unaotaka kuwasahaulisha watu changamoto kubwa ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani! Mang’amuzi haya yawe ni sehemu ya ukuaji na ukomavu wa Kanisa, unaofumbatwa katika ari na mwamko wa Kanisa kutembea pamoja ili kumwilisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Kwa njia hii, Kanisa litaweza kupyaishwa na kuendelea kuwa ni chombo cha huduma ya Injili ya upendo na mshikamano miongoni familia ya Mungu duniani!

Idara ya Takwimu za Kanisa Katoliki inaonesha kwamba, kumekuwepo pia na wimbi kubwa la Mapadre wa Majimbo kuhama kutoka Bara moja kwenda Bara jingine kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Takwimu hizi ni zile zinazohusu Mwaka 1978, mwaka 2005, Mwaka 2013 pamoja na Mwaka 2017. Hizi ni takwimu zinazowahusu Mapadre wa Majimbo peke yao, kwani si rahisi sana kupata takwimu za Mapadre wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume. Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha Mwaka 2017 zaidi ya Mapadre 19, 000 walihamia sehemu mbali mbali za dunia, ikiwa ni ongezeko la asilimia 21.3%, ikilinganishwa na Takwimu za Mwaka 2005 na zile za Mwaka 1978.

Mwenendo wa jumla unaonesha kwamba, tangu mwaka 1978 hadi mwaka 2017 Idadi ya Mapadre wa Jimbo waliokuwa wanakimbilia Barani Ulaya ilipungua kwa asilimia 38.4%, Amerika ilikuwa ni asilimia 19%, lakini kumekuwepo na ongezeko kubwa kwa Mapadre wa Jimbo kwenda Oceania kwa asilimia zaidi 123.4%, Barani Asia kwa asilimia 37.6% na Barani Afrika kwa asilimia 30.8%. Idara ya Takwimu za Kanisa Katoliki inabainishwa kwamba, Bara la Ulaya limepokea takribani nusu ya Mapadre wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia, hii ikiwa ni sawa na asilimia 36.7% ya wahamiaji wote. Bara la Amerika limepokea asilimia 36% ya Mapadre wahamiaji na Bara la Afrika limepokea walau asilimia 6.6%.

Hakuna mabadiliko makubwa na takwimu ziliohifadhiwa katika kumbu kumbu kwa Mwaka 2013, kukiwepo na ongezeko kidogo, ikilinganishwa na takwimu za mwaka 1978. Kimsingi tangu mwaka 1978 hadi mwaka 2017 kuna wastani wa Mapadre wa Jimbo asilimia 7.2% ambao wamehamia kwenye Majimbo mengine, wengi wao ni wale wanaotoka Barani Afrika na Asia. Mapadre wa Majimbo kutoka Mabara mengine kwenda Barani Afrika na Asia imekuwa ni ndogo sana na kwamba, wengi wa Mapadre wa Jimbo wamekimbilia Ulaya na Marekani. Idara ya Takwimu za Kanisa Katoliki inaangalisha kwamba, wimbi la Mapadre wa Jimbo kuhamia Ulaya na Marekani linaonekana kwamba, litaongezeka kwa siku za usoni, kumbe kuna haja ya kuhakikisha kwamba, amana na urajiri huu wa rasilimali watu unatumika vizuri zaidi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Mungu.

Kupungua kwa miito ya kitawa na kipadre Barani Ulaya na Amerika; Ongezeko la Mapadre wenye umri mkubwa Amerika na Ulaya pamoja na idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa katika nchi zilizoendelea ni sababu msingi zinazopelekea ongezeko kubwa la hitaji ya Mapadre kutoka Afrika na Asia ambako idadi ya miito ya kipadre na kitawa inaendelea kushamiri. Changamoto hii inapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa kwa kutambua kwamba, ukarimu lazima uanzie nyumbani.  Kanisa Katoliki Barani Afrika na Asia linaendelea kukua na kupanuka kwa kasi kubwa kiasi kwamba kwa miaka ya hivi karibuni, Vatican imeanzisha Majimbo mapya na Parokia zinaendelea kufunguliwa kila kukicha ili kusogeza huduma za kichungaji kwa watu wa Mungu.

Hivi karibuni katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Nchini Tanzania, Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki Geita, alisikika akisema kwamba, familia ni vitalu na chemchemi ya miito mitakatifu ya upadre, utawa na ndoa. Familia zina wajibu na dhamana ya kuhakikisha kwamba, kweli familia inakuwa ni mahali pa kutakatifuzana; mahali pa wakuwajenga na kuwafunda mashuhuda na vyombo vya uinjilishaji, huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya watu. Familia iwe ni shule ya kwanza ya malezi ya tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii. Kumbe, wazazi na walezi wanapaswa kutekeleza vyema dhamana hii kwa unyofu na uadilifu mkubwa, ili kuweza kukabiliana na changamoto za uinjilishaji katika maisha na utume wa Kanisa!

Mapadre wa Jimbo: Wahamiaji
08 July 2019, 15:58